Serikali
imekitaka Chuo cha Diplomasia kutoa taaluma ya vitendo kwa wanafunzi
wanaojiunga na chuo hicho ili kuwawezesha wahitimu kuwa na mchango katika Taifa
hususani wakati huu wa utekelezaji wa sera ya Diplomasia ya Uchumi.
Akihutubia
mahafali ya 22 ya Chuo cha Diplomasia, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) ambaye ni Mgeni Rasmi
katika mhafali hayo, amesema Serikali itafurahi kusikia chuo kinatoa mafunzo ya
stratejia, jiopolitiki na demokrasia pamoja na haki za binadamu hasa kwa
muktadha wa kiafrika.
Waziri
Kabudi ameongeza kuwa taaluma inayotolewa na Chuo hicho isiwe ya nadharia pekee
bali iambatane na vitendo ili elimu hiyo itumike kusaidia kufafanua masuala ya
Kidiplomasia na uhusiano wa Kimataifa yanayotokea duniani.
"Nakiagiza
Chuo kuandaa mpango mkakati wa mafunzo kwa vitendo ili tuangalie ni jinsi gani
Wizara inaweza kusaidia. Aidha, Chuo kipitie mitaala yake mara kwa mara kama
ilivyopendekezwa ili kisipitwe na wakati. Dunia inabadilika kwa kasi. Nasi
hatuna budi kwenda kwa kasi hiyo," Amesema Prof. Kabudi.
Prof.
Kabudi ameongeza kuwa, ni vyema Chuo kikawa mstari wa mbele kutoa mafunzo hayo
kwa wanadiplomasia, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, na wafanyabiashara
waliopo hapa nchini.
"Nimefarijika
kusikia kuwa mmefanya mazungumzo na Chuo cha ISRI cha Angola kwa nia ya kufikia
makubaliano ya kutoa mafunzo ya lugha ya Kiswahili nchini Angola ambapo rasimu
ya Hati ya Makubaliano imeandaliwa na inasubiri kusainiwa," Amesema Prof.
Kabudi.
Prof.
Kabudi aliongeza kuwa, Serikali inatambua kwamba Balozi za Iran, Libya, Urusi,
Indonesia na China zimekuwa zikitumia wigo huu wa ushirikiano na kubadilishana
uzoefu, kutoa mada mbalimbali chuoni hapo. Aidha, alitumia fursa hiyo
kuzikaribisha ofisi nyingine za kibalozi hapa nchini kutembelea Chuo cha
Diplomasia na kutoa uzoefu wao kwa vinafunzi pamoja na wakufunzi. Hivyo basi,
ni vyema menejimenti ya Chuo kutoa mwaliko kwa Balozi zote na wawakilishi wa
kudumu wa Mashirika ya Kimataifa hapa nchini kuja kutoa uzoefu wao kwani nayo
itakuwa sehemu ya diplomasia ya ulimwengu.
Awali
akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Drkt. Faraji Mnyepe amesema wahitimu 453 wametunikiwa
vyeti baada ya kupata mafunzo na kufuzu ambapo kati yao 98 ni wa ngazi ya
Astashahada ya Msingi, 119 ni wa Stashahada ya kawaida, 130 ni wa Shahada, 83
ni wa Stashahada ya Uzamili, 45 Stashahada ya uzamili wa diplomasia ya uchumi.
"Nina
imani kuwa wahitimu wa leo kama wale wa miaka ya iliyopita, wameiva ipasavyo
katika fani za mahusiano ya kimataifa, Diplomasia na Stratejia. Naamin pia kuwa
mtakuwa rasilimali kubwa kwa Taifa letu katika fani mlizosomea" Amesema
Dkt. Mnyepe.
Dkt.
Mnyepe ameongeza kuwa, katika mwaka wa masomo 2019/20 chuo kimeweza kuongeza
udahili wa wanafunzi kutoka 1029 kwa 2018/19 hadi kufikia 1275 kwa mwaka wa
masomo 2019/20 ambapo pamoja na mambo mengine juhudi zinaendelea katika kutanua
wigo wa udahili kwa kuanziasha udahili wa mwezi Machi pamoja na kuanzisha
program mpya.
"Katika mwaka wa masomo 2019/20 chuo pia
kimeweza kupanua mawanda ya program zake kwa kuongeza idadi ya program za muda
mrefu. Chuo kimeanzisha Stashahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Amani na
Udhibiti wa Migogoro ambapo kwa sasa program hii inaendeshwa Dar es Salaam na
Dodoma," Amesema Dkt. Mnyepe.
Chuo
cha Diplomasia kilianzishwa rasmi tarehe 13 Januari 1978 kwa kusainiwa
Makubaliano yaliyofanywa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi zetu mbili wa wakati
huo, Mhe. Benjamini William Mkapa wa Tanzania na Mhe. Joaquim Chissano wa
Msumbiji. Kwa miaka yote hiyo, Chuo cha Diplomasia kimejikita kuwaandaa
wanadiplomasia, wanastratejia na wabobezi wengi wa masuala ya Uhusiano wa
Kimataifa.
Chuo
kilitumika kuwaandaa wapigania uhuru wa nchi ya Msumbiji na baadae kilipanua
huduma zake na kutumika kuwaandaa pia wapigania uhuru wa nchi za Angola,
Zimbabwe, Namibia n.k.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), ambaye pia alikua mgeni rasmi wa Mahafali ya 22 ya
Chuo cha Diplomasia, Dar es Salaam, akifungua rasmi Mahafali hayo yaliyofanyika
katika viwanja vya Chuo hicho Kurasini Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika MasharikiDkt. Faraji
Mnyepe akifuatiwa na Kaimu
Mkurugenzi wa Chuo, Dkt. Jeremia Ponera.
Baadhi
ya wanafunzi wakisubiri kutunikiwa
|
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji
Mnyepe akisoma hotuba yake kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi
|
Baadhi ya wahadhiri wa Chuo cha Diplomasia wakiwa wamesimama huku wakiimba wimbo wa Taifa kabla ya kuanza
kwa mahafali
|
Baadhi ya Mabalozi na viongozi waandamizi wa Serikali
wakiwa wanaimba wimbo wa Taifa kabla ya kuanza kwa Mahafali ya 22 ya chuo cha
Diplomasia Jijini Dar es Salaam
|
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof.
Palamagamba John Kabudi (Mb), akimkabidhi zawadi mmoja kati ya wanafunzi
walifaulu vizuri masomo yake |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.