Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki imewasilisha taarifa ya utendaji kazi wake kwa kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na kusema Serikali ina
mpango wa kujenga bandari ndogo katika ziwa Tanganyika mpakani mwa Tanzania na
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema hayo
alipowasilisha taarifa taarifa ya Utekelezaji wa Wizara ya mwezi Juni
hadi Desemba 2019 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na
Usalama katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.
“Mhe. Mwenyekiti, ili kunufaika kiuchumi kupitia DRC, tumepanga kujenga bandari ndogo katika Ziwa Tanganyika na kufungua Ubalozi mdogo katika mji wa Lubumbashi, mji huu uko umbali wa kilomita 3000 kutoka jijini Kinshasa,” alisema Dkt. Ndumbaro.
Amesema ujenzi wa bandari ndogo eneo la mpakani katika Ziwa Tanganyika kutawezesha bidhaa zinazozalishwa Tanzania kwenda nchini humo kiurahisi kuliko ilivyo sasa ambapo wafanyabiashara wanapitisha biashara zao nchini Zambia hadi kufika nchini DRC.
Aidha amesema Serikali inachukua hatua mbalimbali katika maeneo ya mpaka na nchi hiyo ikiwemo kuhakikisha amani na usalama vinaimarishwa ili wananchi wa pande zote mbili wafanye biashara bila hofu yoyote.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Mussa Azzan Zungu imekutana na Menejimenti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dodoma na kupata taarifa mbalimbali za utendaji wa Wizara.
Mhe. Zungu amesisitiza umuhimu wa Tanzania kushirikiana na DRC katika kuhakikisha amani na usalama vinaimarika hata baada ya Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa (MONUSCO) kumaliza muda wake nchini humo.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.