Saturday, January 18, 2020

TANZANIA YATANGAZA UTALII UHOLANZI

Ubalozi wa Tanzania nchini Uholanzi na wadau wengine; Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro (NCAA) pamoja na makampuni binafsi kama vile, Sea-Cliff Resort & Spa Ltd, Natures Land Safari’s & Rentals na Mbalageti Safari wanashiriki Maonesho ya Kimataifa ya Utalii (Holiday Fair 2020) yanayofanyika katika mji wa Utretch, Uholanzi kuanzia tarehe 16 hadi 19 Januari 2020.

Hii ni fursa nyingine muhimu kwa Tanzania kujitangaza na kuzidi kuvutia wadau zaidi katika Sekta ya Utalii, kuja kutembelea na kufanya biashara na Tanzania. Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene F. M. Kasyanju tayari amekutana na wadau wote waliofika Uholanzi, kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika ipasavyo na maonesho hayo.

Maonesho hayo ambayo kwa lugha ya kidachi yanajulikana kama “Vakantiebeurs 2020” hufanyika mwezi Januari kila mwaka na yanahudhuriwa na mataifa mbalimbali duniani kwa lengo la kutangaza na kuuza vivutio vya Utalii na Burudani 
Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju (wa pili kushoto) akiwa na baadhi ya wawakilishi wa taasisi za Tanzania wanaoshiriki Maonesho ya Kimataifa ya Utalii nchini Uholanzi. Kutoka kushoto ni Bw. Michael Christian Makombe kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Bibi Alistidia Karaze kutoka Bodi ya Utalii Tanzania na Bw. Gerald Mono kutoka TANAPA. 
Balozi Irene Kasyanju ( wa pili kulia) akiwa na wawakilishi wa TTB na Kampuni ya MAKASA Safaris kutoka Moshi, Kilimanjaro.

Balozi Irene Kasyanju akipokea zawadi ya Kalenda za 2020 kutoka kwa Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye Maonesho hayo, Bibi Alistidia Karaze ambaye ni Afisa Mkuu wa Utafiti na Maendeleo kutoka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

Balozi Kasyanju akiwa na wawakilishi kutoka Hifadhi ya Ngorongoro, TTB, TANAPA; pamoja na Kampuni binafsi yaani, Nature’s Land Safaris & Rentals;  na Mbalageti Safari zote kutoka Mwanza, Tanzania na Sea-cliff ya Dar es Salaam.

Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi akiwa na Balozi wa Uganda nchini humo Mhe. Miriam Blaak ambaye alitembelea  kwenye Banda la Tanzania.
Mandhari ya Banda la Tanzania likionesha wateja mbalimbali wanavyolitembelea. Wateja wanaotembelea licha ya kujionea vivutio vya utalii, wanaonjeshwa pia vyakula vitamu vya Tanzania kama vile vitumbua na mandazi.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.