Tanzania
imewataka Mabalozi, Makaimu Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa
kuzingatia sheria za nchi pamoja na mikataba ya kimataifa ili kuhakikisha kuwa
wanatekeleza majukumu yao nchini kwa ufanisi na ufasaha.
Akiongea katika mkutano na Mabalozi, Makaimu
Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amesema
kuwa mahusiano ya Tanzania na nchi nyingine yanajengwa katika misingi ya
mkataba wa Viena, Mkataba wa umoja wa mataifa na sheria mbalimbali, hivyo ni
vizuri mabalozi kuzingatia taratibu hizo.
"Sisi kama tumesisitiza kuwa ni vyema mabalozi
na wawakilishi wa nchi zao wakafuata taratibu, mila pamoja na desturi zilizopo
katika mikataba hiyo ili kuhakikisha shughuli zao ndani ya Tanzania zinaendana
na kufuatana na mkataba wa Viena, mkataba wa umoja wa mataifa lakini pia kunga,
mila na desturi za kibalozi," Amesema Prof. Kabudi.
Aidha, Waziri Kabudi aliongeza kuwa Tanzania
kupitia mkutano huo imeanza ukurasa mpya wa mahusiano na uendeshaji wa shughuli
za Serikali na balozi pamoja na mashirika ya kimataifa yaliyopo Tanzania.
"………tunepata nguvu mpya baada ya mabalozi wote
kueleza kuridhika kwao kwa hali ya juu sana na hatua ambazo Serikali ya
Tanzania imechukua kupambana na rushwa, kupambana na ubadhirifu wa mali za
umma, hatua ambazo Tanzania imechukua katika kuimarisha makusanyo ya kodi
lakini pia kusimamia matumizi ya fedha za ndani pamoja na zile zinazotolewa na
nchi mbalimbali katika maendeleo ya Tanzania," Amesema Prof. Kabudi.
Katika mkutano huo, Waziri Kabudi amewahamasisha
mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa hapa nchini kuhusu kuhamia Makao
Makuu ya Nchi Dodoma kwa kuwaeleza maendeleo yaliyofikiwa kuhusu ujenzi wa
miundombinu mbalimbali muhimu na kwamba wakati umefika wa kuharakisha kuhamia
Dodoma kwa wakati muafaka kwa kuwa maendeleo yaliyofikiwa nayatoa fursa ya kuwawezesha
wao kuhamia jijini Dodoma.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mabalozi hao hapa
Nchini ambae pia ni Balozi wa Comoro Dkt. Ahamada Mohamed ameipongeza Tanzania
kwa kuitisha mkutano huo mapema ikiwa ni siku tisa tu tangu kuanza kwa mwaka
mpya wa 2020 kwa nia ya kubadilishana mawazo na kusikiliza changamoto za
mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa pia kuwaelezea hatua za utekelezaji
za masuala ya maendeleo chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli jambo
linalowapa fursa mabalozi hao kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi hapa nchini.
Nae balozi wa Kenya hapa Nchini Mhe. Dan Kazungu
ambaye pia Kiongozi wa Mabalozi wa Bara la Afrika amesema wao kama mabalozi
hawawezi kujua mipango, vipaumbele na changamoto za serikali bila ya kuelezwa
na kutaka mikutano ya namna hiyo kufanyika mara kwa mara jambo ambalo linatoa
uelewa na muelekeo wa utendaji kazi wa serikali
na hivyo kusaidia kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia kwa kutambua
fursa na changamoto zilizopo.
Awali akiwakaribisha mabalozi katika mkutano huo,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt.
Faraji Mnyepe, aliwataka mabalozi kuhakikisha kuwa wanazingatia taratibu na
kanuni za nchi ili kuhakikisha shughuli zao ndani ya Tanzania zinaendana na
kufuatana na mkataba wa Umoja wa Mataifa.
"Nawasihi sana tufanye kazi kwa kuzingatia
taratibu za nchi pamoja na sheria na mikataba kwa manufaa ya nchi yetu
(Tanzania) na nchi zenu ili tuweze kuendelea kuimarisha uhusiano wa
kidiplomasia baina yetu kwa maendeleo endelevu" Amesema Dkt. Mnyepe
Mkutano huo umehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro,Katibu Mkuu
Dkt Faraji Mnyepe na Mkuu wa Itifaki Balozi, Kanali Wilbert Ibuge, mabalozi 28,
Makaimu Mabalozi 12 na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa 10.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe akiongea na mabalozi, (hawapo pichani) wakati wa mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiongea na mabalozi, manaibu
mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa katika mkutano uliofanyika
leo jijini Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.