Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi
(Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Uwekezaji wa Norway kwa
nchi zinazoendelea (Norwegian Investment Fund for Developing Countries - Norfund),
Bw. Tellef Thorleifsson.
Mazungumzo hayo yamefanyika leo katika ofisi ndogo
za wizara Jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine, Mhe. Waziri Prof.
Kabudi pamoja na Bw. Thorleifsson wamejadili masuala yanayohusu fursa za
uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na Norway.
"Kwa kweli sisi tunafurahishwa na mradi wa Africado
ambao umewekezwa katika Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro kwani umekuwa
ukizalisha maparachichi yanayopelekwa nchi mbalimbali za Ulaya kama vile Uholanzi,
Uingereza, Ufaransa, Hispania, Ureno, na Mashariki ya Kati, na kuisaidia serikali
kukuza pato lake la taifa," Amesema Prof. Kabudi na kuongeza kuwa mradi
huo umetoa fursa za ajira takribani 600 kwa wananchi wa Tanzania.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Uwekezaji
wa Norfund, Bw. Thorleifsson amesema kuwa lengo la mkfuko huo ni kuwekeza
katika miradi mbalimbali ndani ya nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ili
kuzisaidia nchi hizo kukuza uchumi wake.
"Lengo letu ni kuwekeza katika nchi za Kusini
mwa Jangwa la Sahara ambapo hadi kufika mwishoni mwa 2018 tayari mfuko ulikuwa
umewekeza nchini Tanzania kiasi cha Dola za Marekani milioni 160 katika miradi
mbalimbali katika sekta za nishati, fedha, chakula na kilimo. Uwekezaji huo
umeifanya Tanzania kuwa nchi ya nne katika nchi zinazonufaika na miradi ya Norfund,"
amesema Bw. Thorleifsson
Norfund ni taasisi iliyo chini ya Serikali ya
Norway yenye jukumu la kuwekeza mitaji na utaalamu katika uanzishwaji wa miradi
mbalimbali endelevu kwenye nchi zinazoendelea kwa lengo la kuchangia maendeleo
ya kiuchumi na kijamii. Ziara imetoa fursa kwa pande zote mbili kuweza kujadili
namna bora ya kuboresha maeneo ya vipaumbele katika sekta ya uwekezaji.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.