Thursday, January 30, 2020

BALOZI DKT. DAU, BALOZI WA INDONESIA WAKUBALIANA KUTANGAZA UTALII WA TANZANIA


Balozi wa Tanzania nchini Malaysia Mhe Dkt Ramadhani Kitwana Dau, ambaye pia anawakilisha Indonesia amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Indonesia nchini Malaysia Mhe Rusdi Kirana na kukubaliana kutangaza fursa za utalii wa Tanzania.

Mara baada ya mazungumzo hayo, Balozi Dau alipata fursa ya kumkabidhi Mhe Balozi Kirana filamu za kutangaza utalii wa Tanzania ambapo filamu hizo zitaoneshwa kwenye ndege bila malipo yoyote kutoka ya Serikali ya Tanzania.

Mhe. Balozi Kirana ni mfanyabiashara mkubwa anaemiliki Mashirika ya ndege ya Lions Group, Batik na Malindo. Kwa pamoja, mashirika hayo yana ndege zaidi ya 300 na limeajiri wafanyakazi 43,000.

Aidha mashirika hayo yanahudumia abiria milioni 60 kwa Mwaka (wastani wa abiria 160,000 kwa Siku) na ina Safari 3,400 za kwenda na kurudi kwa Siku. Mashirika hayo yanatoa Huduma za Safari kwenye nchi zaidi ya 50 duniani.

Ubalozi wa Tanzania umemshawishi na amekubali kutangaza utalii wa Tanzania kwenye ndege zake kupitia inflight entertainment bure ambapo pamoja na mambo mengine filamu hizo zitasaidia kutangaza fursa za utalii wa Tanzania.

Katika mazungumzo yao, Mabalozi hao wamekubaliana umuhimu wa kutangaza utalii katika ukanda wa Kusini Mashariki ya Asia ambapo Balozi Kirana ameahidi kuanzisha Safari za ndege kwenda Tanzania baada ya kufanya mazungumzo na Mawakala wa utalii wa Tanzania. Balozi huyo pia ameonesha utayari wake wa kukutana na kujadiliana na mawakala wa utalii wa Tanzania kuhusu kuanzisha Safari za ndege baina ya Indonesia na Tanzania. Mkutano huo Utafanyika mwezi Februari 2020 katika Kongamano la Uwekezaji baina ya Tanzania na Indoensia (Tanzania/Indoensia Investment Forum) litakalofanyika Jijini Jakarta Indoensia tarehe 24-26 Septemba 2020.

Aidha katika mazungumzo hayo, Mhe Dkt Dau alimwalika Mhe Balozi Kirana kutembelea Tanzania Mwaliko ambao ameukubali na ameahidi kuja Tanzania katikati ya mwezi Septemba 2020.

kwa upande wake, Mhe. Balozi Kirana amemkabidhi Mhe. Balozi Dkt Dau mfano wa ndege zake kwa ajili ya kupamba ofisi.


Balozi wa Tanzania nchini Malaysia Mhe Dkt. Ramadhani Kitwana Dau akimuonesha moja kati ya filamu ya utalii Balozi wa Indonesia nchini Malaysia Mhe. Balozi Rusdi Kirana


Balozi wa Tanzania nchini Malaysia Mhe. Dkt. Ramadhani Kitwana Dau akimkabidhi moja kati ya filamu za utalii Balozi wa Indonesia nchini Malaysia Mhe Balozi Rusdi Kirana 



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.