Friday, December 27, 2019

Mhe. Waziri Kabudi akutana na kupokea nakala za Hati za Utambulisho za Mabalozi Wateule wa Algeria na Ujerumani


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amekutana, kufanya mazungumzo na kupokea nakala za Hati ya Utambulisho ya Balozi Mteule wa Algeria Mhe.  Ahmed Djellal pamoja na Balozi Mteule wa Ujerumani Mhe. Balozi Regine Hess.

Prof. Kabudi amekutana na mabalozi hao wateule leo jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine, kabla ya kukabidhiwa nakala za hati za utambulisho kukoka kwa mabalozi hao, Prof. Kabudi amefanyaa mazungumzo na Mabalozi wateule ambapo mazungumzo hayo yaliyolenga kuimarisha uhusiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria pamoja Shirikisho la Ujerumani.

Waziri Kabudi alimweleza Balozi mteule wa Algeria nchini Tanzania kuwa Tanzania na Algeria zimeendelea kuwa na uhusiano mzuri na wa kihistoria tangu miaka ya 1960 wakati wa harakati za ukombozi wa bara la Afrika dhidi ya ukoloni…"Misingi ya uhusiano wa Tanzania na Algeria ulijengwa na Waasisi wa Mataifa haya mawili, Hayati Mwl. Julius Nyerere na Hayati Ahmed Ben Bella wa Algeria," Amesema Prof. Kabudi

Waziri Kabudi ameongeza kuwa, Algeria imeendelea kuwa na Ubalozi wake hapa nchini Tanzania tangu mwaka 1964 ikiwa ni miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa kufungua ubalozi hapa nchini. Mwaka 1981 nchi hizi mbili zilianzisha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) ambayo imechangia kuimarisha na kukuza ushirikiano katika masuala mbalimbali ikiwemo diplomasia, ulinzi, elimu, madini, nishati na michezo.

 Kwa upande wake Balozi mteule wa Algeria Mhe. Balozi Ahmed Djellal ameahidi kuwa Serikali ya Algeria itaendeleza ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Tanzania hususani diplomasia, kukuza na kuimarisha biashara, uwekezaji na utalii.
"Mimi Balozi Mteule nitashughulikia na kuhakikisha kwamba uwekezaji na biashara unaofanywa kati ya Algeria na Tanzania unakuwa wa manufaa kwa pande zote mbili lengo likiwa ni kukuza sekta ya biashara hapa Tanzania" Amesema Mhe. Balozi Djellal

Katika tukio jingine, Prof. Kabudi amepokea nakala za Hati ya Utambulisho za Balozi Mteule wa Shirikisho la Ujerumani hapa nchini, Mhe. Balozi Regine Hess ambaye amemweleza Waziri Kabudi kuwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Ujerumani ni mzuri na kuongeza kuwa jukumu lake kubwa kwa sasa ni kuendeleza uhusiano huo.

Balozi Regine Hess ameyasema hayo wakati akikabidhi nakala za Hati ya Utambulisho kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb).

Balozi Regine Hess amesema kuwa mbali na uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Ujerumani, ushirikiano mzuri uliopo wa uwekejzaji, biashara, utalii na elimu utaendelea kuimarika na kutoa zaidi fursa za maendeleo kwa Tanzania.

"Kuna baadhi ya wawekezaji kutoka Ujerumaani ambao wameshaonesha nia ya kutaka kuwekeza Tanzania, hivyo nitawasiliana nao na kuweza kujua wamefikia wapi kwani Tanzania ina sifa nzuri. Jukumu langu nikiwa Balozi hapa ni kukuza na kuendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya Ujerumani na Tanzania, hivyo nitajitahidhi niwezavyo kufanikisha jukumu hilo," Amesema Balozi Hess.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akisoma nakala ya Hati ya Utambulisho mara baada ya kukabidhiwa na Balozi Mteule wa Shirikisho la Ujerumani hapa nchini katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akisoma nakala ya Hati ya Utambulisho mara baada ya kukabidhiwa na Balozi Mteule wa Shirikisho la Ujerumani hapa nchini Mhe. Balozi Regine Hess katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Balozi Mteule wa Shirikisho la Ujerumani Mhe. Balozi Regine Hess akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) kabla ya kuwasilisha nakala ya Hati ya Utambulisho. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akimkaribisha Balozi Mteule wa Shirikisho la Ujerumani Mhe. Balozi Regine Hess alipowasili katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam kuwasilisha nakala ya Hati ya Utambulisho kwa mhe. waziri 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiongea na Balozi mteule wa Algeria nchini Tanzania Mhe. Balozi Ahmed Djellal kabla ya kuwasilisha nakala ya Hati ya Utambulisho. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.




Balozi mteule wa Algeria nchini Tanzania Mhe. Balozi Ahmed Djellal akimkabidhi nakala ya Hati ya Utambulisho Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) leo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.