Friday, December 13, 2019

TANZANIA, KENYA ZAAHIDI KUENDELEZA NA KUKUZA MAENDELEO

Tanzania na Kenya zimeahidi kuendeleza na kushirikiana katika kuhakikisha kuwa maendeleo baina ya nchi hizo yanakuwa kila wakati. 

Akihutubia sherehe za maadhimisho ya 56 ya Jamhuri ya Kenya, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amesema kuwa Tanzania na Kenya ni ndugu na nchi hizo zitaendelea kushikiana katika kuhakikisha kuwa maendeleo baina ya nchi hizo yanakuwa kila wakati.

"Sisi Tanzania na Kenya ni ndugu wa damu, kwa hiyo basi tunawatakia sana kila la kheri katika kuiletea Kenya maendeleo…lakini mjue kuwa maendeleo ya Kenya ni maendeleo ya pia ya Tanzania, maendeleo pia ya Uganda, ni maendeleo pia Burundi, maendeleo pia Rwanda na Maendeleo pia ya Sudani Kusini na ni maendeleo pia ya jumuiya ya Afrika Mashariki" Amesema Prof. Kabudi

Kwa upande wake, Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa umoja na mshikamano ambao imekuwa ikionesha kwa Kenya na kusema kuwa umoja huo umekuwa ni chachu ya maendeleo kwa Tanzania na Kenya.

"Napenda kuwafahamisha kuwa umoja na mshikamano wetu umekuwa chachu ya maendeleo baina ya mataifa haya mawili…..tukumbuke kuwa umoja ni nguvu na dhamira yetu ni kushirikiana na mataifa yote duniani. Na dhamira yetu ni kuishi kwa amani umoja na mshikamano ili kukuza uchumi wetu," Amesema Balozi Kazungu

Aidha, Balozi Kazungu amebainisha kuwa Tanzania itaendelea kuwa ya kipekee kwa taifa la Kenya kutokana na mshikamano ambao imekuwa ikionesha kwa nchi ya Kenya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

"Itakumbukwa kuwa, mwezi Aprili 2019 Kenya tulipokutana na Tanzania jijini Arusha tuliweza kuondoa vikwazo vya biashara 25 kati ya 37, hii inadhihirisha ni kwa jinsi gani Kenya na Tanzania na ndugu ambao wanapenda kukuza na kuendeleza maendeleo ya biashara" ameongeza Balozi Kazungu.



Baadhi ya wageni waalikwa wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) (hayupo pichani) wakati wa maadhimisho ya miaka 56 ya Jamhuri ya Kenya jana jijini Dar es Salaam  

Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu akigonga glasi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) ikiwa ni ishara ya upendo, umoja na mshikamano baina ya nchi hizo mbili mara baada ya kuzindua rasmi maadhimisho ya miaka 56 ya Jamhuri ya Kenya jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwasilisha hotuba yake wakati wa maadhimisho ya miaka 56 ya Jamhuri ya Kenya yaliyofanyika jana jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu


Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu akihutubia hadhara iliyojitokeza wakati wa maadhimisho ya miaka 56 ya Jamhuri ya Kenya jana jijini Dar es Salaam  
Baadhi ya wageni waalikwa wakiimba nyimbo za taifa za Tanzania pamoja na Kenya kabla ya kuanza rasmi kwa sherehe za maadhimisho ya miaka 56 ya Jamhuri ya nchi hiyo.





No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.