Waziri
wa Mamb ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba
Kabudi akizungumza na waandishi wa habari (hawaako pichani), kulia ni
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge baada ya kumaliza kwa Mkutano wa
Baraza la Mawaziri wa SADC uliofanyika kwa njia ya mtandao katika Katika
Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (JNICC) jijini Dar es Salaam
Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC
uliofanyika kwa njia ya video umepitisha kwa kauli moja Mwongozo wa Kikanda wa
Urazinishaji (harmonization) na uwezeshaji wa shughuli za usafirishaji ndani ya
SADC wakati huu wa janga la Corona.
Mkutano huo pamoja na mambo mengine umepitia na kujadili masuala ya uratibu, usimamizi na uangalizi wa
usafirishaji kwa njia ya barabara katika vituo vya kuingilia, ukaguzi dhidi ya
Virusi vya Corona vinavyotambuliwa na SADC na namna ya kuendeleza shughuli za
biashara wakati huu wa janga la Corona ili kunusuru uchumi na kupunguza
umasikini ndani ya jumuiya.
Mkutano huo pia umekubaliana kuwa na
mpango wa pamoja wa kununua dawa, vifaa tiba na kinga kutoka nchini India na
kuwa na hatua za pamoja za kukabiliana na ugonjwa wa COVID 19.
Mkutano wa Baraza la Mawaziri
ulitanguliwa na Kikao cha Makatibu Wakuu
ambao waliandaa nyaraka ambazo zilitumiwa na Mkutano wa Baraza la Mawaziri na
kufikia makubaliano hayo.
Mkutano huo umekutanisha Mawaziri wenye
dhamana ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Fedha na Mipango, Viwanda
na Biashara, Uchukuzi, Utalii na Afya kutoka nchi 16 wanachama wa SADC ambazo
ni Angola, Afrika Kusini, Botswana, Comoro, DRC, Eswatini, Lesotho, Malawi,
Mauritius, Msumbiji, Madagascar, Namibia, Visiwa vya Shelisheli, Zambia,
Zimbabwe na Mwenyekiti Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.