Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb.) amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Dkt. Donald J. Wright, jijini Dodoma leo tarehe 15 Juni 2021.
Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano baina nchi hizi mbili.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Balozi Mulamula amemhakikishia Balozi Wright ushirikiano hususan kupitia Sekta muhimu ambazo nchi hizi mbili zinashirikiana kwa muda mrefu ikiwemo sekta ya afya, elimu, miundombinu, teknolojia, uwekezaji na biashara.
"Leo nimekutana na Balozi wa Marekani hapa
nchini ikiwa ni utaratibu niliojiwekea wa kukutana na Mabalozi wawanaowakilisha
nchi zao hapa Tanzania mara kwa mara kwa lengo la kubadilishana nao mawazo kuhusu namna
bora ya kuimarisha uhusiano wetu na nchi hizo. Katika mazungumzo yangu na
Balozi Wright tumejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo mpango wanaoufadhili
wa kupambana na UKIMWI wa PEPFAR na jambo kubwa amenijulisha kuwa Marekani ipo
tayari kushirikiana na Tanzania na kwamba kampuni nyingi za nchi hiyo zipo tayari
kuja kuwekeza na kufanya biashara hapa nchini wakati wowote kuanzia sasa”
alisema Balozi Mulamula.
“Pia amenifahamisha kuwa, Tanzania mwaka huu
imekuwa miongoni mwa nchi za Afrika zinazostahili kupeleka bidhaa zake za
kilimo nchini Marekani bila kutozwa ushuru kupitia Mpango wa AGOA. Hii ni fursa
muhimu kwetu na kinachotakiwa sasa ni sisi kujiimarisha katika kuzalisha bidhaa
bora zitakazokidhi vigezo vya kuingia kwenye soko la Marekani” alisisitiza Mhe. Waziri.
Kwa upande wake, Balozi Wright amemshukuru Mhe.
Balozi Mulamula kwa kumpokea na kueleza kuwa nchi yake inathamini na kuuenzi ushirikiano
wa muda mrefu uliopo kati yake na Tanzania na kwamba itaendelea kuuimarisha
ushirikiano huo kwa kuchangia sekta mbalimbali.
“Nimekuwa na mkutano mzuri na Mhe. Balozi Mulamula
na tumejadili masuala muhimu na yenye manufaa kwa nchi zetu mbili hususan
umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kupitia sekta mbalimbali. Marekani inaihesabu
Tanzania kama rafiki na mshirika muhimu hivyo mkutano huu ni moja ya jitihada
za kuimarisha ushirikiano na urafiki huo” alieleza Balozi Wright.
Maafisa kutoka Ubalozi wa Marekani walioongozana na Mhe. Balozi Wright nao wakifuatilia mazungumzo |
Mazungumzo yakiendelea |
Mazungumzo yakiendelea |
Picha ya pamoja kati ya Mhe. Waziri Mulamula na Mhe. Balozi Wright |
Picha ya pamoja |