Thursday, August 5, 2021

WATANZANIA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA NJE YA NCHI

Na Mwandishi wetu, Dar

Watanzania wamepewa changamoto ya kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana Nje ya Nchi ili waweze kuinua uchumi wao pamoja na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Changamoto hiyo imetokewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) wakati alipofanya ziara ya kutembelea Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd leo Jijini Dar es Salaam.

Balozi Mulamula amewasihi watanzania kuchangamkia fursa za masomo, masoko pamoja na biashara na uwekezaji na endapo kuna mtanzania anakwama basi asisite kuwasiliana na Wizara ili asaidiwe kupata ufumbuzi wa changamoto inayomkabili na kumwezesha kupata fursa husika.

“Fursa mbalimbali zimekuwa zikitangazwa katika Mashirika na Asasi za Kimataifa lakini watanzania wamekuwa wazito kiasi flani kuchangamkia fursa hizo, mfano fursa ya kufundisha lugha ya Kiswahili nje ya nchi, fursa ya kuuza bidhaa za kilimo nje ya nchi na nyingine nyingi………rai yangu kwa watanzania tuchangamkie fursa hizi ili tuweze kuinua kipato na uchumi wetu na taifa kwa ujumla,” amesema Balozi Mulamula

Pia Balozi Mulamula amewahakikishia ‘Diaspora’ kuwa serikali inatambua na kuthamini mchango wao na kwa sasa inaendelea kuandaa Sera ya Mambo ya Nje ili kuwawekea mazingira bora na salama ya uwekezaji nchini.

Pamoja na mambo mengine, Balozi Mulamula ameipongeza Kampuni ya Mwananchi kwa kuhabarisha na kuelimisha jamii kwa weledi wa taaluma ambao umekuwa ukiwawezesha wananchi kufahamu mambo mbalimbali yanayoendela nchini.

“Vyombo vya habari vya Mwananchi ni mdau muhimu sana kwani vimekuwa vikihabarisha na kuelimisha wadau mbalimbali mambo mazuri yanayotekelezwa na Serikali ya Tanzania,” amesema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula ameongeza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itaendelea kushirikiana kwa karibu na vyombo vya habari katika kuhakikisha kuwa vinaitambulisha vyema Serikali ya Tanzania vyema katika mataifa mbalimbali.

Balozi Mulamula ametembelea Kampuni ya Mwananchi Communications Limited wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti na kujionea shughuli zinavyofanyika pamoja na kuongea na wahariri wa Magazeti hayo. 

Tarehe 04 Juni, 2021 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula alifanya ziara yake ya kwanza katika vyombo vya habari vya habari vya IPP ambavyo ni ‘The Guardian Ltd’ inayozalisha magazeti ya The Guardian na Nipashe, Radio One, Capital radio, East Africa radio, ITV, Capital TV pamoja na East Africa TV.

1.  Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Limited Bw. Bakari Machumu akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi za Mwananchi Communications Ltd Jijini Dar es Salaam. Mwingine ni Naibu Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi, Bw. Rashid Kejo 


1.  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwaelezea jambo Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Limited Bw. Bakari Machumu pamoja na Naibu Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi, Bw. Rashid Kejo 


1.  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiangalia gazeti la Mwananchi wakati wa kikao


1.  Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Limited Bw. Bakari Machumu akimkabidhi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nakala za Magazeti ya Mwananchi, The Citizen pamoja na Mwanaspoti


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimsikiliza mmoja kati ya wafanyakazi wa mwananchi   

1.  Naibu Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi, Bw. Rashid Kejo akimuonesha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula namna magazeti yanavyohifadhiwa katika jalada maalum


Kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula na wahariri wa Mwananchi Communications Limited kikiendelea 

1.  Kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula na wahariri wa Mwananchi Communications Limited kikiendelea  



Wednesday, August 4, 2021

BALOZI MULAMULA: ZIARA YA RAIS SAMIA RWANDA IMEIMARISHA UHUSIANO WA KIDIPLOMASIA

 Na Mwandishi wetu, Dar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema moja ya mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini Rwanda ni kuimarisha uhusiano wa Kidiplomasia, kukuza biashara na uwekezaji pamoja na kuimarisha sekta ya uchukuzi baina ya Tanzania na Rwanda.

Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Waziri Mulamula amesema kuwa mbali na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, pia ziara ya Mhe. Rais nchini Rwanda nchini Rwanda ziara hiyo imekuwa kielelezo kizuri cha ujirani mwema, na imeweka msingi mzuri wa ushirikiano baina ya nchi zetu mbili katika siku za usoni na walionesha kuridhishwa kwao na hali ya uhusiano uliopo.

Pamoja na mambo mengine, Waheshimiwa Marais walikubaliana kuharakisha majadiliano kuhusu Rwanda kuongeza matumizi yake ya Mkongo wa Taifa wa Tanzania.

“Nchi zetu zilikubaliana kuhakikisha kwamba upembuzi yakinifu unaofanywa kuhusu kuanzisha kiwanda cha maziwa Mkoani Mwanza unakamilika ifikapo mwezi Septemba, 2021. Kukamilika kwa mchakato huo na kuanza kwa uwekezaji kutatoa fursa za ajira kwa vijana wetu, lakini pia kutaongeza soko kwa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa katika Kanda ya Ziwa,” amesema Balozi Mulamula.

Balozi Mulamula ameongeza kuwa Waheshimiwa Marais wamebaini fursa mbalimbali za ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda ambazo zitakuwa na manufaa kwa Serikali na wananchi ikiwemo sekta za biashara na uwekezaji na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.  

“Ziara ya Mhe. Rais Samia nchini Rwanda ililenga pia kuimarisha ushirikiano katika uendelezaji wa miundombinu ya ushoroba wa kati ambapo Serikali ya Tanzania inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha uchukuzi kupitia ushoroba wa Dar es Salaam chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, ikiwemo uboreshaji wa Bandari za Dar es Salaam na Tanga na ujenzi wa miundombinu ya reli. Jitihada hizo zinalenga kurahisisha na kupunguza muda na gharama za usafirishaji. Hivyo, Mhe. Rais aliwakaribisha wafanyabiashara na wasafirishaji kutoka Rwanda kuendelea kutumia Bandari za Tanzania, ameongeza Balozi Mulamula.

Balozi Mulamula pamoja na Mambo mengine amesema kuwa katika ziara hiyo, Mhe. Samia akiwa na mwenyeji wake Mhe. Paul Kagame walishuhudia utiaji saini wa Hati za Makubaliano ya Ushirikiano nne (4) ambazo ni ati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya Elimu, Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya TEHAMA, Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya Uhamiaji pamoja na Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya Usimamizi wa Bidhaa za Dawa.

“Waheshimiwa Marais walishuhudia pia uwekaji saini wa Tamko la Pamoja la Ziara (Joint Communique) linaloainisha maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa na kutoa mwongozo wa utekelezaji,” amesema Balozi Mulamula.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mulamula ameongeza kuwa, Rais Samia alitembelea kiwanda cha kutengeneza maji, maziwa na juisi cha Inyange, kutembelea eneo la Makumbusho la Mauaji ya Kimbari yaliyotokea nchini Rwanda Mwaka 1994 ambapo aliweka Shada la Maua kama ishara ya kumbukumbu kwawote waliopoteza maisha.

Katika ziara hiyo, Mhe. Rais Paul Kagame alielezea utayari wa Rwanda kuanza kufundisha lugha ya Kiswahili katika shule zake na hivyo watahitaji walimu wa lugha ya kiswahili.  

Katika Tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Vietnam nchini, Mhe. Nguyen Nam Tien.

Pamoja na mambo mengine, mazungumzo ya viongozi hao yalilenga kuimarisha uhusiano wa Kidiplomasia uliopo baina ya Tanzania na Vietnam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza na Waandishi wa Habari (Hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam. kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz.  


 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz.  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Balozi wa Vietnam nchini, Mhe. Nguyen Nam Tien katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

 


Kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Vietnam nchini, Mhe. Nguyen Nam Tien kikiendelea


BALOZI MULAMULA AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE MAREKANI

 Na Mwandishi wetu, Dar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anaeshughulikia masuala ya Siasa Mhe. Victoria Nuland Jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine, mazungumzo ya viongozi hao yalilenga kuimarisha uhusiano wa Kidiplomasia uliopo baina ya Tanzania na Marekani.

 Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anaeshughulikia masuala ya Siasa Mhe. Victoria Nuland akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akimuelezea jambo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anaeshughulikia masuala ya Siasa Mhe. Victoria Nuland katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Kikao baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anaeshughulikia masuala ya Siasa Mhe. Victoria Nuland kikiendelea   


Kikao baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anaeshughulikia masuala ya Siasa Mhe. Victoria Nuland kikiendelea   



Saturday, July 31, 2021

SERIKALI YA ZANZIBAR YAAPA KUULINDA MUUNGANO

 Na Mwandishi wetu, Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea kuulinda Muungano kwa kuwa ndio tunu kubwa ambayo imeachwa na waasisi wa Muungano huo na kwamba Serikali haitotumia nguvu kwa baadhi ya wananchi wenye maoni taofauti bali itawaelimisha.

Ahadi hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla wakati alipokuwa akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ulioongozwa na Waziri wa Wizara hiyo Balozi Liberata Mulamula (Mb) na kuongeza kuwa Zanzibar inatambua umuhimu wa Muungano uliopo pamoja na manufaa yake huku akitolea mfano kwa baadhi ya Wazanzibar wanaoishi Bara ambao ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameongeza kuwa kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele katika masuala ya kuimarisha uchumi na kuwaletea Wazanzibar maendeleo kutokana na umoja, amani na mshikamano uliopo tangu uwepo wa muafaka wa Serikali ya Kitaifa na kuwataka wafanyabiashara na wawekezaji kujitokeza kuwekeza visiwani humo katika sekta mbalimbali ikiwemo eneo la Uchumi wa Buluu.

Akizungumza wakati wa kujitambulisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano uliopo katika utendaji kazi na kwamba kwa sasa Wizara inaendelea na maandalizi ili kuwawezesha Viongozi wakuu wa pande zote mbili kushiriki kikamilifu katika mikutano ya Kimataifa.

Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ukiongozwa na Balozi Liberata Mulamula ambaye ameambatana na Naibu Waziri Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine pamoja na Naibu Katibu Mkuu Balozi Fatma Mohammed Rajab na baadhi ya Wakurugenzi wa Wizara hiyo uko visiwani Zanzibar kwa lengo la kujitambulisha kwa viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiongea na Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati uongozi huo ulipomtembelea Ofisini kwake Zanzibar. Uongozi wa Wizara umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, Naibu Waziri Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk, Katibu Mkuu, Balozi Joseph Sokoine, Naibu Katibu Mkuu, Balozi Fatma Mohammed Rajab pamoja na baadhi ya wakurugenzi wa Idara na vitengo vya Wizara.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akimueleza jambo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje ulipomtembelea Ofisini Kwake Zanzibar   


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akisisitiza jambo kwa Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati uongozi huo ulipomtembelea Ofisini kwake Zanzibar. Uongozi wa Wizara umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, Naibu Waziri Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk, Katibu Mkuu, Balozi Joseph Sokoine, Naibu Katibu Mkuu, Balozi Fatma Mohammed Rajab pamoja na baadhi ya wakurugenzi wa Idara na vitengo vya Wizara.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na  Naibu Waziri Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk




Thursday, July 29, 2021

DKT MWINYI ATOA MAELEKEZO KWA WIZARA YA MAMBO YA NJE

Na Mwandishi wetu, Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kipaumbele cha Serikali yake hususani katika sekta ya mafuta na gesi,Utalii,Uvuvi Biashara na Uwekezaji ni katika Uchumi wa Buluu ambao utamsaidia Mzazibar katika kuimarisha kipato pamoja na kuondoa kodi za kero kwa Wanzazibar.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa juu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ulioongozwa na Waziri wa Wizara hiyo Balozi Liberata Mulamula (Mb) kwa lengo la kujitambulisha na kupokea maelekezo ya kutekeleza  vipaumbele vya Serikali ya mapinduzi Zanzibar.

Dkt. Mwinyi ameilekeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutilia mkazo katika uwekezaji wa maeneo ya Uchumi wa Buluu katika mazungumzo na Mashirika ya fedha duniani ikiwemo IMF na Benki ya dunia ikiwa ni pamoja na wawekezaji na wafadhili mbalimbali kwa kuwa Serikali yake ina imani kuwa bahari ikitumiwa vizuri itainufaisha Zanzibar kiuchumi kuliko maeneo mengine.

Pia Dkt. Mwinyi ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuwasaidia wafanyabiashara kutoka Zanzibar kwa kuwaunganisha na wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nje ili Zanzibar nayo iweze kusafirisha bidhaa zake za ndani kwenda nje badala ya kupokea bidhaa kutoka mataifa mengine kama ilivyo sasa.

Dkt. Mwinyi amezitaja bidhaa kutoka Zanzibar zinazoweza kusafirishwa Nje ya Zanzibar kuwa ni pamoja na karafuu,samaki na nyama ambazo zina soko kubwa nje ya nchi hususani katika nchi za Kiarabu.

Mbali na hilo Dkt. Mwinyi ametaka kupitiwa upya kwa Sera ya Mambo ya Nje ya Nchi hususani katika suala Wazanzibar wanaoishi nje maarufu kama Diaspora ikiwemo kupatiwa hadhi maalum itakayowawezesha kushiriki katika uchumi wa nchi ikiwemo kuwekeza,kubadilishana uzoefu wa kitaaluma na masuala mengine ya maendeleo.

Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amesema Wizara imeyapokea maelekezo ya Rais Dkt Hussein na kwamba tayari kuna mkakati na maelekezo maalum kwa Mabalozi wanaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mataifa mbalimbali duniani ili kuhakikisha mahusiano ya Tanzania na Nchi hizo yanakuwa ya manufaa katika uchumi wa pande zote za Jamuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika tukio jingine Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula na ujumbe wake wamekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa kwanza wa Rais Mhe. Othman Masoud Othman ambaye kwa upande wake ameeleza nia ya Ofisi yake katika kupambana kudhibiti biashara na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na suala la mazingira ambayo kwa kiasi kikubwa yameathirika kutokana na mabadiliko ya Tabia nchi jambo ambalo linatishia uhai wa Visiwa mbalimbali duniani ikiwemo Zanzibar.

Katika tiara hiyo Balozi Mulamula ameambatana na Naibu Waziri Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine, Naibu Katibu Mkuu Balozi Fatma Mohammed Rajab pamoja na baadhi ya Wakurugenzi wa Idara na Vitengo vya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula alipokuwa Ikulu - Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiongea na uongozi wa juu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ulioongozwa na Waziri wake Mhe. Balozi Liberata Mulamula walipokuwa Ikulu - Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na Katibu wa baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi - Zanzibar na Uongozi wa juu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ukiongozwa na Waziri wake Mhe. Balozi Liberata Mulamula. wengine ni Naibu Waziri, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Katibu Mkuu, Balozi Joseph Sokoine pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Balozi Fatma Mohammed Rajab

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wakuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Uongozi wa Wizara umeongozwa na Mhe. Waziri, Balozi Liberata Mulamula (Mb) na kuwataka kuandaa mpango maalumu wa kushirikiana na Zanzibar kwa lengo la kuendelea kuitangaza na kuboresha uhusiano wake na nchi mbalimbali duniani

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, akizungumza na viongozi wakuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Uongozi wa Wizara umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Liberata Mulamula (Mb), Naibu Waziri, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Katibu Mkuu, Balozi Joseph Sokoine pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Balozi Fatma Mohammed Rajab katika ziara rasmi ya kujitambulisha kwa Viongozi Waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.  


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman katika picha ya pamoja na  viongozi wakuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Uongozi wa Wizara umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Liberata Mulamula (Mb), Naibu Waziri, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Katibu Mkuu, Balozi Joseph Sokoine pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Balozi Fatma Mohammed Rajab. 





  



Wednesday, July 28, 2021

WAZIRI MULAMULA AMUAGA BALOZI WA UHOLANZI

 Na mwandishi wetu, Dar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amemuaga Balozi wa Uholanzi nchini, Mhe. Jeroen Verheul ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi.

Balozi Mulamula amempongeza Balozi Verheul kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kudumisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Uholanzi na Tanzania wakati wote wa uwakilishi wake hapa nchini.

“Tanzania tunakuahidi ushirikiano lakini pia tunakutakia kila la kheri katika maisha yako nje ya Tanzania na ni imani yangu kuwa utakuwa balozi mzuri wa Tanzania duniani," Amesema Balozi Mulamula

Balozi wa Uholanzi aliyemaliza muda wake wa Uwakilishi Mhe. Verheul ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano iliompatia wakati wote alipokuwa akitekeleza majukumu yake ya uwakilishi hapa nchini.

“Nawashukuru sana kwa ushirikiano mlionipatia wakati wote niliokuwa hapa nikitekeleza majukumu yangu kama Balozi, hakika nilifarijika sana……….Ninawaahidi kuwa balozi mwema kote niendako,” Amesema Balozi Verheul

Katika tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Mhe. Khalifa Abdulrahman Mohamed Al-Marzooqi katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao walijadili masuala ya kukuza, kuimarisha na kudumisha uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na UAE.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza na Balozi wa Uholanzi nchini, Mhe. Jeroen Verheul wakati wa hafla ya kumuaga mara baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. 


Balozi wa Uholanzi nchini, Mhe. Jeroen Verheul akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Libarata Mulamula akimkabidhi moja kati ya zawadi Balozi wa Uholanzi nchini aliyemaliza muda wake wa uwakilishi nchini, Mhe. Jeroen Verheul


Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Mhe. Khalifa Abdulrahman Mohamed Al-Marzooqi akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Libarata Mulamula wakati walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Libarata Mulamula akiongea na Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Mhe. Khalifa Abdulrahman Mohamed Al-Marzooqi wakati walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Libarata Mulamula na Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) hapa nchini Mhe. Khalifa Abdulrahman Mohamed Al-Marzooqi yakiendelea



Tuesday, July 27, 2021

AWLN, TAASISI YA MWALIMU NYERERE ZAPEWA CHANGAMOTO YA KUSIMAMIA AMANI AFRIKA

 Na Mwandishi wetu, Dar

Mtandao wa Uongozi wa Wanawake Afrika (AWLN) kwa kushirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere umepewa changamoto ya kukuza na kusimamia masuala ya umoja na amani katika Bara la Afrika ili kuleta maendeleo ya watu.  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ametoa wito huo wakati alipokutana na Mtandao huo pamoja na Taasisi ya Mwalimu Nyerere ikishirikiana na Shirika la Kimataifa la kutetea Haki na Maendeleo ya Wanawake (UN Women) leo jijini Dar es Salaam

“Agenda yetu ni muhimu, hamuwezi kusema kuwa tuna maendeleo kama hakuna amani…….amani ni sehemu ya Diplomasia ya Uchumi, kama amani huwezi kuitafuta kwa njia nyingine tuseme amani ni maendeleo na maendeleo ni amani,” Amesema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula ameongeza kuwa, kwa kuzingatia kwamba amani ni matokeo ya haki juhudi zinahitajika katika kuhamasisha na kuunga mkono ushiriki kamili wa wanawake kama wadau muhimu wa kulinda na kutetea amani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Bw. Joseph Butiku amesema kuwa Taasisi yake ina jukumu la kuhakikisha kuwa amani na haki zinapatikana hasa katika ukanda wa Maziwa Makuu.

“Tumepokea changamoto tuliyopewa na Mhe. Waziri na mimi ninakubaliana na yeye kabisa kuwa tushirikiane na wanawake katika kuhamasisha na kutunza amani na haki hasa kwa kushirikiana na wanawake ambao wamekuwa na mchango mkubwa sana wa kutunza amani na kuwa hakuna mpaka na yote yanawezekana,” Amesema Bw. Butiku.

Mtandao wa Uongozi wa Wanawake Afrika (AWLN) na UN Women umekuwa ukishirikiana katika kuisaidia Tanzania kuandaa Mpango kazi wa Kitaifa wa Utekelezaji wa ajenda ya wanawake, amani na usalama ya Maamuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Na. 1325.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Bw. Joseph Butiku akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (wa kwanza kulia), Mtandao wa Uongozi wa Wanawake Afrika (AWLN) pamoja na baadhi pamoja na baadhi ya viongozi wa Shirika la Kimataifa la kutetea Haki na Maendeleo ya Wanawake (UN Women) leo jijini Dar es Salaam 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiongea na baadhi ya viongozi na maafisa wa Mtandao wa Uongozi wa Wanawake Afrika (AWLN) pamoja na Taasisi ya Mwalimu Nyerere (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiongea na baadhi ya viongozi na maafisa wa Mtandao wa Uongozi wa Wanawake Afrika (AWLN) pamoja na Taasisi ya Mwalimu Nyerere leo jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na viongozi na maafisa wa Mtandao wa Uongozi wa Wanawake Afrika (AWLN) wafanyakazi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere pamoja na Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki 



Friday, July 23, 2021

SERIKALI YAWATOA HOFU MABALOZI KUHUSU MAPAMBANO YA UVIKO 19

 Na Mwandishi wetu, Dar

Serikali imewaeleza Mabalozi njia mbalimbali inazozitumia kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona ikiwa ni pamoja na kuridhia uingizwaji wa chanjo ya Uviko 19 kwa Balozi, Taasisi na Mashirika ya Kimataifa yanayotaka kufanya hivyo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amewaeleza baadhi ya Mabalozi wanaotoka katika nchi za Kiislamu wakati alipokutana nao kwa ajili ya kuhitimisha sherehe za Eid El Haj leo jijini Dar es Salaam.

Pia Balozi Mulamula amefafanua kuhusiana na maswali aliyokuwa akiulizwa na baadhi ya mbalozi juu ya chanjo ya kukabiliana na ugonjwa wa Uviko 19 na kusema kuwa hakuna Balozi, Taasisi au Mashirika ya Kimataifa yalizuiliwa kuingiza chanjo kwaajili ya kuwachanja watu wao na kuwasihi kutoa taarifa kwa wizara ya Afya ili kuwezesha namna bora ya kuratibu na kupokea chanjo hizo.

“…….Naomba niwahakikishie waheshimiwa mabalozi kuwa Serikali yetu ni sikivu sana, nimekuwa nikiulizwa maswali mbalimbali kuhusu uingizwaji wa chanjo kwa ajili ya kuwachanja watumishi katika balozi zenu hapa nchini ila naomba msisite kuwasiliana na Wizara ya Afya kwa ajili ya kuratibu njia bora ya kupata chanjo hiyo,” Amesema Balozi Mulamula.

Katika tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Canada nchini Mhe. Pamela O'Donnell pamoja na Balozi wa Uingereza nchini Mhe. David Concar.

Balozi Mulamula amekutana na mabalozi hao kwa nyakati tofauti katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ambapo awali amekutana na Balozi wa Canada nchini, Mhe. Pamela O'Donnell akifuatiwa na Balozi wa Uingereza nchini Mhe. David Concar kwa lengo la kujadiliana masuala mbalimbali ya uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na nchi zao.  

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa uwili (Bilateral Cooperation).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akimsikiliza Balozi wa Palestina nchini, Mhe. Hamdi Mansour wakati alipokutana na Mabalozi wanaotoka katika nchi za Kiislamu kwa ajili ya kuhitimisha sherehe za Eid El Haj leo jijini Dar es Salaam 


Balozi wa Visiwa vya Comorro nchini, Mhe. Dkt. Ahmada El Badaoui Mohammed akimkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika hafla kuhitimisha sherehe za Eid El Haj leo jijini Dar es Salaam 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea na Mabalozi wanaotoka katika nchi za Kiislamu alipokutana nao kwa ajili ya kuhitimisha sherehe za Eid El Haj leo jijini Dar es Salaam 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Mohammed Rajab pamoja na baadhi ya Wakurugenzi wa Idara mbalimbali za Wizara wakiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi wanaotoka katika nchi za Kiislamu  mara baada ya kuhitimisha sherehe za Eid El Haj leo jijini Dar es Salaam 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Balozi wa Canada hapa nchini Mhe.  Pamela O'Donnell wakati walipokutana kwa Mazungumzo katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. David Concar wakati walipokutana kwa Mazungumzo katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam