Tuesday, July 27, 2021

AWLN, TAASISI YA MWALIMU NYERERE ZAPEWA CHANGAMOTO YA KUSIMAMIA AMANI AFRIKA

 Na Mwandishi wetu, Dar

Mtandao wa Uongozi wa Wanawake Afrika (AWLN) kwa kushirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere umepewa changamoto ya kukuza na kusimamia masuala ya umoja na amani katika Bara la Afrika ili kuleta maendeleo ya watu.  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ametoa wito huo wakati alipokutana na Mtandao huo pamoja na Taasisi ya Mwalimu Nyerere ikishirikiana na Shirika la Kimataifa la kutetea Haki na Maendeleo ya Wanawake (UN Women) leo jijini Dar es Salaam

“Agenda yetu ni muhimu, hamuwezi kusema kuwa tuna maendeleo kama hakuna amani…….amani ni sehemu ya Diplomasia ya Uchumi, kama amani huwezi kuitafuta kwa njia nyingine tuseme amani ni maendeleo na maendeleo ni amani,” Amesema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula ameongeza kuwa, kwa kuzingatia kwamba amani ni matokeo ya haki juhudi zinahitajika katika kuhamasisha na kuunga mkono ushiriki kamili wa wanawake kama wadau muhimu wa kulinda na kutetea amani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Bw. Joseph Butiku amesema kuwa Taasisi yake ina jukumu la kuhakikisha kuwa amani na haki zinapatikana hasa katika ukanda wa Maziwa Makuu.

“Tumepokea changamoto tuliyopewa na Mhe. Waziri na mimi ninakubaliana na yeye kabisa kuwa tushirikiane na wanawake katika kuhamasisha na kutunza amani na haki hasa kwa kushirikiana na wanawake ambao wamekuwa na mchango mkubwa sana wa kutunza amani na kuwa hakuna mpaka na yote yanawezekana,” Amesema Bw. Butiku.

Mtandao wa Uongozi wa Wanawake Afrika (AWLN) na UN Women umekuwa ukishirikiana katika kuisaidia Tanzania kuandaa Mpango kazi wa Kitaifa wa Utekelezaji wa ajenda ya wanawake, amani na usalama ya Maamuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Na. 1325.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Bw. Joseph Butiku akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (wa kwanza kulia), Mtandao wa Uongozi wa Wanawake Afrika (AWLN) pamoja na baadhi pamoja na baadhi ya viongozi wa Shirika la Kimataifa la kutetea Haki na Maendeleo ya Wanawake (UN Women) leo jijini Dar es Salaam 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiongea na baadhi ya viongozi na maafisa wa Mtandao wa Uongozi wa Wanawake Afrika (AWLN) pamoja na Taasisi ya Mwalimu Nyerere (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiongea na baadhi ya viongozi na maafisa wa Mtandao wa Uongozi wa Wanawake Afrika (AWLN) pamoja na Taasisi ya Mwalimu Nyerere leo jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na viongozi na maafisa wa Mtandao wa Uongozi wa Wanawake Afrika (AWLN) wafanyakazi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere pamoja na Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki 



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.