Friday, July 2, 2021

WIZARA YA MAMBO NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI YAVUTIWA NA KASI YA UJENZI WA SGR


Wizara ya Mambo ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inajivunia na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa reli mpya ya kisasa (Standard Gauge Railway - SGR) unaoendelea katika hatua mbalimbali nchini. 

Haya yamesemwa na Bw. Eliabi Chodota Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii,alipotembelea mradi huo ambao kwa sasa ndio mradi pekee mkubwa wa reli ya kisasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ameongeza kuwa mradi huu sio tu ni muhimu kwa Tanzania bali utazinufaisha pia nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki na nchi zingine jirani. Bwana Chodota pia ameeleza kuridhishwa kwake na ushiriki wa Watanzania katika katika ujenzi wa mradi huo, ambapo kati ya Wafanyakazi zaidi ya 6000, zaidi ya asilimia 80 ni Watanzania. 

Bwana Chodota ametembelea maradi huo unaotekelezwa katika awamu tano (5) kama ifuatavyo: sehemu ya awamu ya kwanza Kilomita 202 (Dar es Salaam-Morogoro), awamu ya pili Kilomita 348 (Morogoro – Makutopora) awamu ya tatu Kilomita 294 (Makutopora-Tabora) awamu ya nne (Tabora-Isaka), na sehemu ya awamu ya tano Kilomita 341 (Isaka-Mwanza) kwa lengo la kujionea hatua ya maendeleo iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo.

Mradi huu wa SGR, unaoendelea kujengwa kwa kasi, baada ya kukamilika kwake unatarajiwa kuiunganisha Tanzania na nchi jirani za Rwanda na Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Reli hii mpya inatarajiwa kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya usafiri na usafirishaji nchini kwa kupunguza msongamano barabarani, kupunguza muda wa kusafiri na kupunguza uharibifu wa miundombinu ya barabara. Sambamba na hayo, pia inatarajiwa kupunguza gharama za usafirishaji kwa 40%. Kila treni ya mizigo inatarajiwa kusafirisha hadi tani 10,000 kiasi ambacho kinaweza kusafirishwa na malori 500 kwa njia ya barabara.

Bwana Chodota ametoa rai kwa Watanzania hasa ambao wanazunguka eneo la mradi kuendelea kutoa ushirikiano kwa mamlaka na Mkandarasi ili kuendelea kuruhusu kasi ujenzi wa mradi iendelee na kuweka mazingira rafiki na salama kwa mradi huo wakati wote.
Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Bw. Eliabi Chodota (wa kwanza kushoto) wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa katika kituo cha reli ya kisasa SGR cha mjini Morogoro muda mfupi baaada ya kuwasili katika kituo hicho. Wengine pichani ni Watumishi wa Wizara na Shirika la Reli Nchini.
Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Bw. Eliabi Chodota (wa kwanza kulia) akifuatilia maelezo ya Waandisi wa ujenzi wa mradi wa SGR.
Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Bw. Eliabi Chodota (wa pili kushoto) akifuatilia maelezo ya Waandisi wa ujenzi wa mradi wa SGR katika Kituo Kikuu cha mradi huo jijini Dar es Salaam
Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Bw. Eliabi Chodota (mwenye tai) akiwa na baadhi ya watumishi wa Wizara na Shirika la Reli nchini kwenye kituo cha SGR cha Soga.
Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Bw. Eliabi Chodota (mwenye tai) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Wizara aliombatana nao katika ziara ya kutembelea mradi wa SGR.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.