Thursday, July 8, 2021

TANTRADE, BALOZI ZA TANZANIA ZAELEKEZWA KUTANGAZA FURSA ZA BIASHARA

Na Mwandishi wetu, Dar

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeelekezwa kushirikiana na Balozi za Tanzania katika kutangaza fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji hapa nchini.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab wakati alipotembelea Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

“…………….Balozi zetu zina uhusiano wa karibu na TanTrade ambapo TanTrade moja kati ya majukumu yake ni kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wetu hapa nchini wanapata taarifa sahihi ili kusaidia kujua ni bidhaa gani za Tanzania zinaweza kuuzwa nje kwa urahisi lakini pia kujua ni nchi husika yenye uhitaji wa bidhaa hizo,” amesema Balozi Fatma 

Balozi Fatma ameongeza kuwa ili bidhaa za Tanzania ziendelee kuuzwa katika masoko ya kimataifa ulimwenguni, TanTrade iendelee kushirikiana kwa karibu na Balozi za Tanzania katika kuhakikisha kuwa inatoa taarifa sahihi za bidhaa.

“Ushirikiano baina ya TanTrade na Balozi zetu uendelee kuimarishwa ili kuwawezesha wafanyabiashara kupata taarifa sahihi na kwa wakati, lakini pia ushirikiano huu utasaidia kutangaza fursa za biashara zilizopo nchini Tanzania katika Mataifa ya Kigeni,” amesema Balozi Fatma

Balozi Fatma pia ametoa wito kwa watanzania kutumia fursa ya maonesho ya Sabasaba kujifunza kutoka kwa wafanyabiashara kutoka nje ya Nchi walioshiriki katika maonesho hayo ili kujua ni kwa namna gani wataweza kunufaika na fursa za kuuza bidhaa zetu kwenye nchi za kimataifa

“Kupitia maonesho haya watanzania watumie fursa hii kujifunza kutoka kwa wafanyabiashara kutoka nje ya Nchi walioshiriki katika maonesho haya, lakini pia kuangalia ni namna gani watanufaika na fursa za kuuza bidhaa zetu kwenye nchi za kimataifa,” Amesema Balozi Fatma Rajab. 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akisaini kitabu cha wageni katika banda la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alipotembelea banda la Wizara katika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere Dar es salaam 


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akipokea nakala ya Jarida la Diplomasia linalochapishwa na  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alipotembelea banda la Wizara katika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere Dar es salaam 


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akimsikiliza mtumishi wa Wizara alipokuwa akimpatia maelezo juu ya baadhi ya viongozi (Mawaziri) waliohudumu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki tangu mwaka 1961 hadi sasa mwaka 2021


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akiongea na waandishi wa habari wakati alipokuwa katika banda la Wizara katika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere Dar es salaam 


Afisa kutoka Tume ya Utalii Zanzibar akimfafanulia jambo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab wakati alipotembelea banda la tume hiyo katika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere Dar es salaam 


Afisa kutoka Bodi ya Mapato Zanzibar akimuelezea jambo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab wakati alipotembelea banda la Bodi hiyo katika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere Dar es salaam




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.