Wednesday, August 4, 2021

BALOZI MULAMULA: ZIARA YA RAIS SAMIA RWANDA IMEIMARISHA UHUSIANO WA KIDIPLOMASIA

 Na Mwandishi wetu, Dar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema moja ya mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini Rwanda ni kuimarisha uhusiano wa Kidiplomasia, kukuza biashara na uwekezaji pamoja na kuimarisha sekta ya uchukuzi baina ya Tanzania na Rwanda.

Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Waziri Mulamula amesema kuwa mbali na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, pia ziara ya Mhe. Rais nchini Rwanda nchini Rwanda ziara hiyo imekuwa kielelezo kizuri cha ujirani mwema, na imeweka msingi mzuri wa ushirikiano baina ya nchi zetu mbili katika siku za usoni na walionesha kuridhishwa kwao na hali ya uhusiano uliopo.

Pamoja na mambo mengine, Waheshimiwa Marais walikubaliana kuharakisha majadiliano kuhusu Rwanda kuongeza matumizi yake ya Mkongo wa Taifa wa Tanzania.

“Nchi zetu zilikubaliana kuhakikisha kwamba upembuzi yakinifu unaofanywa kuhusu kuanzisha kiwanda cha maziwa Mkoani Mwanza unakamilika ifikapo mwezi Septemba, 2021. Kukamilika kwa mchakato huo na kuanza kwa uwekezaji kutatoa fursa za ajira kwa vijana wetu, lakini pia kutaongeza soko kwa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa katika Kanda ya Ziwa,” amesema Balozi Mulamula.

Balozi Mulamula ameongeza kuwa Waheshimiwa Marais wamebaini fursa mbalimbali za ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda ambazo zitakuwa na manufaa kwa Serikali na wananchi ikiwemo sekta za biashara na uwekezaji na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.  

“Ziara ya Mhe. Rais Samia nchini Rwanda ililenga pia kuimarisha ushirikiano katika uendelezaji wa miundombinu ya ushoroba wa kati ambapo Serikali ya Tanzania inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha uchukuzi kupitia ushoroba wa Dar es Salaam chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, ikiwemo uboreshaji wa Bandari za Dar es Salaam na Tanga na ujenzi wa miundombinu ya reli. Jitihada hizo zinalenga kurahisisha na kupunguza muda na gharama za usafirishaji. Hivyo, Mhe. Rais aliwakaribisha wafanyabiashara na wasafirishaji kutoka Rwanda kuendelea kutumia Bandari za Tanzania, ameongeza Balozi Mulamula.

Balozi Mulamula pamoja na Mambo mengine amesema kuwa katika ziara hiyo, Mhe. Samia akiwa na mwenyeji wake Mhe. Paul Kagame walishuhudia utiaji saini wa Hati za Makubaliano ya Ushirikiano nne (4) ambazo ni ati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya Elimu, Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya TEHAMA, Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya Uhamiaji pamoja na Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya Usimamizi wa Bidhaa za Dawa.

“Waheshimiwa Marais walishuhudia pia uwekaji saini wa Tamko la Pamoja la Ziara (Joint Communique) linaloainisha maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa na kutoa mwongozo wa utekelezaji,” amesema Balozi Mulamula.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mulamula ameongeza kuwa, Rais Samia alitembelea kiwanda cha kutengeneza maji, maziwa na juisi cha Inyange, kutembelea eneo la Makumbusho la Mauaji ya Kimbari yaliyotokea nchini Rwanda Mwaka 1994 ambapo aliweka Shada la Maua kama ishara ya kumbukumbu kwawote waliopoteza maisha.

Katika ziara hiyo, Mhe. Rais Paul Kagame alielezea utayari wa Rwanda kuanza kufundisha lugha ya Kiswahili katika shule zake na hivyo watahitaji walimu wa lugha ya kiswahili.  

Katika Tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Vietnam nchini, Mhe. Nguyen Nam Tien.

Pamoja na mambo mengine, mazungumzo ya viongozi hao yalilenga kuimarisha uhusiano wa Kidiplomasia uliopo baina ya Tanzania na Vietnam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza na Waandishi wa Habari (Hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam. kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz.  


 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz.  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Balozi wa Vietnam nchini, Mhe. Nguyen Nam Tien katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

 


Kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Vietnam nchini, Mhe. Nguyen Nam Tien kikiendelea


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.