Tuesday, August 31, 2021

UYOGA WA TANZANIA KUPATA SOKO NCHINI UHOLANZI

Balozi Irene Kasyanju (katikati) akiwa katika mazungumzo na uongozi wa LIMAX Group ulioongozwa na Mkurugenzi na Mmiliki wa Kampuni hiyo, Bw. Tom van WALSEM (wa pili kushoto) kuhusu soko la uyoga wa Tanzania nchini Uholanzi kwenye Ofisi za Kampuni hiyo zilizopo katika Mji wa Horst, Uholanzi. LIMAX Group inazalisha faida/pato kwa mwaka (annual turnover) la takriban Euro milioni 25. 

Balozi Irene Kasyanju (kulia) akiangalia namna uyoga unavyofungashwa kwenye makasha (packaging) tayari kwa kupelekwa sokoni huku akipatiwa maelezo ya mchakato mzima wa ufungaji kutoka kwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa LIMAX Group, Bw. Rob Menheere (kushoto). Katikati ni Bw. Petro Mahuwi “intern” Mtanzania aliyeongozana na Balozi Kasyanju kwenye ziara hiyo.


Namna kitalu kimoja wapo cha uyoga uliopandwa na ambao unakaribia kuvunwa kinavyoonekana katika moja ya mashamba makubwa 4 ya LIMAX Group iliyoko Horst, Uholanzi.

Balozi Kasyanju (kushoto) akiwa na Mkurugenzi na Mmiliki wa LIMAX Group, Bw. Tom van WALSEM (wa kwanza kushoto); Mkurugenzi Mwendeshaji, Bw. Rob Menheere (wa pili kushoto); na Meneja Biashara, Bw. Mark Duppen (wa tatu kushoto) wakikamilisha mazungumzo yao baada ya zoezi la kutembelea mashamba ya uyoga mjini Horst, Uholanzi kukamilika.


----------------------------

UYOGA WA TANZANIA KUPATA SOKO NCHINI UHOLANZI

Kampuni maarufu ya Uholanzi, LIMAX B.V. (LimaxGroup) imedhamiria kuwekeza kwenye Sekta ya Uyoga nchini Tanzania kwa kujenga kiwanda cha kusindika na kukausha uyoga Mkoani Iringa kwa thamani ya Euro milioni 2.1 ambazo ni sawa na Shilingi Bilioni 5.5 za Tanzania. Hayo yameelezwa kufuatia Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju kutembelea kampuni hiyo tarehe 26 Agosti 2021 na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi na Mmiliki wa kampuni hiyo, Bw. Tom VanWalsem.

Balozi Kasyanju alieleza kuwa uwekezaji huo utakapokamilika, Tanzania itafaidika kwa kiasi kikubwa kutokana na mtiririko wa biashara ya uyoga kukua kwa kasi duniani ambapo kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), biashara hiyo inakadiriwa kuongezeka hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 62.2 ifikapo mwaka 2023 kutoka Dola za Marekani bilioni 42.4 mwaka 2018.

Balozi Kasyanju aliendelea kueleza kuwa Kilimo cha uyoga ni sekta inayostawi nchini Tanzania na thamani yake ya kila mwaka inakadiriwa kuwa Tsh. Bilioni 4. Hivyo, ni dhahiri kuwa uwekezaji wa LimaxGroup utakuwa na tija kubwa na wazalishaji wa uyoga nchini watafaidika na soko kubwa lililopo katika Jumuiya ya Ulaya likiongozwa na Uholanzi ikifuatiwa na Ujerumani na baadaye Poland.

Balozi Kasyanju akiwa katika kampuni hiyo alipata fursa ya kujionea mashamba ya kisasa ya uyoga unaozalishwa (sio wa asili) na namna zao hilo lenye faida kubwa kwa binadamu linavyosindikwa na kufungashwa (processed and packed) na kuelezea matumaini yake kuwa Tanzania itafaidika na uwezo, uzoefu na utaalam mkubwa wa biashara wa Kampuni  hiyo.

“Tanzania ni nchi yenye maeneo makubwa ya misitu yenye aina anuwai ya uyoga wa porini kwa ajili ya kula, na jamii zimekuwa zinategemea maarifa asilia kukusanya uyoga huo kwa matumizi na kuuza katika masoko ya ndani tu. Ni wakati muafaka sasa kufanya kazi pamoja kukuza ukuaji wa sekta hii kibiashara”., Balozi Kasyanju alisema.

LIMAXGroup itatoa mafunzo ya kuhifadhi na kuvuna uyoga wa porini kwa madhumuni ya biashara na kulinda mazingira pia. Aidha, ujenzi wa kiwanda hicho mkoani Iringa kutawawezesha wakulima kuuza uyoga wanaozalisha moja kwa moja kiwandani, kuongeza ajira kwa Watanzania na kukuza mnyororo wa thamani wa kilimo cha uyoga nchini. 


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.