Na Mwandishi wetu, Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein
Ali Mwinyi amesema kipaumbele cha Serikali yake hususani katika sekta ya mafuta
na gesi,Utalii,Uvuvi Biashara na Uwekezaji ni katika Uchumi wa Buluu ambao
utamsaidia Mzazibar katika kuimarisha kipato pamoja na kuondoa kodi za kero kwa
Wanzazibar.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo wakati alipokutana na kufanya
mazungumzo na uongozi wa juu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki ulioongozwa na Waziri wa Wizara hiyo Balozi Liberata Mulamula (Mb)
kwa lengo la kujitambulisha na kupokea maelekezo ya
kutekeleza vipaumbele vya Serikali ya mapinduzi Zanzibar.
Dkt. Mwinyi ameilekeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki kutilia mkazo katika uwekezaji wa maeneo ya Uchumi wa Buluu
katika mazungumzo na Mashirika ya fedha duniani ikiwemo IMF na Benki ya dunia
ikiwa ni pamoja na wawekezaji na wafadhili mbalimbali kwa kuwa Serikali yake
ina imani kuwa bahari ikitumiwa vizuri itainufaisha Zanzibar kiuchumi kuliko
maeneo mengine.
Pia Dkt. Mwinyi ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki kuwasaidia wafanyabiashara kutoka Zanzibar kwa kuwaunganisha
na wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nje ili Zanzibar nayo iweze kusafirisha
bidhaa zake za ndani kwenda nje badala ya kupokea bidhaa kutoka mataifa mengine
kama ilivyo sasa.
Dkt. Mwinyi amezitaja bidhaa kutoka Zanzibar zinazoweza kusafirishwa Nje ya
Zanzibar kuwa ni pamoja na karafuu,samaki na nyama ambazo zina soko kubwa nje
ya nchi hususani katika nchi za Kiarabu.
Mbali na hilo Dkt. Mwinyi ametaka kupitiwa upya kwa Sera ya Mambo
ya Nje ya Nchi hususani katika suala Wazanzibar wanaoishi nje maarufu kama
Diaspora ikiwemo kupatiwa hadhi maalum itakayowawezesha kushiriki katika uchumi
wa nchi ikiwemo kuwekeza,kubadilishana uzoefu wa kitaaluma na masuala mengine
ya maendeleo.
Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi
Liberata Mulamula amesema Wizara imeyapokea maelekezo ya Rais Dkt Hussein na
kwamba tayari kuna mkakati na maelekezo maalum kwa Mabalozi wanaoiwakilisha
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mataifa mbalimbali duniani ili
kuhakikisha mahusiano ya Tanzania na Nchi hizo yanakuwa ya manufaa katika
uchumi wa pande zote za Jamuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika tukio jingine Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula na ujumbe wake wamekutana na kufanya
mazungumzo na Makamu wa kwanza wa Rais Mhe. Othman Masoud Othman ambaye kwa
upande wake ameeleza nia ya Ofisi yake katika kupambana kudhibiti biashara na
matumizi ya dawa za kulevya pamoja na suala la mazingira ambayo kwa kiasi
kikubwa yameathirika kutokana na mabadiliko ya Tabia nchi jambo ambalo
linatishia uhai wa Visiwa mbalimbali duniani ikiwemo Zanzibar.
Katika tiara hiyo Balozi Mulamula ameambatana na Naibu Waziri
Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine, Naibu
Katibu Mkuu Balozi Fatma Mohammed Rajab pamoja na baadhi ya Wakurugenzi wa
Idara na Vitengo vya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi
akimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.
Balozi Liberata Mulamula alipokuwa Ikulu - Zanzibar kwa mazungumzo na
kujitambulisha
Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi
akiongea na uongozi wa juu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ulioongozwa na Waziri wake Mhe.
Balozi Liberata Mulamula walipokuwa Ikulu - Zanzibar kwa mazungumzo na
kujitambulisha
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali
Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na Katibu wa baraza la Mapinduzi na Katibu
Mkuu Kiongozi - Zanzibar na Uongozi wa juu wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki ukiongozwa na Waziri wake Mhe. Balozi Liberata
Mulamula. wengine ni Naibu Waziri, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb),
Katibu Mkuu, Balozi Joseph Sokoine pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Balozi Fatma
Mohammed Rajab
 |
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman
Masoud Othman, amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wakuu wa Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Uongozi wa Wizara umeongozwa
na Mhe. Waziri, Balozi Liberata Mulamula (Mb) na kuwataka kuandaa mpango
maalumu wa kushirikiana na Zanzibar kwa lengo la kuendelea kuitangaza na
kuboresha uhusiano wake na nchi mbalimbali duniani |
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud
Othman, akizungumza na viongozi wakuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki. Uongozi wa Wizara umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Liberata
Mulamula (Mb), Naibu Waziri, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Katibu Mkuu,
Balozi Joseph Sokoine pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Balozi Fatma Mohammed Rajab
katika ziara rasmi ya kujitambulisha kwa Viongozi Waandamizi wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud
Othman katika picha ya pamoja na viongozi wakuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki. Uongozi wa Wizara umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Liberata
Mulamula (Mb), Naibu Waziri, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Katibu Mkuu,
Balozi Joseph Sokoine pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Balozi Fatma Mohammed Rajab.