Mkutano wa 21 wa Baraza la
Mawaziri la Kisekta (BLM) la Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umefanyika
tarehe 10 Desemba 2021 katika Hotel Verde mjini Zanzibar.
Mkutano wa Baraza la Mawaziri ulitanguliwa
na mikutano miwili ya awali iliyofanyika tarehe 6 hadi 8 Desemba 2021na tarehe
9 Desemba 2021 katika ngazi ya Wataalamu na Makatibu Wakuu mtawalia.
Akizungumza wakati wa ufunguzi
wa mkutano huo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Mhe. Nassor Ahmed Mazrui (Mb) aliwakaribisha wajumbe wa mkutano huo mjini
Zanzibar na kupongeza maamuzi yaliyofikiwa na sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya kwamba mkutano
huo ufanyike mjini humo ili kuwapa fursa wajumbewa mkuano huo kuyafahamu maeneo ya utalii ndani ya kanda.
Vilevile alieleza Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania itaendelea kufanyia kazi maamuzi na mapendekezo mbalimbali yanayotolewa
na vikao hivyo ili yaweze kuwa na tija kwa masalahi ya wananchi ndani ya jumuiya.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Sekta ya Uzalishaji na Jamii, Mhe.
Christophe Bazivamo katika ufunguzi wa
mkutano huo aliipongeza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mapokezi mazuri kwa
wajumbe wa mkutano huo na kwa kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 60 ya Uhuru wa
Tanzania Bara.
Aidha, alitumia nafasi hiyo
kupongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na Jumuiya ya Afrika Mashariki
katika kurasimisha lugha nyingine zitakazotumiwa kwenye mikutano ya jumuiya
hiyo ambapo, alieleza mpaka sasa Sekretarieti ya Jumuiya hiyo inafanyia kazi taratibu
za kuifanya lugha za Kiswahili na kifaransa kuwa lugha rasmi kwa ajili ya matumizi ya
mikutano ya jumuiya.
Pia amepongeza juhudi
zilizooneshwa na Shirika
la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO)
kwa kutangaza tarehe 7 Julai kuwa siku ya Kiswahili.
“UNESCO imeonesha ni namna
gani lugha ya Kiswahili ambayo ndio lugha pekee ya kiafrika yenye watumiaji
wengi imeweza kuthaminiwa ulimwenguni, sisi kama jumuiya tutaendeleza jitihada
za kukuza Kiswahili” alisema Mhe. Bazivamo.
Kadhalika, Mhe. Bazivamo
amezisisitiza Nchi wanachama wa jumuiya hiyo kukamilisha zoezi la uandaaji wa
Hati za Kusafiria za Kielekronik za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC e-Passport)
ambapo, ameeleza mpaka sasa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pekee ndio
imefanikiwa kukamilisha zoezi la ugawaji wa Hati hizo za kusafiria kwa wananchi
wake.
Ujumbe wa Tanzania katika
mkutano huo umeongozwa na Mhe. Nassor Ahmed Mazrui (Mb.) Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
ambaye ameambatana na Mhe. Dkt. Godwin Mollel (Mb.) Naibu Waziri, Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Tanzania Bara.
Viongozi wengine walioshiriki mkutano huo
ni pamoja na; Dkt. Fatma H. Mrisho, Katibu Mkuu Wizara
ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar; Dkt. Othman Mohamed Ahmed, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia - Tanzania Bara, Bw. Eliabi Chodota, Mkurugenzi Idara ya
Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki; na Dkt. Abdul S. Ali, Mganga Mkuu na Mkurugenzi Mkuu
wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia Wazee na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar.
Pamoja na Mambo mengine Mkutano wa 21 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umepokea taarifa ya utekelezaji wa maamuzi/maagizo ya mikutano iliyopita; hali ya mlipuko wa janga la UVIKO-19 Kikanda; na Utekelezaji wa program na miradi ya Afya.
Mkutano huo umehudhuriwa na nchi zote wanachama isipokuwa Jamhuri ya Rwanda na Jamhuri ya Sudan Kusini ambao walishiriki mkutano kwa njia ya mtandao.
==============================
|
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Godwin Mollel (Mb) akifafanua jambo wakati wa Mkutano wa 21 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 10 Desemba 2021 katika Hotel Verde mjini Zanzibar. Pembeni yake ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui. |
|
Meza kuu wakiongozwa na Mwenyekiti wa mkutano huo Naibu Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Rashid Aman (wa pili kutoka kulia). Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Sekta ya Uzalishaji na Jamii, Mhe. Christophe Bazivamo. |
|
Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eliabi Chodota pamoja na Mganga Mkuu na Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Abdul S. Ali wakifuatilia mkutano. |
|
Ujumbe wa Tanzania |
|
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania |
|
Ujumbe kutoka Burundi |
|
Ujumbe kutoka Uganda |
|
Picha ya pamoja viongozi wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mawaziri wa Afya wa Jumuiya hiyo walioshiriki mkutano. |
|
Mkutano ukiendelea |