|
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Balozi Joseph Sokoine akizungumzia maazimio yaliyofikiwa katika Mkutano
wa 114 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya OACPS uliofanyika jijini
Brussels nchini Ubelgiji tarehe 8 na 9 Juni 2022 ambapo alimwakilisha
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi
Liberata Mulamula katika mkutano huo. |
|
Katibu
Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph
Sokoine (aliyekaa katikati) akiwa na Ujumbe wa Tanzania ulioshiriki Mkutano wa 114 wa
Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya OACPS uliofanyika jijini Brussels nchini Ubelgiji
tarehe 8 na 9 Juni 202. Kushoto aliyekaa ni Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Mhe. Jestas Nyamanga na kulia aliyekaa ni mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Marekani Bi Agnes Kiama. |
|
Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na
Pasifiki (OACPS) umetenga kiasi cha Euro milioni 157 kukopesha wadau wa kilimo
katika nchi wanachama kwa masharti
nafuu ili kuwekeza kwenye sekta ya kilimo na hivyo kuongeza mnyororo wa thamani
katika mazao ya kilimo.
Katibu
Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph
Sokoine amesema hilo ni azimio mojawapo lililofikiwa katika Mkutano wa 114 wa
Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya OACPS uliofanyika jijini Brussels nchini Ubelgiji
tarehe 8 na 9 Juni 2022 ambapo alimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula.
Amesema
kuwa wadau wa kilimo kutoka Tanzania wanaotaka mikopo hiyo ya masharti nafuu
watatakiwa kuomba fedha hizo kupitia
Ubalozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na kuweza kushiriki kikamilifu katika
mkakati huo wa kuongeza mnyororo wa thamani kwenye mazao ya kilimo
“ Mkutano
umeazimia kuanzisha mkakati wa kuongeza mnyororo wa thamani katika mazao ya
kilimo, na ili kufanikisha azimio hilo Jumuiya imetenga Euro milioni 157 ambazo
zitatoka kama mikopo ya masharti nafuu kwa wakulima ndani ya jumuiya yetu ya
OACPS” alisema Balozi Sokoine na kuongeza kuwa wadau wa kilimo kutoka Tanzania
wataweza kuomba fedha hizo kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Ubelgiji.
Amesema kuwa
Ubalozi ukikamilisha taratibu za uombaji na utoaji wa mikopo hiyo utatoa kwa
walengwa ili wafanye maombi ya mikopo hiyo.
Akiongelea
mazimio mengine, Balozi Sokoine amesema kuwa ni kuidhinishwa kwa Tanzania
katika nafasi ya Uenyekiti wa Kamati ya masuala ya Uvuvi kwa miaka miwili
kuanzia 2022 hadi 2024 na hivyo kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mawaziri wa masuala Uvuvi
unaotarajiwa kufanyika nchini mwaka 2024.
“Hatua hii ni fursa kubwa kwa Tanzania katika kusimamia
utekelezaji wa ajenda yake ya uchumi wa buluu na kukuza ushirikiano baina ya
nchi za OACPS katika sekta ya uvuvi” alisema.
Amesema Mkutano
huo umejadili changamoto zinazowakabili wafanyabiashara ndani ya jumuiya wakati
wa kuingiza bidhaa katika soko la Ulaya na kuja na mikakati ya kutatua
changamoto hizo kwa kufaya tathmini ya kina ili kuzielewa changamoto husika na
kuanzisha mfumo wa utoaji tahadhari mapema kwa wafanyabiashara.
Amesema
azimio lingine ni kuanzisha Jukwaa Maalum la Wafanyabiashara ndani ya Jumuiya
kwa lengo la kuwakutanisha wafanyabiashara, kubadilishana uzoefu na kukuza
mtandao wa masoko ya bidhaa na huduma na kuongeza kuwa Mkutano
pia umeazimia kuunganisha nguvu ya Diaspora kwa kuanzisha jukwaa maalum la
kuwezesha Diaspora kukaa pamoja na kubadilishana uzoefu kwenye masuala
mbalimbali ikiwemo fursa za uwekezaji ndani ya Jumuiya na kutoa maoni na kufanyiwa
kazi.
Mkutano wa Baraza la Mawaziri la
nchi wanachama wa OACPS ni chombo cha maamuzi cha Jumuiya hiyo ambacho
kinahusika na utekelezaji wa maazimio yanayopitishwa na Mkutano wa Wakuu wa
Nchi na Serikali. Baraza hilo linaundwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka kwa
Nchi wanachama na hukutana mara mbili kwa mwaka kujadili utekelezaji wa
maazimio yaliyofikiwa kutoka katika
mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya hiyo.