Thursday, July 14, 2022

SERIKALI YAIPONGEZA TAASISI YA MAENDELEO YA AGA KHAN KWA KUCHANGIA MAENDELEO NCHINI

  

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ameipongeza Taasisi ya Maendeleo ya Aga Khan (AKDN) kwa mchango wake mkubwa katika kukuza na kuendeleza sekta za elimu, afya, miundombinu, utalii na utamaduni hapa nchini. 


Balozi Mbarouk ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 65 ya Uimamu wa Kiongozi wa Kiroho wa Madhehebu ya Shia Ismailia duniani, Mhe. Karim  Aga Khan. 


Balozi Mbarouk ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Taasisi hiyo, amesema Taasisi hiyo ambayo kupitia miradi mbalimbali iliyopo Tanzania Bara na Zanzibar ikiwemo ya elimu na afya na ile ya kujikwamua kiuchumi imewasaidia watu wengi ambapo hadi sasa takriban watoto 10,000 nusu ya hao wakiwa wasichana wamefaidika kwa kupata elimu bora kupitia taasisi hiyo


"Kupitia uongozi mzuri wa Mheshimiwa Aga Khan, Taasisi ya AKDN imekuwa mstari wa mbele kuchangia katika sekta za elimu, afya, maendeleo ya uchumi na kuondoa umaskini kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar. Hivyo ninayo furaha kuungana na jamii ya Ismailia ya hapa nchini na duniani kwa ujumla kusherehekea siku hii muhimu ya miaka 65 ya Mhe. Aga Khan kuwa Imam wa Madhehebu ya Shia Imailia” alisema Balozi Mbarouk. 


Kadhalika, Mhe. Balozi Mbarouk alisema anapongeza jitihada zinazoendelea kufanywa na AKDN katika kuboresha huduma za afya nchini ambapo kupitia jitihada hizo, mwezi Aprili 2022, Mkuu wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii ya AKDN, Mhe. Zahra Aga Khan, Mkuu wa Kamati ya Jamii ya AKDN alitembelea Tanzania na kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Kituo cha Huduma za Saratani jijini Dar es Salaam cha kiwango cha kimataifa ambacho kitakuwa na uwezo wa kutoa huduma mbalimbali kuhusu ugonjwa wa saratani ikiwemo kinga, utambuzi wa mapema wa ugonjwa, matibabu na huduma  za nyumbani kwa wagonjwa 


 Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Taasisi ya AKDN hapa nchini, Mhe. Balozi Amin Kurji amesema Taasisi yake itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia sekta mbalimbali zikiwemo za afya na elimu. Amesema, kupitia taasisi hiyo tayari miradi mbalimbali ikiwemo ya Vyuo Vikuu, Vyuo vya Afya vya wauguzi na wakunga vimeanzishwa nchini. 


Aidha,  ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maendeleo makubwa ya uchumi na jamii yaliyopatikana nchini katika kipindi kifupi tangu aingie madarakani na kwamba Taasisi ya AKDN itaendelea kushirikiana na Serikali ili kuunga mkono jitihada hizo. 


“Nampongeza Mhe. Rais Samia na Serikali yake kwa ujumla. Tumeshuhudia uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika kuboresha sekta za afya, elimu maji, umeme, miundombinu na sekta za uzalishaji. AKDN inaahidi kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha maisha ya Watanzania” alisisitiza Balozi Kurji. 


Maadhimisho hayo ambayo yalifanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam yalihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, Mabalozi, Wabunge na Wageni wengine waalikwa.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 65 ya Uimamu wa Kiongozi wa Kiroho wa Madhehebu ya Shia Ismailia duniani, Mheshimiwa Karim Aga Khan. Pamoja na mambo mengine Mhe. Balozi Mbarouk aliipongeza Taasisi ya Maendeleo ya Aga Khan (AKDN) kwa mchango wake katika kuboresha na kuendeleza sekta za elimu, afya na miundombinu. Maadhimisho hayo ambayo yalihudhuriwa na  viongozi mbalimbali wa Serikali yalifanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam
Mhe. Balozi Mbarouk akihutubia wageni waalkiwa wakati wa maadhimisho ya miaka 65 ya Imam Aga Khan

Mwakilishi Mkazi wa Taasisi ya AKDN nchini, Mhe. Balozi Amin Kurji naye akizungumza wakati wa maadhimisho hayo

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akifuatilia maadhimisho ya miaka 65 ya Imam Aga Khan

Wageni waalikwa wakifuatilia maadhimisho ya miaka 65 ya Uimamu wa Aga Khan

Mhe. Naibu Waziri akipata maelezo kuhusu kazi mbalimbali za uchapishaji  vitabu unaofanywa na Taasisi ya AKDN

Mhe. Balozi Mbarouk akiwa katika picha ya pamoja

 

Wednesday, July 13, 2022

BALOZI MUSHY AKUTANA NA MEYA WA JIJI LA Linz

Balozi wa Tanzania nchini Austria, Mhe. Celestine Mushy (kushoto)  akutana na kufanya mazungumzo na Meya wa Jiji la Linz, Mhe. Mstahiki Klaus Luger. Balozi alimshukuru kwa mapemzi yake kwa Tanzania ambayo yaliwezesha Jiji la Dodoma kuwa na mahusiano na Jiji la Linz (Sister Cities).   Balozi alimuomba kuimarisha mahusiano hayo zaidi kwa kusainiana makubalino ya ushirikiano kati ya hospitali na vyuo vikuu vya Linz na Tanzania ili kuweza kubadilishana utaalamu, teknolojia, mafunzo, wanafunzi na wahadhiri. Aidha, Balozi alimuomba kuandaa mkutano wa wadau wote ili aweze kuongea nao. Mhe. Mstahiki Meya alikubali maombi hayo.

Balozi wa Tanzania nchini Austria, Mhe. Celestine Mushy na Meya wa Jiji la Linz, Mhe. Mstahiki Klaus Luger wakiwa katika picha ya pamoja na wasaidizi wao baada ya kufanya mazungumzo.



 

BALOZI MULAMULA AKUTANA NA RAIS WA CARE INTERNATIONAL

Shirika lisilo la kiserikali la Care International limetakiwa kupanua huduma zake katika mikoa mingi zaidi badala ya mikoa tisa tu ambayo shirika hilo kwa sasa linatoa huduma zake hapa nchini.

Wito huo umetolewa leo tarehe 13 Julai 2022 jijini Dar Es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, wakati wa mazungumzo yake na Rais na Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo, Bi. Michelle Nunn

Bi. Nunn ametaja baadhi ya shughuli ambazo shirika lake inazifanya hapa nchini kuwa ni pamoja na utunzaji wa mazingira, afya, elimu, kuwawezesha wanawake kiuchumi, kilimo, haki za kijamii na usawa wa kijinisa. Amesema utekelezaji wa shughuli hizo umezingatia kipaumbele cha mwanamke.

“Tunasaidia watoto wa maeneo ya vijijini kupata elimu bora, tunasaidia jamii kutumia aridhi yao vizuri ili izalishe chakula, wakati huo huo ikitunzwa vizuri na programu zetu za kutoa mikopo na kuwasaidia wanawake wa vijijini kujiwekea akiba kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kidigitali zimewawezesha wanawake wengi kumiliki rasilimali na kunyanyuka kiuchumi”, Alisema Bi. Nunn.

Kwa upande wake, Balozi Mulamula alilishukuru shirika hilo kwa misaada inayotoa nchini na kueleza kuwa programu zao za misaada zinaenda sanjari na dira ya maendeleo ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Aliendelea kueleza kuwa changamoto kwa wanawake ni nyingi zikiwemo za afya ya uzazi na ugonjwa wa malaria ambao bado unakatisha maisha ya watu wengi katika nchi za Afrika, hivyo alishauri umuhimu wa “Care International” kuangalia kwa jicho la pekee eneo hilo.

Aidha, Balozi Mulamula alilipongeza shirika hilo kwa kujikita katika utunzaji wa mazingira kwa kuwa tatizo hilo ni kubwa na watu wengi hawalioni, ingawa madhara ya uharibifu wa mazingira yanamfikia kila mmoja wetu.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (kulia) akiwa katika mazungumzo na Rais na Mtendaji Mkuu wa Care International, Bi. Michelle Nunn kuhusu huduma zinazotolewa na shirika hilo nchini Tanzania

Ujumbe ulioambatana na Rais na Mtendaji Mkuu wa Care International, Bi. Michelle Nunn ukifuatilia mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (kulia) akiwa katika mazungumzo na Rais na Mtendaji Mkuu wa Care International, Bi. Michelle Nunn huku maafisa walio chini yao wakifuatilia mazungumzo hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (katikati) akifurahia jambo na Rais na Mtendaji Mkuu wa Care International, Bi. Michelle Nunn (kulia) na Mkurugenzi Mkazi wa Care International, Bi. Prudence Masako

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Rais na Mtendaji Mkuu wa Care International, Bi. Michelle Nunn wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi walioambatana nao wakati walipofanya mazungumzo jijini Dar Es Salaam. 

Tuesday, July 12, 2022

KIWANDA CHA LABIOFAM KIBAHA KUPANULIWA

Serikali za Tanzania na Cuba zipo katika mchakato wa kupanua kiwanda cha Labiofam kilichopo Kibaha, Pwani cha kuzalisha viuadudu vya mazalia ya mbu ili kiwe na uwezo wa kuzalisha mbolea na dawa nyingine za kuua wadudu waharibifu wa mazao ya kilimo.

Hayo yamesemwa leo tarehe 12 Julai 2022 jijini Dar Es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt Grace Magembe wakati wa ufunguzi wa kikao kati ya Serikali za Tanzania na Cuba cha kujadiliana kuhusu upanuzi wa kiwanda hicho kinachoendeshwa kwa ubia baina ya Serikali hizo mbili.

Dkt. Magembe ambaye ni kiongozi wa ujumbe wa Tanzania unaojadiliana na ujumbe wa Cuba, alisema kuwa ana matumaini makubwa katika kikao hicho cha siku mbili, wajumbe watafikia makubaliano yatakayokuwa na manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili.

 

“Kama unavyofahamu asilimia 70 hadi 80 ya Watanzania ni wakulima, hivyo, uwepo wa kiwanda hiki na uzalishaji wa mbolea na viuadudu ni fursa nzuri kwa wakulima wetu na nchi kuendeleza sekta ya kilimo pamoja na wananchi kujipatia kipato kwa mazao watakayovuna”, Dkt. Magembe alisema.

 

Kwa upande wake kiongozi wa ujumbe wa Cuba ambaye ni Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kimataifa kutoka Wizara ya Kilimo ya nchi hiyo, Bw. Orlando Diaz Rodriguez alisema kuwa uwepo wa kiwanda hicho ni ishara ya wazi ya uhusiano mzuri uliopo kati ya Cuba na Tanzania.

Aidha, naye alielezea matumaini yake kuwa majadiliano hayo ya siku mbili yatakuwa na faida kubwa kwa maendeleo ya sekta ya kilimo ya Tanzania na azma ya Serikali ya kupamabana na ugonjwa wa malaria na hatimaye kuuangamiza kabisa.


Kiongozi wa ujumbe wa Cuba ambaye ni Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kimataifa kutoka Wizara ya Kilimo ya nchi hiyo, Bw. Orlando Diaz Rodriguez akitoa neno wakati wa ufunguzi wa kikao kati ya Serikali za Tanzania na Cuba cha kujadiliana kuhusu upanuzi wa kiwanda cha LABIOFAM cha Kibaha. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt Grace Magembe ambaye ni Kiongozi wa timu ya majadiliano ya Tanzania. 


Kiongozi wa ujumbe wa Cuba ambaye ni Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kimataifa kutoka Wizara ya Kilimo ya nchi hiyo, Bw. Orlando Diaz Rodriguez akielezea matumaini yake kuwa kikao cha majadiliano kitakuwa na manufaa kwa pande zote mbili

Wataalamu wa Tanzania wanaoshiriki kikao cha majadiliano kati ya Tanzania na Cuba kuhusu upanuzi wa kiwanda cha LABIOFAM kinachoendeshwa kwa ubia kati ya Cuba na Tanzania

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC),     Dkt. Nicolous Shombe akiongea jambo katika kikao cha majadiliano kati ya Tanzania na Cuba kuhusu upanuzi wa kiwanda cha LABIOFAM kinachoendeshwa kwa ubia kati ya Cuba na Tanzania

Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Valentino Mlowola akiongea jambo katika kikao hicho. Mwingine ni MKurugenzi wa Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme

Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Yordenis Despaigne Vera akiongea jambo katika kikao cha majadiliano kati ya Tanzania na Cuba kuhusu upanuzi wa kiwanda cha LABIOFAM
Wajumbe wa Tanzania na Cuba wakiwa katika ufunguzi wa kikao cha majadiliano kati ya Tanzania na Cuba kuhusu upanuzi wa kiwanda cha LABIOFAM kinachoendeshwa kwa ubia kati ya Cuba na Tanzania

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt Grace Magembe (katikati), Kiongozi wa ujumbe wa Cuba ambaye ni Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kimataifa kutoka Wizara ya Kilimo ya nchi hiyo, Bw. Orlando Diaz Rodriguez (kulia) na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Dkt. Nicolous Shombe wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania na Cuba unaofanya majadiliano kuhusu upanuzi wa kiwanda cha LABIOFAM

 

Monday, July 11, 2022

UBALOZI WA TANZANIA NCHINI ISRAEL ULIVYOADHIMISHA SIKU YA KISWAHILI DUNIANI

Wadau mbalimbali nchini Israel wamepongeza jitihada za Serikali ya Tanzania katika kukuza na kuienzi Lugha ya Kiswahili.

Pongezi hizo zimetolewa na wadau hao wakati wa Maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika tarehe katika Makazi ya Balozi wa Tanzania nchini humo tarehe 07Julai 2022

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Alex Gabriel Kalua amesema kuwa ametumia maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani kukukutana na kujadiliana na wadau mbalimbali kuhusu namna bora ya kukuza na kuendeleza Lugha hiyo adhimu.

Aidha, Mhe. Balozi Kalua ambaye alijumuika na viongozi kutoka Serikali ya Israel, wadau mbalimbali wanaoshirikiana na Tanzania, Watanzania wanaoishi nchini humo na wageni mbalimbali, alitumia maadhimisho  hayo kugawa vitabu vya kujifunzia Kiswahili kikiwemo cha “Jifunze Kiswahili, Hazina ya Afrika: Kitabu cha Kwanza”, pamoja na kushiriki chakula cha Kitanzania na wadau hao.

Kadhalika, Mhe. Balozi Kalua alitoa hotuba yake kwa lugha ya Kiswahili ambayo ilitafsiriwa kwa Kiebrania.

Naye Mkurugenzi wa Ukanda wa Afrika Mashariki katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel, Bibi Amit Gil Bayaz ambaye ni miongoni mwa viongozi kutoka Serikali ya Israel walioshiriki aliipongeza Tanzania kwa maadhimisho hayo.

Maadhimisho hayo yalihitishwa kwa Wadau mbalimbali  kushiriki chakula na vinywaji vya kitanzania  ambapo walieleza kufurahishwa na ukarimu wa watanzanaia na kufurahia vinywaji na chakula cha kitanzania kilichoandaliwa kwa ajili yao.

Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Alex Gabriel Kalua akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika kwenye Makazi ya Balozi nchini humo tarehe 7 Julai 2022 na kuwashirikisha wadau mbalimbali. Wengine katika picha ni Mwakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel ambaye ni Mkurugenzi wa Ukanda wa Afrika Mashariki, Bibi Amit Gil Bayaz (wa pili kutoka kushoto), Rais wa Klabu ya Mabalozi waliopo Israel, Mhe. Balozi Yzihack Elden (kushoto) na Mwakilishi wa Balozi wa Heshima, Mhe. Chirich Nuriel Kasbian (wa pili kulia)


Mhe. Balozi Kalua akimkabidhi kitabu cha kujifunza Kiswahili, Mkurugenzi wa Ukanda wa Afrika Mashariki, Bibi Amit Gil Bayaz.

Mhe. Balozi Kalua akimkabidhi kitabu cha kujifunza Kiswahili, Rais wa Klabu ya Mabalozi waliopo Israel, Mhe. Yitzhack Elden


Mhe. Balozi Kalua akiwa na wadau mbalimbali aliowakabidhi vitabu

Wawakilishi kutoka Jeshi la Israel walioshiriki maadhimisho ya siku ya Kiswahili wakiwa na Mwambata Jeshi wa Ubalozi wa Tanzania nchini, Israel, Brig. Jen. Mziray


Wadau mbalimbali wakionesha vitabu vya kujifunza Kiswahili walivyokabidhiwa

 

BALOZI MULAMULA AKUTANA NA WANAFUNZI-DIASPORA WA MAREKANI.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amekutana na walimu na wanafunzi wenye asili ya Afrika na Marekani wanaofundisha na kusoma vyuo mbalimbali vya Marekani ambao wapo nchini kwa ziara ya kikazi hadi tarehe 17 Julai 2022.

Ziara hiyo iliyoratibiwa na Mtanzania-Diaspora, Bi Zawadi Sakapala ambaye ni mmiliki wa kituo cha “Community Centre” kilichopo Kijichi jijini Dar Es Salaam inalenga pamoja na mambo mngine, kutoa fursa kwa wanafunzi hao kujifunza masuala ya utamaduni wa Tanzania na kubadilishana ujuzi na uzoefu katika masomo ya sayansi, ufundi, ufundishaji na Usimamizi wa watoto wadogo (daycare).

Katika kikao hicho, Bi Zawadi alimfahamisha Mhe. Balozi Mulamula kuwa kituo chake kimekuwa kikishirikiana na vyuo vikuu mbalimbali nchini Marekani kuratibu ziara za walimu na wanafunzi wenye asili ya Afrika na Marekani kutembelea nchi za Afrika kwa ajili ya kubadilishana uzoefu katika sekta ya elimu.

Hivyo, ili kuimarisha sekta ya elimu katika nchi za Afrika, kikao hicho kiliazimia kuongeza jitihada za kuhamasisha Waafrika wengi zaidi kujiunga na vyuo vya Marekani, kuunganisha vyuo vya Afrika na Marekani, wanafunzi-Watanzania wanaopata fursa ya kusoma Marekani, watumike kufundisha lugha ya Kiswahili ikiwa ni moja ya njia ya kueneza lugha hiyo duniani pamoja na kwahimiza watu wenye asili ya Afrika kutumia elimu, ujuzi na maarifa waliyopata wakiwa ughaibuni kuinua jamii za nchi za Afrika.

Wakati huo huo, Balozi Mulamula amekutana na Ujumbe wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Programu ya Maendeleo (UNDP) ambao upo nchini kwa ajili ya kufanya mazungumzo na wadau wa siasa ili kubainisha maeneo ambayo, shirika hilo linaweza kusaidia katika uendeshaji wa uchaguzi mkuu ujao.

Ujumbe huo unaongozwa na Afisa Uchaguzi Mkuu katika Idara ya Siasa na Masuala ya Amani ya Umoja wa Mataifa, Bw. Akinyemi Adegbola umefanikiwa kufanya vikao na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, wawakilishi wa vyama vya siasa na asasi za kiraia, umepokea maoni ya wadau hao ya maoneo yanayohitaji msaada na umeahidi utayafanyia kazi kikamilifu. Maeneo hayo ni pamoja na uelimishaji wa wapiga kura, msaada wa kiufundi katika upigaji na uandikishwaji wa wapiga kura na teknolojia ya mawasiliano wakati zoezi la uchaguzi.

Kwa upande wake, Balozi Mulamula aliueleza ujumbe huo kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kipindi kifupi cha uongozi wake ameonesha dhamira ya dhati ya kuboresha mazingira ya kisiasa nchini, kwa kuhamasisha majadiliano ya kisiasa, ushirikishwaji wa wadau wote, umoja na mshikamano wa kitaifa. Hivyo, aliuhakikishia ujumbe huo kuwa uchaguzi ujao utaendelea kuwa huru, haki na amani kama ilivyo desturi ya Tanzania.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea na walimu na wanafunzi wenye asili ya Afrika na Marekani (hawapo pichani) wanaosoma na kufundisha vyuo mbalimbali vya Marekani ambao wapo nchini kwa ziara maalum hadi tarehe 17 Julai 2022.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akimsikiliza mmoja wa mwanafunzi anayesoma katika vyuo vikuu vya Marekani kuhusu mikakati ya kusaidia vijana wa Afrika kupata elimu bora itakayoweza kukabili mazingira ya dunia ya sasa.

Mhitimu wa Shahada ya Uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Howard cha nchini Marekani ambaye pia ni Kiongozi wa Taasisi ya 3GC Inc. akieleza shughuli za taasisi hiyo zinazolenga kuwasaidia vijana wa Afrika 
Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Balozi Mindi Kasiga wakifuatilia mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na walimu na wanafunzi wenye asili ya Afrika na Marekani wanaosoma na kufundisha vyuo mbalimbali vya Marekani


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akimvisha scurf ya bendera ya Tanzania, mmiliki wa kituo cha “Community Centre” kilichopo Kijichi jijini Dar Es Salaam, Bi. Zawadi Sakapala

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na walimu na wanafunzi wenye asili ya Afrika na Marekani wanaosoma na kufundisha vyuo mbalimbali vya Marekani



BALOZI MULAMULA AKUTANA NA  AFISA UCHAGUZI MKUU WA UN


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Afisa Uchaguzi Mkuu katika Idara ya Siasa na Masuala ya Amani ya Umoja wa Mataifa, Bw. Akinyemi Adegbola yaliyofanyika jijini Dar Es Salaam

Baadhi ya ujumbe uliongozana na Afisa Uchaguzi Mkuu katika Idara ya Siasa na Masuala ya Amani ya Umoja wa Mataifa, Bw. Akinyemi Adegbola kwenye mazungumzo ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Afisa huyo.

Ujumbe wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula ukifuatilia mazungumzo yake na Afisa Uchaguzi Mkuu katika Idara ya Siasa na Masuala ya Amani ya Umoja wa Mataifa

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiagana na ujumbe wa UNDP ambao upo nchini kwa ajili ya kuzungumza na wadau wa siasa kuhusu uchaguzi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa UNDP ambao upo nchini kwa ajili ya kuzungumza na wadau wa siasa kuhusu uchaguzi.


BALOZI MULAMULA AKUTANA NA MWAKILISHI MKAZI WA UN WOMEN

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa  UN Women, Bi.  Hodan Addou kwenye Hoteli ya Seana jinini Dar Es Salaam.


BALOZI MULAMULA AKUTANA NA  BALOZI MTEULE LT. JEN. MATHEW EDWARD MKINGULE 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Balozi Mteule Lt. Jen. Mathew Edward Mkingule yaliyofanyika jijini Dar Es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa na Balozi Mteule Lt. Jen. Mathew Edward Mkingule baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika jijini Dar Es Salaam


 

VACANCY ANNOUNCEMENT