Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amewataka watumishi wa Wizara kuendelea kuchapa kazi kwa bidii, ufanisi na kushirikiana ili kufikia matarajio ya serikali na wananchi kwa ujumla.
Dkt. Tax ametoa rai hiyo leo katika Ofisi za Wizara Jijini Dodoma mara baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula.
Dkt. Tax amesema watumishi wa Wizara wanatakiwa kuhakikisha wanatumia weledi na kuwa wabunifu katika kutekeleza majukumu ya Wizara ili kuleta tija na ufanisi wakati wote.
“Sisi ni timu ya ushindi, tuendelee kuchapa kazi, nitashirikiana na watumishi wote wa Wizara, kuhakikisha tunatekeleza majukumu yetu kwa viwango na kwa muda sahihi, tuwe wabunifu na tujitahidi kufanya kazi kama timu ili kufikia matarajio ya Serikali yetu na wananchi wote kwa ujumla,” alisema Dkt. Tax
Ameongeza kuwa kazi ya kukuza uhusiano kati ya Tanzania na nchi mbalimbali, Jumuiya za kikanda na kimataifa haiwezi kufanikiwa ikiwa watumishi hawatashirikiana na kufanya kazi kwa pamoja kama timu huku wakizingatia weledi, uzalendo na ubunifu kwa maslahi mapana ya taifa.
Akizungumza katika makabidhiano hayo, Balozi Liberata Mulamula amewashukuru Watumishi wa Wizara kwa ushirikiano waliompatia alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambao ulimuwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
“Nimeacha timu imara nawashukuru wote kwa ushirikiano mlionipatia na niwaombe muendelee na moyo huohuo katika kufanikisha majukumu ya wizara,” alisema Balozi Mulamula.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbrouk Nassor Mbarouk amemshukuru Balozi Mulamula kwa ushirikiano aliompatia katika kipindi chake na kumsihi aendelee kushirikiana nao kwa kuzingatia hazina kubwa ya uzoefu na ujuzi alionao katika sekta ya mambo ya nje.