Wednesday, October 26, 2022

UMOJA WA ULAYA KUIPATIA TANZANIA MSAADA WA EURO MILIONI 166



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (kulia) akiwa na Kamishina wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Ubia wa Kimataifa, Mhe. Jutta Urpilainen kabla ya kuanza mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar Es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Kamishina wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Ubia wa Kimataifa, Mhe. Jutta Urpilainen. Kushoto kwa Mhe. Waziri ni Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na katika Umoja wa Ulaya, Mhe. Jestas Nyamanga. 

Kamishina wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Ubia wa Kimataifa, Mhe. Jutta Urpilainen (katikati) na ujumbe wake wakisikiliza jambo kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika jijini Dar Es Salaam

Kamishina wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Ubia wa Kimataifa, Mhe. Jutta Urpilainen akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax

Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na katika Umoja wa Ulaya, Mhe. Jestas Nyamanga akisalimiana na .Kamishina wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Ubia wa Kimataifa, Mhe. Jutta Urpilainen alipowasili kwenye ofisi za Wizara kwa ajili ya mazungumzo 
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akisalimiana na Kamishina wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Ubia wa Kimataifa, Mhe. Jutta Urpilainen alipowasili kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere kwa ajili ya kufanya mazungumzo

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba na ujumbe wake wakiwa katika mazungumzo na Kamishina wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Ubia wa Kimataifa, Mhe. Jutta Urpilainen yaliyofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere






 

Tuesday, October 25, 2022

DKT. MWINYI AWATAKA MABALOZI KUZINGATIA MASLAHI YA TAIFA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka Mabalozi wa Tanzania Nje ya nchi kuzingatia maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanapotekeleza Sera ya Mambo ya Nje inayojikita katika diplomasia ya uchumi.

Dkt. Mwinyi ametoa agizo hilo alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipofika Ikulu, Zanzibar tarehe 25 Oktoba 2022 kwa ajili ya kujitambulisha. 

“Mabalozi wa Tanzania Nje ya nchi wahakikishe wanaangalia maslahi mapana ya Tanzania wanapotekeleza diplomasia ya uchumi, hususan uchumi wa buluu ambao ni moja ya vipaumbele vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,” amesema Dkt. Mwinyi

Kwa Upande wake, Mhe. Dkt. Stergomena Tax ameahidi kuyafanyia kazi maagizo na miongozo mbalimbali inayotolewa na itakayotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa weledi na wakati.

“Mhe. Rais napenda kukuhakikishia kuwa nitasimamia na kutekeleza yote uliyotuelekeza kwa wakati na kwa maslahi mapana ya pande zote mbili,” amesema Dkt. Tax

Katika ziara hiyo, Dkt. Tax alipata fursa pia ya kujitambulisha kwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla. 

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wameahidi kumpatia ushirikiano unaohitajika ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake.

Naye Dkt. Tax amesema yupo tayari kwa ajili ya kazi ya kuitumikia nchi na kuhakikisha ushirikishwaji wa Zanzibar juu ya mambo ya muungano sambamba na fursa mbalimbali ikiwemo maazimio yanayopitishwa mbele ya jumuiya za kikanda na za kimataifa.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipofika Ikulu, Zanzibar tarehe 25 Oktoba 2022

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza akimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipofika Ikulu, Zanzibar tarehe 25 Oktoba 2022

Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipokuwa Ofisini kwake Zanzibar tarehe 25 Oktoba 2022

Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipokuwa Ofisini kwake Zanzibar tarehe 25 Oktoba 2022

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipokuwa Ofisini kwake Zanzibar tarehe 25 Oktoba 2022

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akimueleza jambo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla. Dkt. Tax alifika Ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais kwa lengo la kujitambulisha 



KATIBU MTENDAJI WA SADC AFANYA ZIARA YA KIKAZI NCHINI

Tanzania itaendelea kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)ili kufikia malengo ya kukuza uchumi na kudumisha amani na usalama katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo.



Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipokutana kwa mazungumzo na Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Elias Mpedi Magosi wakati wa ziara yake ya kikazi nchini hivi karibuni.



Mhe. Dkt. Tax amesema lengo kuu la Jumuiya hiyo ni kuziwezesha kujikomboa kiuchumi nchi za Kusini mwa Afrika. Lakini pia kuhakikisha nchi za ukanda huo zinakuwa na amani na utulivu, hivyo Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi zozote zinazofanywa na Sekretarieti hiyo ili kufikia malengo hayo.



Pia alivitaja vipaumbele vya Tanzania kwenye Jumuiya hiyo kuwa ni pamoja na Amani na Usalama, Kilimo, Uchumi wa Buluu, maendeleo ya Miundombinu na uchumi  wa kidigitali.



Ameongeza kusema kazi kubwa ya Sekretarieti hiyo ni kusimamia kwa bidii utekelezaji wa mipango, itifaki, na mikataba mbalimbali iliyokwishapitishwa au kuridhiwa na nchi wanachama.


"Nakushukuru sana kwa kutenga muda wako na kuja kutembelea Tanzania. Nakupongeza pia kwa kazi nzuri unayoendelea kufanya ya kuongoza chombo muhimu kinachosimia utekelezaji wa malengo ya Jumuiya yetu. Ushauri wangu kwako ni kuendelea kusimamia utekelezaji wa masuala mbalimbali ambayo tayari yapo kwa ajili ya utekelezaji" alisema Mhe. Dkt. Tax.



Kadhalika alimkumbusha Mhe. Magosi kuendeleza jitihada za kutangaza majukumu na umuhimu wa Jumuiya hiyo katika Nchi Wanachama kwani bado Agenda na Madhumuni ya Jumuiya hayajulikani ipasavyo miongoni mwa wananchi katika Nchi Wanachama.

 

Kwa upande  wake, Mhe. Magosi alitumia fursa hiyo kumpongeza Mhe. Dkt. Tax kwa kuteuliwa kwenye wadhifa huo mpya na kumuahidi ushirikiano wake binafsi na kutoka katika Sekretarieti. Pia alimpongeza kwa uongozi makini wa miaka nane kama Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya SADC  hususan katika uandaaji wa nyaraka ikiwemo  Mpango Mkakati wa Maendeleo wa SADC wa mwaka 2020-2030.



Pia aliipongeza Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa Kituo cha Kikanda cha Kupambana na Ugaidi na kwamba uwepo wa kituo hicho hapa nchini kunadhihirisha utayari wa Tanzania katika kuhakikisha suala la usalama katika kanda linapewa kipaumbele.



Wakati wa ziara hiyo ya siku mbili hapa nchini kuanzia tarehe 24 hadi 25 Oktoba, 2022, Mhe. Magosi amekutana kwa mazungumzo na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametembelea Kituo cha Kikanda cha Kupambana na Ugaidi pamoja na Bohari Kuu ya Dawa (MSD). 

 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, Mhe. Elias Masego alipomtembelea jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Mhe. Masego yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 24 hadi 25 Oktoba 2022.
Mhe. Masego akizungumza wakati wa kikao kati yake na Mhe. Dkt. Tax
Ujumbe uliofuatana na Mhe. Masego wakifutilia kikao

Ujumbe wa Tanzania akiwemo Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola (kushoto) wakifuatilia mazungumzo
Mhe. Masego akimpatia zawadi Mhe. Dkt. Tax

Picha ya pamoja
Mhe. Masego akizunguza wakati alipotembelea Kituo cha Kikanda cha SADC cha Kupambana na Ugaidi kilichopo Dar es Salaam

Mhe. Masego alipotembelea Kituo cha Kikanda cha SADC cha Kupambana na Ugaidi 
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, Balozi Kayola (kushoto) wakati wa ziara ya Mhe. Masego kwenye Kituo cha Kupambana na Ugaidi 
Kikao kikiendelea
Kaimu Mkurugenzi wa Bahari Kuu ya Dawa (MSD), Bw. Leopold Shayo akizungumza wakati wa ziara ya Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Elias Masego kwenye Bohari hiyo. Kushoto ni Mhe. Masego akimsikiliza. Mhe. Masego ametembelea Bohari hiyo kutokana na kushinda zabuni ya kusambaza dawa na vifaa tiba kwa nchi za SADC
Kikao kati ya Mhe. Masego na MSD kikiendelea
Kaimu Mkurugenzi wa MSD, Bw. Shayo akimsikiliza Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Masego (hayupo pichani)
Mhe. Masego akizungumza alipotembelea MSD
Mazungumzo yakiendelea

Mhe. Maseko akipokea zawadi ya barakoa zinazotengenezwa na MSD kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa MSD, Bw. Shayo. 
Picha ya pamoja




























 

TANZANIA YAIKUMBUSHA JUMUIYA YA KIMATAIFA KUISADIA AFRIKA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

Tanzania imeikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza ahadi  yake ya  kuzisaidia kiuchumi nchi za Afrika ili kuziwezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotokana na mabadiliko ya Tabianchini kama makubaliano ya  Mkataba wa Paris  yanavyoelekeza.


Wito huo umetolewa na  Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro wakati akihutubia maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja yaliyofanyika jijini Dar es Salaam leo tarehe 24 Oktoba 2022.



Amesema  Mkataba huo unaitaka Jumuiya ya Kimataifa  kuzisaidia nchi za Afrika katika maeneo mbalimbali ikiwemo kujenga uwezo, kubadilishana  teknolojia na kuhakikisha nchi hizo  kiuchumi ili kuziwezesha kujitegemea katika kukabiliana na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.



“Wiki mbili zijazo kuanzia leo, Mkutano wa 27 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi utafanyika Sharm El Sheikh, Misri. Ni kwa muktadha huo tunahitaji kuikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kwamba pamoja na mchango mdogo wa Afrika katika ongezeko la joto duniani, bado Afrika ni Bara linaloathirika zaidi na mabadiliko hayo kutokana na uwezo mdogo wa kukabiliana na changamoto hizo. Hivyo, tunaikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kutimiza ahadi kulingana na maelekezo katika  Mkataba wa Paris,’’ amesema Mhe. Dkt. Ndumbaro.



Aidha,  Mhe. Dkt. Ndumbaro amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa katika kutekeleza program mbalimbali za maendeleo nchini ikiwa ni pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu kwa manufaa ya wananchi.



Mhe. Dkt. Ndumbaro amesema, Tanzania inapoungana na ulimwengu mzima kuadhimisha miaka 77 ya Umoja wa Mataifa ni kielelezo kinachowakumbusha wadau wote nchini kujiimarisha katika ushirikiano ili kuiwezesha Tanzania kutekeleza pamoja na mambo mengine Mpango wake wa Maendeleo wa Miaka Mitano; Malengo ya Maendeleo Endelevu na Mpango wa Tatu wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano.



Amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inayosema “Maendeleo Yanayozingatia Ujumuishwaji wa Makundi yote” imebeba ujumbe mzito unaomkumbusha kila mmoja kuungana na kutafuta suluhu kwa changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia pasipo kumwacha mtu yoyote nyuma.



Pia amesema Tanzania ipo kwenye hatua za mapitio ya utekelezwaji  wa Malengo ya Maendeleo Endelevu na kuwataka wadau mbalimbali kushirikiana nayo ili kufanikisha mapitio hayo.


Vilevile, wakati wa maadhimisho hayo,  Mhe. Dkt. Ndumbaro ameuomba Umoja wa Mataifa kuitambua Lugha ya Kiswahili kama Lugha rasmi ya Umoja huo.



“Tunapoadhimisha miaka 77 ya Umoja wa Mataifa, Tanzania inaikumbusha dunia kuwa wakati umefika sasa wa kuridhia Kiswahili kuwa miongoni mwa Lugha rasmi za Umoja huo” alisema Dkt. Ndumbaro.



Kwa upande wake, Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Kimataifa nchini, Bw. Zlatan Milisic ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kuhifadhi wakimbizi na kwamba Umoja wa Mataifa na Taasisi zake utaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuwaletea wananchi maendeleo.



Amesema Umoja huo unachangia katika miradi mbalimbali ya  kuwainua kiuchumi wanawake na vijana walio katika mazingira magumu ikiwemo kuchangia katika uunzishwaji wa madawati ya jinsia yaliyo chini ya Jeshi la Polisi ambapo kwa mwaka huu madawati 400 yameanzishwa nchini kote.



Wakati wa maadhimisho hayo, Mhe. Dkt. Ndumbaro alipata fursa ya kuzindua Tovuti ya Kwanza ya Umoja wa Mataifa inayochapisha maudhui yake kwa Lugha ya Kiswahili.



Maadhimisho hayo ya aina yake yamehudhuriwa na Viongozi na wadau mbalimbali wakiwemo Mhe. Tabia Mwita, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Zanzibar, Mhe. Lela Muhammed Mussa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar, Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyopo nchini.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akihutubia wakati wa maadhimisho ya Miaka 77 ya Umoja wa Mataifa. aadhimisho hayo ambayo yalibeba kaulimbiu isemayo "Maendeleo yanayozingatia Ujumuishwaji wa Makundi Yote" yamefanyika kwenye Viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam hivi karibuni
Mhe. Dkt. Ndumbaro akiwa na Viongozi wengine walioshiriki maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Robert Kahendaguza na wa tatu kulia ni Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Mhe. Bw. Zlatan Millisic
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Mhe. Zlatan Milisic akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa
Mhe. Dkt. Ndumbaro akifuatilia Wimbo wa Taifa wakati wa maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa
Mhe. Dkt. Ndumbaro akikagua gwaride la heshima liloandaliwa maalum kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa
Mhe. Dkt. Ndumbaro akishuhudiwa tukio maalum la upandishaji wa Bendera ya Umoja wa Mataifa kama ishara ya kuadhimisha miaka 77 ya Umoja huo

Mkurugenzi Msaidizi katika Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa ambaye pia alikuwa Mshereheshaji wa maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa , Bi. Ellen Maduhu akitoa mwongozo wa maadhimisho hayo kwa washiriki
Wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari ya Kibasila ya jijini Dar es Salaam wakitoa burudani na elimu kuhusu historia ya Umoja wa Mataifa kupitia sanaa ya uimbaji
Mhe. Dkt. Ndumbaro akizindua rasmi Tovuti ya Umoja wa Mataifa inayochapisha maudhui yake kwa Lugha ya Kiswahili
Picha ya pamoja




 

TANZANIA YAJIDHATITI KUSHIRIKIANA NA WADAU KUKUZA UCHUMI



 

Monday, October 24, 2022

RAIS TSHISEKEDI AMALIZA ZIARA YA KITAIFA NCHINI

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mhe. Felix Tshisekedi amemaliza ziara ya Kitaifa ya siku mbili aliyoifanya nchini tarehe 23 na 24 Oktoba, 2022. 

Rais. Tshisekedi ameagwa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. 

Mapema kabla ya kuondoka, Mhe. Rais Tshisekedi ametembelea mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) Jijini Dar es Salaam na kujionea hatua mradi huo ulipofikia. 

Rais Tshisekedi alipotembelea mradi wa ujenzi wa SGR, aliambatana na Waziri wa Maambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax pamoja na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa.

Juni 14, 2019 Rais Tshisekedi kwa mara ya kwanza alifanya ziara ya siku mbili nchini Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania - (TRC), Bw. Masanja Kadogosa wakati Rais Tshisekedi alipofanya ziara katika mradi wa ujenzi wa SGR Jijini Dar es Salaam. Mhe. Tshisekedi ameambatana na Waziri wa Maambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax pamoja na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa. 


Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi akimuuliza jambo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania - (TRC), Bw. Masanja Kadogosa wakati Rais Tshisekedi alipofanya ziara katika mradi wa ujenzi wa SGR Jijini Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi wakiwa katika jukwaa la salamu za heshima za kijeshi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam kabla ya Rais Tshisekedi kuondoka nchini baada ya kumaliza ziara yake

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi akiagana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam baada ya kumaliza ziara yake nchini

Rais wa Jamhuri ya KIdemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi akimuaga Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam baada ya kumaliza ziara yake nchini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi waandamizi wa serikali wakimuaga Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Félix Tshisekedi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam baada ya kuhitimisha ziara yake nchini





Sunday, October 23, 2022

TANZANIA, DRC ZAKUBALIANA KUIMARISHA BIASHARA NA UCHUMI

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan inaedelea kuudhirihishia ulimwengu kuwa imedhamiria kushirikiana na wadau wote, zikiwemo nchi jirani ili kuleta manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa pande zote.

Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) nchini, Mhe. Felix Tshisekedi ambayo ni mwendelezo wa ziara kadhaa za viongozi wa kitaifa na mashirika ya kimataifa nchini ni kielelezo cha wazi cha kutambua nguvu ya ushirikiano katika kukuza uchumi wa nchi na dunia kwa ujumla.

Rais Samia na mgeni wake, Rais Tshiseked katika mazungumzo yao yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar Es Salaam tarehe 23 Oktoba 2022, waliafikiana nchi zao ziongeze nguvu kuimarisha ushirikiano katika sekta za kiuchumi, miundombinu, biashara, usafirishaji, uwekezaji, ulinzi, usalama na mawasiliano.

Rais Samia aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamekubaliana kuondoa vikwazo vyote visivyo vya kibishara ili kukuza biashara na kwamba mawaziri wa biashara wa pande zote mbili wameagizwa  kulifanyia kazi suala hilo haraka iwezekanavyo. 

"Ikumbukwe DRC ni mwanachama mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na katika mikakati ya kuendeleleza miundombinu ya Jumuiya hiyo, kuna mpango wa kujenga ushoroba wa kati utakaounganisha Tanzania na DRC ili kukuza biashara na mtangamano baina ya nchi wanachama', alisema Rais Samia.

Kwa upande wake, Rais Tshisekedi alisisitiza umuhimu wa kuimarisha usalama kwa sababu bila ya amani na usalama hakuna miradi itakayoweza kutekelezwa

“Sisi kwetu DRC usalama ni muhimu sana na ndiyo maana mimi kama Rais nimeweka mkazo wa kujenga na kuimarisha uhusiano wa kindugu na majirani zetu,” alisema Rais Tshisekedi.

Rais Samia na mgeni wake walishuhudia uwekaji saini wa Mkataba wa Teknolojia ya Habari na Posta uliosainiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye na Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Mhe. Christophe Lutundula.

Uwekaji saini wa mkataba huo umekuja muda mfupi baada ya nchi hizo pia kusaini Hati ya Makubaliano ya kushirikiana katika masuala ya ulinzi na usalama wakati wa Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya nchi hizo uliofanyika Jijini Dar Es Salaam mwezi Septemba 2022. Ikumbukwe pia Rais Samia alifanya ziara ya kitaifa nchini DRC mwezi Agosti 2022 mara baada ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika nchini humo ambapo Rais Tshesiked alikabidhiwa uenyekiti wa Jumuiya hiyo.

Ziara hii ya Rais wa DRC na nyingine zilizofanywa na viongozi wa ngazi tofauti baina ya nchi hizi mbili pamoja na uamuzi wa Tanzania wa kufungua Ofisi ya Konseli Kuu katika mji wa Lubumbashi vinatajwa kuwa vitaimarisha uhusiano na kukuza biashara baina ya mataifa hayo mawili yenye utajiri mkubwa wa maliasili.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi wakishuhudia utiaji saini wa Mkataba wa Teknolojia ya Habari na Posta uliosainiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye na Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Mhe. Christophe Lutundula Ikulu Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax akifuatilia Mkutano wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi na waandishi wa Habari uliofanyika Jijini Dar es Salaam