|
Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mhe. Baraka Luvanda (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mauzo wa Kampuni ya Tully’s inayomiliki migahawa maarufu ya Tully's nchini Japan, Bw. Daisuke Shindo wakati wa uzinduzi wa uuzaji rasmi wa kahawa ya Tanzania kwenye migahawa hiyo katika hafla iliyofanyika jijini Tokyo tarehe 9 Juni 2023 |
|
Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mhe. Baraka Luvanda (katikati) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mauzo wa Kampuni ya Tully’s inayomiliki migahawa maarufu ya Tully's nchini Japan, Bw. Daisuke Shindo (kulia) pamoja na Meneja Mkuu wa Idara ya Bidhaa za Vinywaji wa Kampuni
ya Marubeni ambayo ni mbia wa Tully’s na miongoni mwa kampuni zinazosafirisha
kwa wingi kahawa kutoka Tanzania kuingia nchini Japan, Bw. Masahiko Yoshimura (kushoto) wakati wa uzinduzi wa uuzaji rasmi wa kahawa ya Tanzania kwenye migahawa hiyo katika hafla iliyofanyika jijini Tokyo tarehe 9 Juni 2023 |
|
Mhe. Balozi Luvanda (wa tatu kulia) akiwa na Bw. Shindo ( wa tatu kushoto) na wadau wengine wa Japan wakati wa zoezi la uonjaji wa kahawa ya Tanzania |
|
Wadau mbalimbali wa Japan wakishiriki hafla ya uzinduzi wa uuzaji wa kahawa ya Tanzania kwenye migahawa ya Tully's ya nchini Japan |
|
Mhe. Balozi Luvanda (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Bw. Shindo (wa tatu kulia) na Bw. Yoshimura (wa tatu kushoto) na Maafisa kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Japan na wadau wengine wakati wa uzinduzi wa uuzaji wa kahawa ya Tanzania kwenye migahawa ya Tully's iliyopo Japan |
|
Balozi Luvanda akiwa katika picha na Mkurugenzi Mtendaji wa Mauzo wa Kampuni ya Tully’s inayomiliki migahawa maarufu ya Tully's nchini Japan, Bw. Daisuke Shindo |
|
Mhe. Balozi Luvanda akionesha baadhi ya kahawa za Tanzania zinazouzwa nchini Japan |
|
Mhe. Balozi Luvanda akihojiwa na Mtangazaji kutoka Shirika la Utangazaji la Japan-NHK, Idhaa ya Kiswahili kuhusu jitihada za Ubalozi zilivyofanikisha uuzaji wa kahawa ya Tanzania kwenye migahawa maarufu ya Tully's ya nchini Japan. |
|
Kahawa ya Tanzania kama inavyoonekana pichani |
==========================================================
Kampuni ya Tully’s inayomiliki migahawa
maarufu ya TULLY’s imezindua rasmi uuzaji wa kahawa ya Tanzania katika migahawa
yao yote
700 iliyoko nchini Japan katika hafla
iliyofanyika jijini Tokyo tarehe 9 Juni 2023.
Uzinduzi huo ambao ulienda
sambamba na zoezi la uonjaji wa kahawa ya Tanzania, ulishuhudiwa na Balozi wa Tanzania
nchini Japan, Mhe. Baraka Luvanda; Mkurugenzi
Mtendaji wa Mauzo wa Tully’s; Bw. Daisuke Shindo pamoja na Meneja Mkuu wa Idara
ya Bidhaa za Vinywaji wa Kampuni ya Marubeni ambayo ni mbia wa Tully’s na
miongoni mwa kampuni zinazosafirisha kwa wingi kahawa kutoka Tanzania kuingia
nchini Japan, Bw. Masahiko Yoshimura.
Akitoa
hotuba yake katika uzinduzi huo, Balozi Luvanda alizihakikishia kampuni za Japan, uwepo wa
mazingira wezeshi ya biashara na hata uwekezaji wanapoamua kuwekeza katika
kilimo au sekta nyingine za Tanzania.
Aidha, amelitaja kuwa zao la
kahawa ni miongoni mwa mazao ya kimkakati nchini ambalo linatumika kibiashara kwa
kulipatia Taifa pato kubwa kwa mauzo mengi ya kigeni. Akitolea mfano wa Japan,
alieleza kuwa kwa mwaka, Tanzania
inauza kahawa yake Japan, kwa wastani wa asilimia 33 ya kahawa inayolimwa nchini,
ambayo ni sawa na wastani wa kilogramu million 15 (tani 15,000) ya kahawa yote
ya Tanzania inayouzwa nchini Japan.
Balozi
Luvanda alieleza kuwa, soko la kahawa nchini Japan bado ni kubwa, ikilinganishwa
na matumizi na uhitaji wa Japan ambapo, Japan inahitaji wastani wa kilogramu milioni
453 (tani 453,000) za kahawa kwa mwaka na kutoa rai kwa watanzania hususan,
wakulima wa zao la kahawa, watayarishaji, wasafirishaji na wafanyabiashara wa
zao hili kuchangamkia fursa ya soko kubwa la Japan ambalo linakua siku hadi
siku.
“Napenda
kutoa wito kwa watanzania wenzangu kuzingatia ubora wa viwango kwa mazao tunayolima
nchini kwani nchi nyingi tunazouza bidhaa zetu hususan, hapa Japan wanazingatia
sana viwango. Hivyo, ili kulikamata soko hili la Japan ipasavyo, inatupasa kwenda
sambamba na mahitaji ya kidunia ikiwemo, uzalishaji kwa viwango bora” alieleza
Balozi Luvanda.
Vilevile,
Balozi Luvanda alieleza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya
kilimo kwa kuwekeza katika miradi ya muda mrefu na mifupi pamoja na maeneo ya
msingi ya kutatua changamoto za kilimo kuanzia shambani hadi sokoni ili kujihakikishia
uhakika wa chakula, kulisha wengine kibiashara duniani, na pia wakulima kujipatia
kipato cha kutosha ili kupunguza umaskini.
“Serikali
ya Tanzania kwa kasi kubwa imewekeza kwenye rasilimali fedha na watu pamoja na uhamasishaji
wa sekta binafsi kuwekeza na kukifanya kilimo kuanza kutoa ajira zenye staha hususan,
kwa vijana na wanawake, ikiwa ni pamoja na hatua ya kuongeza bajeti ya Wizara
ya Kilimo na kujenga msingi imara wa utekelezaji wa mipango ya kilimo yenye kutazama
Tanzania ifikapo mwaka 2050”, alieleza.
Alihitimisha
hotuba yake kwa kuelezea jitihada za ubalozi za kufanikisha azma ya Serikali ya
Tanzania katika mageuzi ya sekta ya kilimo ya kukifanya kuwa biashara. “Ubalozi
unatekeleza jukumu kubwa la kuendelea kutafuta masoko ya bidhaa mbalimbali zinazozalishwa
nchini ikiwemo, mazao ya kilimo kama kahawa, kwa kuzitangaza bidhaa hizo na
kutafuta wawekezaji wa kuendeleza sekta mbalimbali kama vile sekta ya kilimo hususan,
kilimo cha biashara kwa mazao ya kimkakati”, alihitimisha.
Kadhalika,
Balozi Luvanda alihamasisha ushiriki wa
wadau wa kahawa nchini katika Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa ya Mwaka 2023 (World
Specialty Coffee Conference and Exhibition 2023) yatakayofanyika jijini Tokyo
kuanzia tarehe 27 hadi 29 Septemba 2023, ambayo yanaratibiwa na
Ubalozi kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa Tanzania. Tanzania
ilishiriki kikamilifu katika Maonesho hayo kwa mwaka 2023 na manufaa yake
yameonekana.
Tully’s Co. Ltd., inamiliki
migahawa takribani 700 nchini Japan na imejipatia umaarufu mkubwa katika
biashara ya uuzaji wa kahawa za aina mbalimbali duniani. Kahawa ya Tanzania iliyozinduliwa
ni kutoka Mashamba ya Kahawa ya GDM (GDM Farms) yaliyoko Mbozi mkoani Mbeya.
Kuzinduliwa kwa kahawa ya GDM nchini
Japan kunapandisha zaidi uhakika wa soko la kahawa ya Tanzania nchini Japan
ambayo imejizolea umaarufu mkubwa kwa ubora na radha ya aina yake na kupelekea kupewa
jina maarufu la kibiashara la Kilimanjaro Coffee. Jina
hili hutumika nchini Japan, kwa kahawa zinazozalishwa Tanzania pekee, kwa
kutambua kivutio kikubwa cha Mlima Kilimanjaro uliopo nchini Tanzania.
Tanzania inasifika Japan kwa
kutoa kahawa bora aina ya Arabica (Arabica laini - full washed na
Arabica ngumu - natural) inayolimwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha,
Manyara, Mara, Tanga, Morogoro, Njombe, Iringa, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Kigoma, Songwe
na Mbeya; na kahawa ya Robusta inayolimwa mkoani Kagera.
IMETOLEWA NA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI JAPAN
TAREHE 9 JUNI 2023