Tuesday, September 5, 2023

TANZANIA IMEDHAMIRIA KUMALIZA TATIZO LA NJAA IFIKAPO 2030

Serikali ya Tanzania imeazimia kutimiza lengo namba 2 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG-2) la kuondoa njaa nchini ifikapo mwaka 2030.

 

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 05, 2023 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango alipofungua Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam.

 

Kufikia lengo hilo, Makamu wa Rais amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali kwa lengo sio tu la kuondoa njaa nchini, bali pia kuwa hazina ya chakula katika kanda na duniani kwa ujumla.

 

Ametaja hatua zilizochukuliwa na Serikali kuwa ni pamoja na kukifanya kilimo kuwa uti wa mgongo na injini ya ukuaji wa uchumi jumuishi. Akifafanua vizuri hatua hiyo, Mheshimiwa Makamu wa Rais alisema asilimia 65 ya watu nchini wamejiajiri katika sekta ya kilimo inayokua kwa asilimia 5 kwa mwaka na hivyo kuchangia asilimia 30 ya mapato ya mauzo ya nje, huku asilimia 65 ya malighafi zinazotumika viwandani nchini zikitoka katika sekta ya kilimo ambayo mchango wake katika pato ghafi la nchi ni asilimia 27 na 21 kwa Tanzania Bara na Zanzibar mutawalia.

 

Hatua nyingine iliyochukuliwa na Serikali ni kuongeza bajeti ya kilimo kwa asilimia 70 kutoka Dola za Marekani milioni 120 mwaka 2021/2022 hadi kufikia milioni 397 mwaka 2023/2024. Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza kasi ya mabadiliko ya mifumo katika sekta ya kilimo ili pamoja na mambo mengine, sekta hiyo ikue kwa asilimia 10 kwa mwaka kutoka ukuaji wa asilimia 5.4 ya sasa.

 

Aidha, Mhe. Dkt. Mpango alieleza kuwa Serikali imeweka sera zinazolenga kuinua sekta ya kilimo nchini, kuendesha kilimo kinachozingatia athari za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza uwekezaji katika tafiti na elimu kwa wakulima na umma kwa ujumla.

 

Awali, kabla ya Mhe. Makamu wa Rais hajakaribishwa kuhutubia jukwaa hilo, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe alisema Afrika haiwezi kufikia azma ya mabadiliko ya mifumo katika sekta ya kilimo kama wanawake na vijana hawatashirikishwa ipasavyo na kuwasihi viongozi wa Afrika washirikiane badala ya kushindana.

 

Naye, Rais wa AGRA, Dkt. Agnes Kalibata amesema mkutano wa mwaka huu ni mkubwa na wa aina yake kuliko mikutano yote iliyofanyika katika miaka ya nyuma. Alisema zaidi ya watu 5000 kutoka nchi 70 duniani walijitokeza kujisajili ili kushiriki Mkutano huo na kusababisha sekretarieti kufunga zoezi la usajili kutokana na idadi ya watu kuwa kubwa kuliko iliyotarajiwa. Awali ilikadiriwa kuwa watu 3000 ndiyo watakaojisajili kushiriki mkutano huo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Philip Isdor Mpango akisoma hotuba wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Philip Isdor Mpango na Rais wa AGRA, Dkt. Agnes Kalibata  wakizindua ripoti ya hali ya kilimo ya Afrika (Africa Agriculture Status Report- AASR)

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Philip Isdor Mpango akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali walioshiriki hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere.

Waziri wa Fedha, Mhe. Mwigulu Nchemba akisoma baadhi ya mambo kutoka katika kishikwambi huku Mkutano wa Jukwa la Mifumo ya Chakula ukiendelea katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere.
Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe akifuatilia Mkutano wa Jukwa la Mifumo ya Chakula unaendelea katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere.



MAKATIBU WAKUU SADC WAKUTANA KWA DHARURA KUJADILI HALI YA ULINZI NA USALAMA NCHINI DRC

Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Kamati ya Utatu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) uliofanyika kwa mtandao.

Balozi Shelukindo ameshiriki katika Mkutano huo akiwa katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine, mkutano umejadili hali ya ulinzi na usalama mashariki mwa DRC. 

Mkutano huo umefuatiwa na Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC MCO) ambapo ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo umeongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.)

Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akichangia jambo katika Mkutano wa Kamati ya Utatu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) uliofanyika kwa mtandao katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri.


Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akiongoza ujumbe katika Mkutano wa Kamati ya Utatu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) uliofanyika kwa mtandao katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri.

Mkutano wa Kamati ya Utatu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) ukiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



WAZIRI MAKAMBA ATEMBELEA ENEO LITAKALOJENGWA UBALOZI NAIROBI , KENYA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (wa tatu kushoto) katika picha ya pamoja na maafisa Ubalozi na wakandarasi alipotembelea kiwanja cha Ubalozi wa Tanzania kilichopo eneo la UpperHill, Nairobi Kenya.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (wa tatu kushoto) katika picha ya pamoja na maafisa Ubalozi na wakandarasi alipotembelea kiwanja cha Ubalozi wa Tanzania kilichopo eneo la UpperHill, Nairobi Kenya.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (wa tatu kushoto) katika picha ya pamoja na maafisa Ubalozi na wakandarasi alipotembelea kiwanja cha Ubalozi wa Tanzania kilichopo eneo la UpperHill, Nairobi Kenya.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba atembelea kiwanja cha Ubalozi wa Tanzania kilichopo UpperHill, Nairobi Kenya. Ziara hiyo ameifanya tarehe 4 Septemba 2023 kwa lengo kukagua maandalizi ya kuanza ujenzi wa jengo la Ubalozi na kitega uchumi

Akiwa kwenye kiwanja hicho, Waziri Makamba amejionea baadhi ya mahitaji na vifaa muhimu ambavyo vimeanza kukusanywa na Mkandarasi tayari kuanza ujenzi huo.

Mhe. Waziri yuko Nairobi, nchini Kenya kuhudhuria Mkutano wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi unaofanyika Jijini Nairobi.

Monday, September 4, 2023

TANZANIA KUIUNGA MKONO SAUDI ARABIA EXPO 2023

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeahidi kuiunga mkono Saudi Arabia kuwa mwenyeji wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara mwaka 2030 (EXPO 2030).

Ahadi hiyo imeelezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo alipoelezea yaliyojiri katika mkutano kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mjumbe Maalum wa Mfalme wa Saudi Arabia, Mhe. Ahmed Abdulaziz Kattan uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Balozi Shelukindo amesema katika kikao hicho Mhe. Rais amemhakikishia mjumbe huyo maalum kuwa Tanzania itashiriki mkutano ya Nchi za Kiarabu na Afrika (Afro Arab Summit) na Mkutano kati ya Saudi Arabia na Nchi za Afrika itakayofanyika Jijini Riyadh mwezi Novemba 2023.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amemhakikishia mjumbe huyo Maalum kuwa Tanzania itaiunga mkono Saudi Arabia kuwa mwenyeji wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya mwaka 2030 alisema Dkt. Shelukindo.

Balozi Shelukindo pia aliongeza kuwa Mhe. Rais amemhakikishia mjumbe huyo kuwa Tanzania itashiriki Mkutano kati ya Nchi za Kiarabu na Afrika (Afro Arab Summit) na Mkutano kati ya Saudi Arabia na Nchi za Afrika inayotarajiwa kufanyika Jijini Riyadh, Saudi Arabia mwezi Novemba 2023.

Naye Mjumbe Maalum wa Mfalme wa Saudi Arabia, Mhe. Ahmed Abdulaziz Kattan amesema Saudi Arabia inaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kukubali kuiunga mkono kuwa mwenyeji wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya mwaka 2030 (EXPO 2030)

“Kwa niaba ya Serikali ya Saudi Arabia tunaishukuru sana Serikali ya Tanzania kwa kuahidi kutuunga mkono kuwa mwenyeji wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya mwaka 2030 (EXPO 2030),” alisema Mhe. Kattan.

Aliongeza kuwa Saudi Arabia inamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kitendo cha kukubali Tanzania ishiriki katika Mikutano kati ya Nchi za Kiarabu na Afrika (Afro Arab Summit) na Mkutano kati ya Saudi Arabia na Nchi za Afrika itakayofanyika Jijini Riyadh mwezi Novemba 2023

“Kwa niaba ya Serikali ya Saudi Arabia namshukuru Mheshimwa Rais kwa kukubali kutuunga mkono kuwa mwenyeji wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya EXPO 2030 na kukubali kushiriki mikutano kati ya Nchi za Kiarabu na Afrika (Afro Arab Summit) na Mkutano kati ya Saudi Arabia na Nchi za Afrika itakayofanyika Jijini Riyadh mwezi Novemba 2023,” aliongeza Mhe. Kattan.

Amesema katika kikao hicho wamejadili pia masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Saudi Arabia na Tanzania katika nyanja mbalimbali.  

Tanzania na Saudi Arabi zimekuwa na uhusiano mzuri na zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali hususan utalii, biashara za bidhaa za nyama, matunda na mazao mengine ya chakula.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza na Mjumbe Maalum wa Mfalme wa Saudi Arabia, Mhe. Ahmed Abdulaziz Qattan katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mazungumzo baina ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na Mjumbe Maalum wa Mfalme wa Saudi Arabia, Mhe. Ahmed Abdulaziz Qattan yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. Wengine pichani ni Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Ali Jabir Mwadini na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga.

Mazungumzo baina ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na Mjumbe Maalum wa Mfalme wa Saudi Arabia, Mhe. Ahmed Abdulaziz Qattan yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. Wengine pichani ni Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Ali Jabir Mwadini na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na Mjumbe Maalum wa Mfalme wa Saudi Arabia, Mhe. Ahmed Abdulaziz Qattan wakieleza yaliyojiri katika mkutano kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mjumbe Maalum wa Mfalme wa Saudi Arabia Ikulu Jijini Dar es Salaam  




Wednesday, August 30, 2023

DKT. SHELUKINDO AHIMIZA WELEDI KATIKA KUIMARISHA DIPLOMASIA YA UCHUMI


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza na Watumishi wa Wizara (hawapo pichani) kwenye kikoa kilichofanyika Ukumbi wa Mtakatifu Gasper jijini Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amewataka watumishi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa maarifa, ubunifu na kitimu ili kutimiza azma ya Serikali ya awamu ya sita ya kuimarisha diplomasia ya uchumi.

Balozi Dkt. Shelukindo ametoa rai hiyo Agosti, 30, 2023 jijini Dodoma w 

Balozi Shelukindo alisisitiza umuhimu wa watumishi kuboresha maarifa yao kila mara kwa kusoma vitabu ili wawe na ujuzi na mbinu za kutosha za kutekeleza majukumu yanayowakabili ambayo yanabadilika kulingana na wakati na teknolojia.

Dkt. Shelukindo aliwahimiza watumishi hao ambayo Wizara wanayoitumikia ni mtambuka kuhakikisha wanafuatilia utekelezaji wa makubaliano ambayo nchi imesaini na nchi nyingine kutoka kwa wadau wote ili iweze kufaidika na makubaliano hayo.

Tuwe wepesi kujibu wadau wetu tanaofanya nao kazi na kuhakikisha tunatoa huduma bora kwa wateja wa Wizara, huku tukizingatia ufanisi na hatimaye kuleta tija kwa nchi”, Balozi Shelukindo alisisitiza.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akifuatilia kikao cha watumishi wa Wizara kilichokuwa kikiendelea

Walioketi; Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (katika), Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama na Kaimu Naibu Katibu Mkuu Balozi Stephen P. Mbundi (kushoto) na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu Bi. Chiku Kiguhe (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi kwenye kikao cha watumishi wa Wizara kilichokuwa kikiendelea
Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama na Kaimu Naibu Katibu Mkuu Balozi Stephen P. Mbundi akifuatilia kikao cha watumishi wa Wizara kilichokuwa kikiendelea
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu Bi. Chiku Kiguhe akifafanua jambo kwenye kikao cha watumishi wa Wizara kilichofanyika kwenye jijini Dodoma. 

Sehemu ya Menejimenti ya Wizara wakifuatilia kikao kilichokuwa kikiendelea
Watumishi wa Wizara wakifuatilia kikao
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu Bi. Chiku Kiguhe akifuatilia kikoa cha Watumishi kilichokuwa kikiendelea
Picha ya pamoja Meza Kuu na Menejimenti ya Wizara
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Balozi Swahiba Mndeme akizungumza kwenye kikao cha Watumishi wa Wizara kilichofanyika jijini Dodoma
Sehemu ya Watumishi wakifuatilia kikao

Kikao kikiendelea

Sehemu ya Menejimenti ya Wizara wakifuatilia kikao kilichokuwa kikiendelea

Sehemu ya Menejimenti ya Wizara wakifuatilia kikao cha watumishi wa Wizara kilichokuwa kikiendelea

BALOZI SHELUKINDO AIHAKIKISHIA USHIRIKIANO WFP


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akisalimiana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP), Bi. Sarah Gordon-Gibson walipokutana kwa mazungumzo jijini Dodoma


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amemhakikishia ushirikiano Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP), Bi. Sarah Gordon-Gibson.

Balozi Dkt. Shelukindo ametoa ahadi hiyo alipokutana na Bi Gibson aliyemtembelea Ofisini kwake jijini Dodoma.

Katika mazungumzo yao viongozi hao wamejikita katika kuimarisha ushirikiano na kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano.

Balozi Shelukindo ameeleza kuwa Tanzania inatambua mchango mkubwa unaotolewa na WFP katika ukanda wa Afrika na Tanzania katika utekelezaji wa vipaumbele vyake.

“Tanzania chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua mchango wa WFP hivyo, itaendelea kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya kitaifa na kikanda.” Alisema Dkt. Shelukindo.

Naye Bi. Sarah ameeleza kuwa katika mpango mkakati wa miaka mitano (5) (2022-2027) Shirika hilo limejielekeza katika usaidizi wa masuala ya kibinadamu kwa wakimbizi waliopo Kigoma, shughuli za maendeleo kwa nchi ya Tanzania na Watanzania kwakuwa ongezeko la idadai ya watu kupitia uwepo wa wakimbizis linaathiri mfumo wa nchi katika namna mbalimbali.

Maeneo mengine ni pamoja na kujenga uwezo katika mpango wa tahadhari za kukabiliana na majanga, vifaa vya TEHAMA, lishe kwa jamii hususan katika uzalishaji wa vyakula na uelewa juu ya lishe bora ili kuondoa utapiamlo na usaidizi wa wanawake na watoto.

Kadhalika, WFP imeweka mkazo katika kilimo cha mahindi, maharage na mtama, kuongeza maeneo mapya ya usaidizi katika uzalishaji wa maua, matunda na mbogamboga na kujenga uwezo katika kukuza mnyororo wa thamani wa mazao ya chakula na biashara kuanzia kwenye uzalishaji hadi usambazaji kupitia bandari za Dar es Salaam, Kigoma na Mwanza. 

WFP imeweka mpango wa kushirikiana na Shirika la Reli (TRC) nchini ili kuwezesha kuwa na vituo vya ukusanyaji wa vyakula na kuwezesha usafirishaji wa vakula hivyo kwa walengwa. 

WFP kwasasa ina ofisi katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na inatarajiwa kufungua ofisi mpya mkoani Arusha.
Mazungumzo yakiendelea 

 Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) Bi. Sarah Gordon-Gibson akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo yaliyofanyika jijini Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) Bi. Sarah Gordon-Gibson katika picha ya pamoja

Picha ya pamoja











Tuesday, August 29, 2023

TANZANIA INATHAMINI MCHANGO WA ASASI ZA KIRAIA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema inathamini mchango wa Asasi za Kiraia katika kutekeleza mipango na sera mbalimbali za maendeleo.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amebainisha hayo wakati wa uzinduzi wa Warsha ya Baraza la Umoja wa Afrika la Uchumi, Kijamii, na Utamaduni la Umoja wa Afrika (ECOSSOC) Jijini Dar es Salaam

Dkt. Shelukindo amesema kuwa Serikali ya Tanzania chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inathamini mchango wa Asasi za Kiraia ambazo hushiriki kwa kiasi kikubwa katika kutekeleza  shughuli mbalimbali zinazofanywa na Serikali. Hivyo, ni vyema kuwa na asasi za kiraia zenye ubora ambazo zitaleta mchango chanya katika maendeleo.

“Serikali imekuwa ikipanga Mipango na Sera za maendeleo ambayo utekelezaji wake hufanywa na wadau mbalimbali ikiwemo Asasi za Kiraia. 

Hivyo, utekelezaji wa sera na mipango hiyo inahitaji asasi za kiraia zenye ubora,” alisema Balozi Shelukindo

“Nimeona mada mbalimbali katika Warsha ya leo ambazo zinazungumzia masuala mengi, ikiwemo misingi ya kidemokrasia, haki za binadamu, utawala bora na vitu vya msingi katika kukuza uchumi wa nchi yetu ambapo vitu vyote vinakwenda sambamba,” aliongeza Dkt. Shelukindo.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania Nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Afrika (AU), Balozi Innocent Shiyo amesema Warsha hiyo ni muhimu ambapo mwaka 2002, uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) uliibadilishwa na kugeuzwa kuwa Umoja wa Afrika. Lengo la hayo ilikuwa ni kuongeza ushiriki wa wananchi kwenye shughuli za Umoja wa Afrika. Ili kufikia azma hiyo, mwaka 2004, Umoja wa Afrika ulipitisha Mkataba wa kuanzisha Baraza la Uchumi, Kijamii na Kitamaduni (ECOSOCC).

“Baraza la Uchumi, Kijamii na Kitamaduni linatoa fursa kwa asasi za kiraia zilizopo Barani Afrika kushiriki kwenye shughuli za Umoja wa Afrika kwa kutoa ushauri kwenye Vyombo vya Kisera vya Umoja wa Afrika na kuwaelimisha pia wananchi kuhusu mipango na mikakati mbalimbali ya Umoja wa Afrika ili kurahisha utekelezaji wake,” alisema Balozi Shiyo.

Balozi Shiyo aliongeza kuwa utendaji kazi wa Baraza la Uchumi, Kijamii na Kitamaduni la Umoja wa Afrika hufanyika katika ngazi ya Kanda, ambapo kila nchi inawakilishwa kwenye Kamati Tendaji (Permanent General Assembly). Sambamba na hilo, kila nchi ina jukumu la kuanzisha Jukwaa la Kitaifa (ECOSOCC National Chapters) ili kuhamasisha asasi nyingi zaidi za kiraia kushiriki kwenye masuala ya Umoja wa Afrika.

“Lengo la warsha ni kuhamasisha na kuongeza uelewa na kuzijengea uwezo wa Asasi za Kiraia za Tanzania kushiriki kwenye shughuli za Umoja wa Afrika. Pamoja na Mambo mengine, Warsha hii itasaidia kuongeza ushiriki na uelewa wa Asasi za Kiraia na Watanzania kwa ujumla kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Umoja wa Afrika,” aliongeza Balozi Shiyo. 

Naye Mkuu wa Mkuu wa Sekretarieti ya ECOSOCC, Bw. William Carew amesema kuwa ECOSOCC itasaidia kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya Umoja wa Afrika (AU) na Asasi za Kiraia nchini Tanzania. Hivyo kutoa fursa ya jukwaa la ushirikishwaji katika kutafuta Afrika bora.

“lengo letu kama ECOSOCC ni kusaidia kuimarisha ushirikiano kati ya Umoja wa Afrika (AU) na Asasi za Kiraia Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla,” alisema Br. Carew.  

Tanzania ni miongoni mwa nchi ya tano za awali kuanzisha majukwaa ya kitaifa ya Ecosocc ili kuwa karibu na asasi za kiraia kwa lengo la kuhamasisha maendeleo nchini pamoja na kufikia malengo ya Ajenda ya 2063 inayohusu masuala mbalimbali ikiwemo elimu, afya na demokrasia. Mbali na Tanzania, nchi nyingine ni Mauritius, Sierra Leone, Zambia na Misri.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza wakati wa uzinduzi wa Warsha ya Baraza la Umoja wa Afrika la Uchumi, Kijamii, na Utamaduni la Umoja wa Afrika (ECOSSOC) Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Tanzania Nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Afrika (AU), Balozi Innocent Shiyo akizungumza wakati wa uzinduzi wa Warsha ya Baraza la Umoja wa Afrika la Uchumi, Kijamii, na Utamaduni la Umoja wa Afrika (ECOSSOC) Jijini Dar es Salaam

Mkuu wa Mkuu wa Sekretarieti ya ECOSOCC, Bw. William Carew akieleza jambo wakati wa uzinduzi wa Warsha ya Baraza la Umoja wa Afrika la Uchumi, Kijamii, na Utamaduni la Umoja wa Afrika (ECOSSOC) Jijini Dar es Salaam

Sehemu ya Washiriki wakifuatilia Warsha ya Baraza la Umoja wa Afrika la Uchumi, Kijamii, na Utamaduni la Umoja wa Afrika (ECOSSOC) Jijini Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na Balozi wa Tanzania Nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Afrika (AU), Balozi Innocent Shiyo katika picha ya pamoja Washiriki wa Warsha ya Baraza la Umoja wa Afrika la Uchumi, Kijamii, na Utamaduni la Umoja wa Afrika (ECOSSOC) Jijini Dar es Salaam