Tuesday, September 5, 2023

TANZANIA IMEDHAMIRIA KUMALIZA TATIZO LA NJAA IFIKAPO 2030

Serikali ya Tanzania imeazimia kutimiza lengo namba 2 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG-2) la kuondoa njaa nchini ifikapo mwaka 2030.

 

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 05, 2023 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango alipofungua Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam.

 

Kufikia lengo hilo, Makamu wa Rais amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali kwa lengo sio tu la kuondoa njaa nchini, bali pia kuwa hazina ya chakula katika kanda na duniani kwa ujumla.

 

Ametaja hatua zilizochukuliwa na Serikali kuwa ni pamoja na kukifanya kilimo kuwa uti wa mgongo na injini ya ukuaji wa uchumi jumuishi. Akifafanua vizuri hatua hiyo, Mheshimiwa Makamu wa Rais alisema asilimia 65 ya watu nchini wamejiajiri katika sekta ya kilimo inayokua kwa asilimia 5 kwa mwaka na hivyo kuchangia asilimia 30 ya mapato ya mauzo ya nje, huku asilimia 65 ya malighafi zinazotumika viwandani nchini zikitoka katika sekta ya kilimo ambayo mchango wake katika pato ghafi la nchi ni asilimia 27 na 21 kwa Tanzania Bara na Zanzibar mutawalia.

 

Hatua nyingine iliyochukuliwa na Serikali ni kuongeza bajeti ya kilimo kwa asilimia 70 kutoka Dola za Marekani milioni 120 mwaka 2021/2022 hadi kufikia milioni 397 mwaka 2023/2024. Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza kasi ya mabadiliko ya mifumo katika sekta ya kilimo ili pamoja na mambo mengine, sekta hiyo ikue kwa asilimia 10 kwa mwaka kutoka ukuaji wa asilimia 5.4 ya sasa.

 

Aidha, Mhe. Dkt. Mpango alieleza kuwa Serikali imeweka sera zinazolenga kuinua sekta ya kilimo nchini, kuendesha kilimo kinachozingatia athari za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza uwekezaji katika tafiti na elimu kwa wakulima na umma kwa ujumla.

 

Awali, kabla ya Mhe. Makamu wa Rais hajakaribishwa kuhutubia jukwaa hilo, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe alisema Afrika haiwezi kufikia azma ya mabadiliko ya mifumo katika sekta ya kilimo kama wanawake na vijana hawatashirikishwa ipasavyo na kuwasihi viongozi wa Afrika washirikiane badala ya kushindana.

 

Naye, Rais wa AGRA, Dkt. Agnes Kalibata amesema mkutano wa mwaka huu ni mkubwa na wa aina yake kuliko mikutano yote iliyofanyika katika miaka ya nyuma. Alisema zaidi ya watu 5000 kutoka nchi 70 duniani walijitokeza kujisajili ili kushiriki Mkutano huo na kusababisha sekretarieti kufunga zoezi la usajili kutokana na idadi ya watu kuwa kubwa kuliko iliyotarajiwa. Awali ilikadiriwa kuwa watu 3000 ndiyo watakaojisajili kushiriki mkutano huo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Philip Isdor Mpango akisoma hotuba wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Philip Isdor Mpango na Rais wa AGRA, Dkt. Agnes Kalibata  wakizindua ripoti ya hali ya kilimo ya Afrika (Africa Agriculture Status Report- AASR)

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Philip Isdor Mpango akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali walioshiriki hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere.

Waziri wa Fedha, Mhe. Mwigulu Nchemba akisoma baadhi ya mambo kutoka katika kishikwambi huku Mkutano wa Jukwa la Mifumo ya Chakula ukiendelea katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere.
Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe akifuatilia Mkutano wa Jukwa la Mifumo ya Chakula unaendelea katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere.



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.