Wednesday, September 27, 2023

TANZANIA YASHIRIKI KWENYE MAONESHO YA KIMATAIFA YA KAHAWA NCHINI JAPAN,

TANZANIA YASHIRIKI KWENYE MAONESHO YA KIMATAIFA YA KAHAWA NCHINI JAPAN,

Mheshimiwa Baraka Luvanda, Balozi wa Tanzania nchini Japan ameungana na mabalozi pamoja na viongozi mbalimbali wa nchi zinazozalisha kahawa duniani, kwenye hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya 20 ya Kimataifa ya Kahawa nchini Japan (2023 Japan Specialty Coffee Conference & Exhibition) iliyofanyika jijini Tokyo, Japan tarehe 27 Septemba 2023 

Uzinduzi huo umeenda sanjari na Maadhimisho ya Miaka 20 ya Maonesho hayo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2003.

Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa Japan yameandaliwa na Taasisi ya Kahawa ya Japan (Specialty Coffee Association of Japan – SCAJ) na kushirikisha makampuni na taasisi zinazohusika na kahawa zipatazo 250 kutoka nchi zinazozalisha kahawa duniani. Maonesho haya yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 29 Septemba 2023; na kuhudhuriwa na wadau wa kahawa wapatao 45,000 wakiwemo, wazalishaji, wanunuzi na wasafirishaji wa zao hilo.

Tanzania inawakilishwa na Bodi ya Kahawa Tanzania (Tanzania Coffee Board) ambayo, imeshiriki pamoja na wawakilishi wa vyama vya ushirika na makampuni ya Kitanzania yanayohusika na uzalishaji, usafirishaji, uuzaji na ufungashaji wa kahawa yakiwemo, Kagera Cooperative Union (KCU),  Kampuni ya Kaderes Peasants Development (KPD), Kampuni ya Kamal Agro, Kampuni ya TANJA, Kampuni ya Ubumwe na Kampuni ya Interbulk Packaging.

Aidha, katika maonesho hayo, Tanzania ina banda maalum la kuonesha bidhaa za kahawa zinazozalishwa Tanzania, zinajumuisha kahawa iliyochakatwa katika hatua za awali (green coffee) kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania. Pia, kupitia maonesho hayo inaoneshwa na kutangazwa kahawa iliyo tayari kwa ajili ya matumizi ikiwemo, kahawa mumunyifu (instant coffee) inayozalishwa na viwanda vikubwa vya kukaanga kahawa nchini Tanzania vya Amimza, Afri Café na Tanica.

Vilevile, siku ya pili ya maonesho hayo tarehe 28 Septemba 2023,  Tanzania itapata fursa ya kufanya semina maalum kuhusu kahawa ya Tanzania itakayoambatana na zoezi la uonjaji wa sampuli za kahawa za Tanzania (Tanzania Coffee Seminar and Cupping Session) kwa makampuni yapatayo 80 ya ukaangaji (coffee roasters) na usafirishaji kahawa ya nchini Japan. Katika tukio hilo, sampuli za kahawa za wazalishaji na makampuni ya Tanzania yapatayo 30 zitaoneshwa, kutangazwa na kuonjwa kwenye siku hiyo iliyotengwa maalum kwa ajili ya kuitangaza kahawa ya Tanzania. Sampuli hizo ni za kahawa ya Arabica laini (full washed), Arabica ngumu (naturals) na kahawa ya Robusta.

Maonesho haya, ni fursa adhimu katika kukuza soko la kahawa ya Tanzania nchini Japan ambayo ni kahawa pendwa iliyopewa jina maarufu la kibiashara la “Tanzania Kilimanjaro Coffee”.  Jina hili hutumika nchini Japan, kwa kahawa zinazozalishwa Tanzania pekee, kwa kutambua kivutio kikubwa cha Mlima Kilimanjaro uliopo nchini Tanzania.

Tanzania inasifika Japan kwa kutoa kahawa bora aina ya Arabica (Arabica laini - full washed na Arabica ngumu - natural) inayolimwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mara, Tanga, Morogoro, Njombe, Iringa, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Kigoma, Songwe na Mbeya; na kahawa ya Robusta inayolimwa mkoani Kagera.



Uzinduzi wa Maonesho ya 20 ya Kimataifa ya Kahawa nchini Japan (2023 Japan Special Coffe Conference & Exhibition)
Washiriki wakiwa katika banda la Tanzania katika Maonesho ya 20 ya Kimataifa ya Kahawa nchini Japan (2023 Japan Special Coffe Conference & Exhibition)

Washirikiwakiwa katika banda la Tanzania katika Maonesho ya 20 ya Kimataifa ya Kahawa nchini Japan (2023 Japan Special Coffee Conference & Exhibition)

 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.