Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaeleza vijana wanaoshiriki Mkutano wa Mifumo ya Chakula Barani Afrika (AGRF 2023) kuwa Serikali ya Tanzania imejipanga kutumia vyema Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) ili kuboresha sekta ya Kilimo na kukuza upatikaji wa chakula nchini.
Mhe. Dkt. Samia ametoa kauli hiyo alipozungumza na vijana walioko katika Sekta ya kilimo kuhusu jitihada za kukabiliana na changamoto za kutafuta masoko ya mazao ya kilimo wanaoshiriki Mkutano wa Mifumo ya Chakula barani Afrika (AGRF 2023) unaofanyika Jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 5 – 8 Septemba 2023.
Mhe. Rais amesema matumizi ya teknolojia ya kisasa katika sekta ya Kilimo yataleta matokeo chanya na kutoleo mfano wa kutumia trekta za ‘automatic’ na zinavyosaidia kuleta tija katika sekta ya kilimo.
Amesema Serikali ya Tanzania inategemea kufikia mwaka 2025 kuhakikisha robo tatu ya mbegu zinazotumiwa na wakulima zinazalishwa nchini zikiwa na ubora unaokidhi mahitaji kwa kutumia ICT.
“Kutokana na matumizi ya teknolojia ya kisasa tunategemea hadi kufikia mwaka 2025 Serikali itahakikisha robo tatu ya mbegu zinazotumiwa na wakulima zinazalishwa nchini zikiwa na ubora unaokidhi mahitaji kwa msaada wa Tehama,” alisema Rais Samia.
Mhe. Samia akiongelea madhumuni ya programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) amesema imelenga kuwawezesha vijana kushiriki katika kilimo na kuongeza kuwa program hiyo ilianzishwa kwa lengo la kuinua maisha ya vijana na kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo nchini.
“Madhumuni ya BBT ni kuwawezesha vijana kushiriki katika sekta ya kilimo ili kuweza kuinua Maisha yao na kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo,” alisema Rais Samia
Rais Samia ameongeza kuwa pamoja na mambo mengine, malengo ya kimkakati ya BBT ni kuwavuta vijana kushiriki kwenye miradi ya kilimo chenye tija na faida kwa maisha yao.
BBT ilianzishwa mwaka 2022, na tangu ilipoanzishwa imechukua vijana 1,252 na vijana wengine 812 wamejiandikisha kupata mafunzo hayo yanayotolewa kwa miezi minne.
Kadhalika, Rais Samia ameongeza kuwa Tanzania imejipanga kuiendeleza sekta ya kilimo siyo tu kwa manufaa yake bali kwa manufaa ya bara la Afrika na Dunia kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.