Friday, September 29, 2023

TANZANIA YANADI FURSA ZA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA KILIMO KUPITIA MAONESHO YA KIMATAIFA YA KAHAWA NCHINI JAPAN

Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mhe. Baraka Luvanda amewahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Japan kuja kuwekeza nchini kwenye zao la kahawa na mazao mengine ya kimkakati.


Rai hiyo ameitoa hivi karibuni wakati akifungua semina maalum iliyoandaliwa kwa ajili ya Tanzania ikiwa ni siku ya pili ya Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa yaliyofanyika kwa siku tatu nchini Japan kuanzia tarehe 27 hadi 29 Septemba 2023.


Semina hiyo ilipata mwitikio mkubwa kwa kuhudhuriwa na wadau wa kahawa wapatao 80 wa ndani na nje ya Japan ambapo Tanzania ilitumia fursa hiyo kutangaza kahawa ya Tanzania na zoezi la uonjaji  wa sampuli za kahawa ya Tanzania kutoka kampuni 30 zilizopo nchini lilifanyika. Sampuli hizo ni za kahawa ya Arabica laini Arabica ngumu na kahawa ya Robusta.


Tanzania inasifika Japan kwa kutoa kahawa bora aina ya Arabica inayolimwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mara, Tanga, Morogoro, Njombe, Iringa, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Kigoma, Songwe na Mbeya; na kahawa ya Robusta inayolimwa mkoani Kagera.


Mbali na kuinadi Tanzania pamoja na vivutio vyake nchini Japan, kahawa ya Tanzania ni miongoni mwa vivutio hivyo ambapo imeweza kujipatia umaarufu mkubwa kutokana na ladha ya kipekee na kupewa Jina la Kibiashara la Tanzania Kilimanjaro Coffee. Jina hili hutumika nchini Japan kwa kahawa zinazozalishwa Tanzania pekee, kwa kutambua kivutio kikubwa cha Mlima Kilimanjaro uliopo nchini Tanzania.


Kadhalika, Tanzania imeshiriki Maonesho hayo ya Kimataifa ya Kahawa kama mdau  mkubwa wa kahawa duniani ambapo kwa mwaka huu yametimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2003. Maonesho ya mwaka huu, yameshirikisha makampuni na taasisi zinazohusika na kahawa zipatazo 250 kutoka nchi zinazozalisha kahawa duniani na kuhudhuriwa na wadau wa kahawa wapatao 45,000 wakiwemo, wazalishaji na wanunuzi.

Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mhe. Baraka Luvanda (mwenye scarf ya bendera ya Tanzania) akifungua semina maalum iliyoandaliwa wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa yaliyofanyika kwa siku tatu nchini Japan kuanzia tarehe 27 hadi 29 Septemba 2023. Semina hiyo pamoja na mambo mengine ililega kutangaza fursa za uwekezaji zinazopatikana kwenye sekta ya kilimo hapa nchini ikiwemo kilimo cha kahawa

Washiriki wa Semina wakifuatilia hafla ya ufunguzi
Zoezi la uonjaji wa kahawa ya Tanzania likiendelea wakati wa maonesho ya kimataifa ya Kahawa yaliyofanyika Japan kuanzia tarehe 27 hadi 29 Septemba 2023
Balozi Luvanda katika picha ya pamoja na washiriki na wadau wa kahawa kutoka Tanzania na Japan

Picha ya pamoja

 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.