Tanzania imeahidi kuwa
itaendelea kuheshimu na kusimamia misingi ya mtangamano wa bara la Afrika kama
ilivyofundishwa na kuachwa na waasisi wa Taifa hili, ili kufikia Afrika yenye
ustawi na umoja.
Hayo yameelezwa leo Septemba
15, 2023 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
wakati anafungua Kikao cha Umoja wa
Afrika cha Nne cha Kamati Maalumu ya Kitaalam kuhusu Uchukuzi, Miundombinu ya Kikanda
na ya Bara, na Nishati kinachofanyika mjini Zanzibar.
Dkt. Biteko aliwambia
wajumbe wa kikao hicho ambacho kinalenga kutoa mapendekezo ya kisera na miongozo
ya kimkakati katika uendelezaji wa sekta ya miundombinu barani Afrika kuwa,
Tanzania ipo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya miundombinu ambayo msingi
wake ni kuimarisha mtangamano baina ya Tanzania na nchi inazopakana nazo,
Afrika na dunia kwa ujumla.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa yenye urefu wa kilomita
1,800 inayounganisha Bandari ya Dar es Salaam na nchi jirani za Uganda,
Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ujenzi wa Bomba la Mafuta
Ghafi la Afrika Mashariki lenye urefu wa kilomita 1,400 linalounganisha
Tanzania na Uganda, Mradi wa Bwawa la Kuzalisha umeme wa Maji la
Julius Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 kwa ajili ya matumizi ya Tanzania
na nchi jirani na kufufua shirika la ndege ambalo kwa sasa lina ndege 12 zinazoiunganisha
Tanzania na nchi zisizopungua 9 za Afrika.
Dkt. Biteko alisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kushirikiana ili kufikia
matarajio ya mamilioni ya Waafrika ya kuwa na miundombinu ya uhakika. Kufanikisha
hilo, Dkt. Biteko alitoa wito kwa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, washirika wake na wabia wa maendeleo kuimarisha juhudi za utafutaji wa rasilimali fedha
kwa ajili ya kutekeleza miradi ya miundombinu ambayo ni muhimu katika kuimarisha biashara,
kuongeza ajira na kukuza uchumi barani Afrika.
Awali, wakati wa uzinduzi wa ripoti ya miaka
10 ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Miundombinu Barani Afrika (PIDA),
wajumbe waliainisha masuala mbalimbali ya kuzingatia ili awamu ya pili ya
mpango huo, uweze kufanikiwa. Masuala hayo ni pamoja na kuwa na sera
zinazoendana na mabadiliko ya dunia, kushirikisha sekta binafsi katika ujenzi
wa miundombinu na kupeana taarifa muhimu ili kufanikisha uandaaji na
utekelezaji wa miradi ya kipaumbele ya miundombinu.
Kufanyika kwa mkutano huo nchini ni jitihada
za Serikali ya awamu ya sita kupitia Ubalozi wake nchini Ethiopia, chini ya uongozi
wa Balozi Innocent Shiyo za kukuza diplomasia ya uchumi na utalii wa mikutano.
Wajumbe takribani 400 kutoka barani Afrika;
washirika wa maendeleo, kama Benki ya Maendeleo ya Afrika, Exim Bank; Kamisheni
ya Uchumi ya Afrika; watafiti na wanazuoni wa fani mbalimbali duniani wameshiriki
mkutano huo. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.