Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
amezihimiza nchi za Afrika kushirikiana ili kukabiliana na aibu ya baa la njaa,
kwakuwa bara hilo lina asilimia 65 ya ardhi inayofaa kwa kilimo duniani,
asilimia 60 ya utajiri wa rasilimali na maziwa makubwa, nguvu kazi ya kutosha
ya vijana na madini yanayoweza kuingizia fedha nyingi za kuwekeza katika kilimo
barani humo.
Rais Samia ametoa kauli hiyo alipohutubia Mkutano wa
Jukwaa la Mifumo ya Chakula ngazi ya Marais uliofanyika jijini Dar Es Salaam
tarehe 07 Septemba 2023.
Mhe. Rais Samia amesikitishwa na hali ya Afrika ya
kuwa Bara la walalamikaji badala ya kuweka mikakati na kutafuta mbinu za
kujiiletea mapinduzi ya kijani. Alisema watu takribani milioni 283 barani Afrika
wana lala na njaa kila siku, wengine wanapata utapia mlo na baadhi yao kufariki
kwa kukosa chakula, jambo ambalo amelitaja ni la aibu na halikubaliki kwa dunia
ya leo.
Mhe. Rais Samia amezitaka nchi za Afrika kuzigeuza
changamoto zinazoikabili dunia kuwa fursa kwao, kwa kuwekeza zaidi katika
kilimo, hususan kwa kuwawezesha vijana na kuwatatulia matatizo yao. Matatizo
hayo yanayowakabili vijana ni pamoja na ukosefu wa taarifa sahihi, ardhi,
mitaji, athari za mabadiliko ya tabianchi na kuibuka kwa magonjwa duniani.
Dkt. Samia amebainisha kuwa ili kufikia malengo ya
usalama wa chakula barani Afrika, nchi za Afrika hazina budi kutathmini
vipaumbele vyake na kutunga sera zinazoendena na mahitaji ya sasa ya dunia.
Alisema ni muhimu kwa nchi za Afrika kutekeleza ahadi
ilizojiwekea ambazo zimebainishwa katika Progaramu ya Maendeleo ya Kilimo ya
Umoja wa Afrika ya Mwaka 2003, Azimio la Malabo la mwaka 2014 kuhusu kuongeza
kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo na mikakati mingine kuhusu kilimo.
Miongozo ya maazimio hayo yanaelekeza nchi za Afrika
kuongeza bajeti ya kilimo hadi asilimia 10, kukuza sekta ya kilimo kwa asilimia
6, kuimarisha ukuaji jumuishi wa sekta ya kilimo, kuhamasisha na kushirikisha
sekta binafsi katika kilimo, kutoa fursa za ajira kwa vijana angalau kwa
asilimia 30 katika minyororo ya uongezaji thamani katika mifumo ya kilimo na
kuongeza biashara ya bidhaa na huduma za kilimo barani Afrika.
Mhe. Rais alieleza kuwa Tanzania inatekeleza maazimio
hayo kwa kuongeza bajeti ya sekta ya kilimo, kutekeleza agenda Namba 1030 ya
kuongeza ukuaji wa sekta ya kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, kuingia
katika masoko ya chakula ya kikanda na ya kimataifa ili kukidhi mahitaji ya
chakula katika nchi mbalimbali.
Aidha, alieleza kuwa ili kuchochea sekta ya kilimo
nchini, Serikali inatekeleza programu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwawezesha
vijana na wanawake kupitia mpango wa Jenga Kesho iliyo bora (BBT) ambayo
imezinduliwa na kutekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini.
Rais Samia ambaye aliungana na Rais wa Kenya, Mhe. William Ruto, Rais wa Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye na Rais wa Senegal, Mhe. Macky Sall na Rais wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi aliahidi kuwa Afrika ipo tayari kuzalisha chakula cha kutosha na kuacha kutegemea bidhaa hiyo muhimu kutoka nje.
Washiriki mbalimbali wakifuatilia Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam |
Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akifuatilia Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam |
Wanadiplomasia mbalimbali wakifuatilia Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.