Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi ametoa wito
kwa wadau kusaidia kilimo cha mwani Zanzibar, zao ambalo amelitaja kuwa
linaongoza kwa kuwa na virutubisho vingi kuliko mazao mengine yote duniani.
Mama Mariam Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Septemba 06, 2023 alipokuwa anaelezea hatua zinazochukuliwa na taasisi yake ya Maisha Bora kusaidia kilimo cha mwani kwa wananwake kisiwani Zanzibar.
Mama Mariam Mwinyi ambaye alikuwa mmoja wa jopo la watu
waliokuwa wanajadili mada kuhusu kubadilisha mifumo ya chakula kwa ajili ya kuleta
lishe bora wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula unaondelea katika
Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere tarehe 05 hadi 08 Septemba
2023.
Alisema taasisi yake ilianzishwa miaka miwili
iliyopita kwa lengo la kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambayo
moja ya malengo yake ni kuendeleza uchumi wa buluu.
“Zanzibar inaongoza barani Afrika kwa kilimo cha zao
la mwani ambalo ni chanzo cha tatu kwa kuingizia fedha za kigeni kisiwa chetu,
huku asilimia 90 ya watu wanaojihusisha na kilimo hicho ni wanawake”, Mama
Mariam Mwinyi alisema.
Aliendelea kueleza kuwa taasisi ya Maisha Bora inasaidia
takribani vikundi 16 vyenye watu 20 kila kimoja katika maeneo mbalimbali ili viweze
kufaidika kiuchumi na kilimo hicho.
Misaada hiyo ni pamoja na kuvirasimisha vikundi vyao,
kuwawezesha kupata mikopo kwa ajili ya kununulia vifaa vya kisasa, mafunzo ya
kuogelea pamoja na kuwapatia boti ili waweze kuendesha kilimo chao mbali zaidi baharini
kwa sababu ufukweni mwa bahari, hali ya hewa sio muafaka kwa kilimo cha mwani.
Miasaada mingine ni vichanja vya kukaushia mwani na mashine
za kuchakata mwani ili kwawezesha kuuza mwani iliyoongezwa thamani ambayo
inakuwa na bei nzuri sokoni.
Mama Mariam Mwinyi alihitimisha wasilisho lake kwa
kueleza kuwa mwani ni mkombozi wa maisha duni ya wanawake, lishe duni na udumavu
kwa watoto kufuatia matumzi tofauti ya zao hilo ikiwa ni pamoja na vipodozi,
mbolea na chakula chenye virutubisho vya kutosha.
Watu mbalimbali wakisikiliza mada kuhusu kubadilisha mifumo ya chakula kwa ajili ya kuleta lishe bora wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula unaondelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere tarehe 05 hadi 08 Septemba 2023. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.