Friday, September 15, 2023

TANZANIA ,CUBA ZAKUBALIANA KUSHIRIKIANA ELIMU YA JUU NA KUFUNDISHA KISWAHILI NCHINI CUBA

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato na Waziri wa Elimu ya Juu wa Cuba Mhe. Dkt. Walter Garcia wakisaini hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba kupitia elimu ya juu

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato na Waziri wa Elimu ya Juu wa Cuba Mhe. Dkt. Walter Garcia wakionesha hati ya makubaliano ya ushirikiano waliyosaini kati ya Tanzania na Cuba kupitia elimu ya juu

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam Prof. William Anangisye na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Havana Prof. Miriam Garcia wakionesha Hati ya Makubaliano waliyosaini ya ushirikiano kati ya vyuo hivyo katika hafla ya uzinduzi wa Ubalozi wa Tanzania jijini Havana nchini Cuba tarehe 14 Septemba 2023






Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Cuba zimesaini Hati za Makubaliano ya kushirikiana kupitia elimu ya juu, kubadilsihana wakufunzi na wanafunzi na kufundisha lugha ya kiswahili nchini Cuba na kutengeneza kamusi ya kiswahili na kihispaniola.

Makubaliano hayo yamesainiwa wakati wa hafla ya uzinduzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Cuba iliyofanyika jijini Havana na kushuhudiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba Mhe. Salvador Valdes Mesa.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato kwa niaba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Waziri wa Elimu ya Juu wa Cuba Mhe. Dkt. Walter Garcia.

Makubaliano mengine yaliyosainiwa ni kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salam kilichowasilishwa na Makamu Mkuu wa chuo hicho Prof. William Anangisye na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Havana Prof. Miriam Garcia

Katika makubaliano hayo Tanzania na Cuba zimekubaliana kushirikiana katika masuala ya kubadilishana ujuzi na uzoefu kupitia wahadhiri, wanafunzi, masuala ya utafiti, sayansi, teknolojia, kufundisha lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Havana na kutengeneza kamusi ya lugha ya Kiswahili na Kispaniola ili kusambaza matumizi ya kugha ya kiswahili nchini Cuba na nchi nyingine zinazozungumza lugha ya kispaniola.

Akizungumza katika hafla ya utuaji saini makubaliano hayo Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Cuba Mhe. Humphrey Polepole amesema Ubalozi wa Tanzania Havana unajivunia kusainiwa kwa makubaliano hayo ambayo yanatoa mwongozo maalum wa jinsi ya kutekeleza mpango wa kufundisha lugha ya Kiswahili nchini humo.

"Haya ni mafanikio makubwa kwetu, Ubalozi wa Tanzania Havana unajivunia kusainiwa kwa makubaliano haya, sasa yatatoa mwongozo   maalum utakaowezesha taasisi husika za elimu ya juu kutekeleza kikamilifu mpango wa kusambaza na kueneza lugha ya Kiswahili  nchini Cuba," alisema Mhe. Balozi Polepole.

Makubaliano yaliyosainiwa ni kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Cuba ambapo Chuo Kikuu cha Havana kilikubaliana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kushirikiana katika masuala ya utafiti, sayansi na Teknolojia na kufanya kazi kwa pamoja ili kutunga Kamusi ya Kiswahili na Kihispaniola.

 

Makubaliano mengine yaliyosainiwa ni kati ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknojia na Wizara ya Elimu ya Juu ya nchini Cuba ambayo yatawezesha ubadilishanaji wa wanafunzi, wahadhiri na watafiti katika eneo la sayansi na teknolojia ili kuwawezesha wahusika kubadilishana ujuzi na uzoefu katika maeneo hayo na hivyo kuleta tija na ufanisi kwa pande zote mbili.


 



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.