Thursday, September 14, 2023

BALOZI WA TANZANIA NCHINI MALAWI AZUNGUMZA NA ALIYEKUWA MWAKILISHI MKAZI WA UNDP MALAWI

Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Malawi, Bw. Shigeki Komatsubara ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi nchini humo mara baada ya mazungumzo baina yao yaliyofanyika katika Ubalozi wa Tanzania, Lilongwe hivi karibuni
===================================================================

Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola amekutana kwa mazungumzo na aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Malawi, Bw. Shigeki Komatsubara ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi nchini humo.

 

 

Lengo la mazungumzo yao ambayo yalifanyika katika Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Lilongwe hivi karibuni, lilikuwa ni kumuaga Bw. Komatsubara na kujadili ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali.

 


Katika mazungumzo yao, Balozi Kayola alimshukuru Mwakilishi huyo Mkazi kwa kufika kumuaga rasmi na kumtakia kila la kheri anapokwenda kuwa Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Tanzania. Vile vile, alimpongeza Bw. Komatsubara kwa kumaliza muda wa uwakilishi nchini Malawi kwa mafanikio na kuahidi kuendelea kushirikiana nae anapotekeleza majukumu yake nchini Tanzania.

 


Kadhalika Mhe. Balozi alimweleza Mwakilishi Mkazi kuwa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ni moja ya mashirika muhimu ya maendeleo yanayothaminiwa sana na Serikali ya Tanzania, hivyo anategemea kuendelea kufanya kazi na kushirikiana nae ili kusaidia Tanzania kufikia malengo ya maendeleo. Alimueleza kuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anaendelea kuleta mabadiliko chanya kwenye sekta zote muhimu nchini na matokeo yake yanaonekana.

 


Bw. Komatsubara aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kuweka mipango ya Taifa inayoakisi mabadiliko ya dunia na kuipongeza Serikali kwa kuimarisha mikakati ya maendeleo kwa ajili ya kuboresha maisha ya Watanzania.

 


Pia alimshukuru Balozi Kayola kwa kutenga muda kuzungumza nae na aliahidi kuendelea kushirikiana na Ubalozi hata atakapokuwa nchini Tanzania. Aidha, ameuomba Ubalozi umpe ushirikiano mrithi wake hapa Malawi, Bi. Fenella Frost. 

 


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.