Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amekutana na kuzungumza na Waziri wa Viwanda na Tekinolojia ya Juu wa Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu, Mhe. Sultan Ahmed Al Jaber Jijini Nairobi, Kenya.
Waziri Makamba amekutana na Mhe. Al Jaber pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi unaofanyika Nairobi, Kenya.
Pamoja na mambo mengine, Mhe. Waziri Makamba ameihakikishia UAE kuwa Tanzania itashiriki Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) mwezi Disemba 2023, ambapo miongoni mwa masuala itakayoyatilia mkazo ni ufadhili wa miradi ya nishati safi ya kupikia kwa akina mama vijijini.
Aidha, Mheshimiwa Waziri Makamba amesisitiza kuwa Tanzania itaungana na nchi za Afrika na nchi nyingine zinazoendelea duniani, kuhimiza Nchi Wanachama, hususan zilizoendelea kutekeleza ahadi za kupunguza hewa ukaa, kuchangia fedha kwa ajili ya Uhimilivu na kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi na upatikanaji wa teknolojia kwa ajili ya jitihada hizo.
Kwa upande wake, Mhe. Sultan Ahmed Al Jaber, aliishukuru Tanzania kwa kuahidi kushiriki Mkutano wa COP 28 na kwamba Umoja wa Falme za Kiarabu umejipanga kuhakikisha Mkutano wa COP 28 unaleta matokeo chanya katika jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi Duniani.
Aidha, Mhe. Al Jaber aliahidi kuunga mkono masuala ya kipaumbele ya Tanzania katika Mkutano huo kwa kuzingatia uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na UAE.
Mhe. Al Jaber ni Rais ajaye wa Mkutano wa Cop 28 unaotarajiwa kufanyika Dubai, mwezi Disemba 2023.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.