Serikali ya Tanzania imeazimia kutimiza lengo namba 2 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG-2) la kuondoa njaa nchini ifikapo mwaka 2030.
Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 05, 2023 na Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango
alipofungua Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula unaofanyika katika Kituo cha
Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam.
Kufikia lengo hilo, Makamu wa Rais amesema Serikali
imechukua hatua mbalimbali kwa lengo sio tu la kuondoa njaa nchini, bali pia
kuwa hazina ya chakula katika kanda na duniani kwa ujumla.
Ametaja hatua zilizochukuliwa na Serikali kuwa ni
pamoja na kukifanya kilimo kuwa uti wa mgongo na injini ya ukuaji wa uchumi jumuishi.
Akifafanua vizuri hatua hiyo, Mheshimiwa Makamu wa Rais alisema asilimia 65 ya
watu nchini wamejiajiri katika sekta ya kilimo inayokua kwa asilimia 5 kwa
mwaka na hivyo kuchangia asilimia 30 ya mapato ya mauzo ya nje, huku asilimia
65 ya malighafi zinazotumika viwandani nchini zikitoka katika sekta ya kilimo
ambayo mchango wake katika pato ghafi la nchi ni asilimia 27 na 21 kwa Tanzania
Bara na Zanzibar mutawalia.
Hatua nyingine iliyochukuliwa na Serikali ni kuongeza
bajeti ya kilimo kwa asilimia 70 kutoka Dola za Marekani milioni 120 mwaka 2021/2022
hadi kufikia milioni 397 mwaka 2023/2024. Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza
kasi ya mabadiliko ya mifumo katika sekta ya kilimo ili pamoja na mambo
mengine, sekta hiyo ikue kwa asilimia 10 kwa mwaka kutoka ukuaji wa asilimia
5.4 ya sasa.
Aidha, Mhe. Dkt. Mpango alieleza kuwa Serikali imeweka
sera zinazolenga kuinua sekta ya kilimo nchini, kuendesha kilimo
kinachozingatia athari za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza uwekezaji katika
tafiti na elimu kwa wakulima na umma kwa ujumla.
Awali, kabla ya Mhe. Makamu wa Rais hajakaribishwa
kuhutubia jukwaa hilo, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe alisema Afrika
haiwezi kufikia azma ya mabadiliko ya mifumo katika sekta ya kilimo kama
wanawake na vijana hawatashirikishwa ipasavyo na kuwasihi viongozi wa Afrika
washirikiane badala ya kushindana.
Naye, Rais wa AGRA, Dkt. Agnes Kalibata amesema
mkutano wa mwaka huu ni mkubwa na wa aina yake kuliko mikutano yote
iliyofanyika katika miaka ya nyuma. Alisema zaidi ya watu 5000 kutoka nchi 70
duniani walijitokeza kujisajili ili kushiriki Mkutano huo na kusababisha
sekretarieti kufunga zoezi la usajili kutokana na idadi ya watu kuwa kubwa
kuliko iliyotarajiwa. Awali ilikadiriwa kuwa watu 3000 ndiyo watakaojisajili kushiriki mkutano huo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Philip Isdor Mpango na Rais wa AGRA, Dkt. Agnes Kalibata wakizindua ripoti ya hali ya kilimo ya Afrika (Africa Agriculture Status Report- AASR)
Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe akifuatilia Mkutano wa Jukwa la Mifumo ya Chakula unaendelea katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere. |