Saturday, October 7, 2023

WAZIRI MAKAMBA ATUA INDIA KUELEKEA ZIARA YA KIHISTORIA YA MHE. RAIS DKT. SAMIA NCHINI HUMO










 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki   Mhe. January Makamba amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt.Subrahmanyam Jaishankar ikiwa ni maandalizi ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan atakayoifanya nchini humo kuanzia  tarehe 8 hadi 11 Oktoba 2023.



Katika mazungumzo yao yaliyofanyika hivi karibuni jijini New Delhi, viongozi hao pamoja na mambo mengine wamelezea matarajio yao ya kuimarika zaidi kwa ushirikiano kati ya Tanzania na India kupitia ziara hiyo ya kihistoria.



Kwa upande wake , Mhe. Makamba amemshukuru mwenyeji wake kwa kumkaribisha nchini humo lakini pia kwa maandalizi mazuri ya ziara ya Mhe.  Rais Dkt. Samia nchini humo.



Kadhalika, Mawaziri hao walibadilishana taarifa kuhusu ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili na kukubaliana kuongeza jitihada ili kufikia malengo ya pamoja ya kuinua kuwango cha biashara na uwekezaji kati ya nchi hizi mbili na kuhakikisha ushirikiano uliopo unazaa matokeo tarajiwa.



Mhe. Rais Dkt. Samia anatarajiwa kuwasili India tarehe 8 Oktoba 2023 kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu.



Wakati  wa ziara hiyo kutashuhudiwa ubadilishanaji wa mikataba  mbalimbali ya ushirikiano katika sekta za uwekezaji, uchukuzi,  afya, maji na nyingine nyingi.



Ziara hiyo pamoja  na mambo mengine inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na India hususan  kwenye maeneo ya kimkakati  na manufaa kwa Tanzania ikiwemo afya, maji, elimu uchumi wa buluu,  teknolojia, kilimo, na biashara na uwekezaji. 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki   Mhe. January Makamba akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt.Subrahmanyam Jaishankar ikiwa ni maandalizi ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan atakayoifanya nchini humo kuanzia  tarehe 8 hadi 11 Oktoba 2023. Mazungumzo yao yalifanyika katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje ya India jijini New Delhi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizunguza na Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe.Binaya Srikanta Pradhan jijini New Delhi kabla ya Mhe. Makamba kukutana na Waziri wa mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. Jaishankar
Mhe. Waziri Makamba akimsikiliza Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega wakati wa kikao cha kupokea taarifa kuhusu ushirikiano wa Tanzania na India mara baada ya Mhe. Makamba kuwasili nchini India tarehe 6 Oktoba 2023 kwa ajili ya kutathmini na kukamilisha maandalizi ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini humo kuanzia tarehe 8 hadi 1 Oktoba 2023
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega (kulia) akiwa na Mkrugenzi wa Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga (kushoto) wakati wa kikao na Mhe. Waziri Makamba (hayupo pichani) baada ya kuwasili nchini India. Wengine katika picha ni Mkuu wa utawala Ubalozini, Bw. Deogratius Dotto na Afisa Mwandamizi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Bi. Latifah

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. John Kambona (kulia) akiwa na Afisa Mwandamizi wa Idara hiyo Bi. Eliet Magogo na Katibu wa Mhe. Waziri Makamba, Bw. Seif Kamtunda wakati wa kikao cha ujumbe wa Tanzania na Mhe. Waziir Makamba (hayupo pichani) jijini New Delhi kuelekea ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini India tarehe 8 hadi 11 Oktoba 2023
Mhe. Makamba akizungumza na Mkurugenzi wa masuala ya ushirikiano wa India na Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya India mara baada ya kuwasili nchini humo kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya ziara ya Mhe. Rais Dkt. Samia. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega

Picha ya pamoja













 

Friday, October 6, 2023

MAKUMBUSHO YA TAIFA YA OMAN WATEMBELEA MAKUMBUSHO YA TAIFA TANZANIA

Mtendaji Mkuu wa Makumbusho ya Taifa ya Oman Mheshimiwa Jamal al-Moosawi (kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa mtalamu wa Makumbusho alipotembelea Makumbusho ya Taifa Dar es Salaam
Mtendaji Mkuu wa Makumbusho ya Taifa ya Oman Mheshimiwa Jamal al-Moosawi (kushoto) akiangalia kitabu kilichowekwa mezani na mtaalamu wa Makumbusho alipotembelea Makumbusho ya Taifa Dar es Salaam

 



Mtendaji Mkuu wa Makumbusho ya Taifa ya Oman Mheshimiwa Jamal al-Moosawi (aliyeshika koti) akizungumza kitu alipotembelea Makumbusho ya Taifa Dar es Salaam

 

Mtendaji Mkuu wa Makumbusho ya Taifa ya Oman Mheshimiwa Jamal al-Moosawi (mwenye tai) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt. Noel Luoga alipotembelea Makumbusho ya Taifa Dar es Salaam
Mtendaji Mkuu wa Makumbusho ya Taifa ya Oman Mheshimiwa Jamal al-Moosawi (kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa mtalamu wa Makumbusho alipotembelea Makumbusho ya Taifa Dar es Salaam

 

 

 

 

Ujumbe wa watu sita kutoka Makumbusho ya Taifa ya Oman umetembelea Makumbusho ya Taifa Dar es Salam kwa ajili ya kujifunza na kujionea historia ya Tanzania.

Ujumbe huo unaongozwa na Mtendaji Mkuu wa Makumbusho ya Taifa ya Oman Mheshimiwa Jamal al-Moosawi.  Pamoja na mambo mengine, ujumbe huo unatarajia pia kutembelea Kijiji cha Makumbusho  Kijitonyama, Jumba la Atiman na Jengo la Boma la zamani yaliyoko katika Mtaa wa Sokoine ambapo majengo hayo yaliyojengwa na kukaliwa na Sultan wa Zanzibar miaka ya 1860’s.

Ujumbe huo kutoka Makumbusho ya Taifa ya Oman unatarajia kutembelea visiwa vya Zanzibar ambapo watakutana na kuzungumza na uongozi wa watendaji wa Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale iliyochini ya Wizara ya Utalii na Urithi Zanzibar.

Ukiwa Zanzibar Ujumbe huo utatembelea Mji Mkongwe, Makumbusho ya amani na historia ya Mnazi Mmoja, Jumba la Kibweni na Magofu ya Mtoni. Ujumbe huo pia utatembelea Pango la Kuumbi la Jambiani, Makumbusho ya Unguja Kuu na  Mji Mkongwe kwa ajili ya kujifunza na kujionea historia iliyosheheni ya Zanzibar.

Ujumbe huo kutoka nchini Oman uliwasili nchini tarehe 05 Oktoba, 2023 ambapo pamoja na mambo mengine, una shiriki Mkutano wa Kwanza wa Pamoja wa Wataalamu kati ya Tanzania na Oman unaofanyika jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo unalenga kuendeleza uhusiano kati ya Tanzania na Oman kupitia Makumbusho ya Taifa ya Tanzania na Makumbusho ya Taifa ya Oman.

Mkutano huo wa Kwanza wa Pamoja wa Wataalamu kati ya Makumbusho ya Taifa ya Tanzania na Makumbusho ya Taifa ya Oman ni moja ya mbinu na nyenzo za kuimarisha Uhusiano kati ya Tanzania na Oman.

Kufanyika kwa Mkutano huo ni utekelezaji wa makubaliano yaliyosainiwa kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Makumbusho ya Taifa ya Oman mwezi Juni ,2022.

Ujumbe huo unatarajiwa kuondoka nchini tarehe 12 Oktoba 2023 kupitia Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar.






Thursday, October 5, 2023

RAIS SAMIA KUZURU INDIA TAREHE 8-11 OKTOBA 2023

 






Friday, September 29, 2023

TANZANIA YANADI FURSA ZA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA KILIMO KUPITIA MAONESHO YA KIMATAIFA YA KAHAWA NCHINI JAPAN

Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mhe. Baraka Luvanda amewahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Japan kuja kuwekeza nchini kwenye zao la kahawa na mazao mengine ya kimkakati.


Rai hiyo ameitoa hivi karibuni wakati akifungua semina maalum iliyoandaliwa kwa ajili ya Tanzania ikiwa ni siku ya pili ya Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa yaliyofanyika kwa siku tatu nchini Japan kuanzia tarehe 27 hadi 29 Septemba 2023.


Semina hiyo ilipata mwitikio mkubwa kwa kuhudhuriwa na wadau wa kahawa wapatao 80 wa ndani na nje ya Japan ambapo Tanzania ilitumia fursa hiyo kutangaza kahawa ya Tanzania na zoezi la uonjaji  wa sampuli za kahawa ya Tanzania kutoka kampuni 30 zilizopo nchini lilifanyika. Sampuli hizo ni za kahawa ya Arabica laini Arabica ngumu na kahawa ya Robusta.


Tanzania inasifika Japan kwa kutoa kahawa bora aina ya Arabica inayolimwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mara, Tanga, Morogoro, Njombe, Iringa, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Kigoma, Songwe na Mbeya; na kahawa ya Robusta inayolimwa mkoani Kagera.


Mbali na kuinadi Tanzania pamoja na vivutio vyake nchini Japan, kahawa ya Tanzania ni miongoni mwa vivutio hivyo ambapo imeweza kujipatia umaarufu mkubwa kutokana na ladha ya kipekee na kupewa Jina la Kibiashara la Tanzania Kilimanjaro Coffee. Jina hili hutumika nchini Japan kwa kahawa zinazozalishwa Tanzania pekee, kwa kutambua kivutio kikubwa cha Mlima Kilimanjaro uliopo nchini Tanzania.


Kadhalika, Tanzania imeshiriki Maonesho hayo ya Kimataifa ya Kahawa kama mdau  mkubwa wa kahawa duniani ambapo kwa mwaka huu yametimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2003. Maonesho ya mwaka huu, yameshirikisha makampuni na taasisi zinazohusika na kahawa zipatazo 250 kutoka nchi zinazozalisha kahawa duniani na kuhudhuriwa na wadau wa kahawa wapatao 45,000 wakiwemo, wazalishaji na wanunuzi.

Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mhe. Baraka Luvanda (mwenye scarf ya bendera ya Tanzania) akifungua semina maalum iliyoandaliwa wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa yaliyofanyika kwa siku tatu nchini Japan kuanzia tarehe 27 hadi 29 Septemba 2023. Semina hiyo pamoja na mambo mengine ililega kutangaza fursa za uwekezaji zinazopatikana kwenye sekta ya kilimo hapa nchini ikiwemo kilimo cha kahawa

Washiriki wa Semina wakifuatilia hafla ya ufunguzi
Zoezi la uonjaji wa kahawa ya Tanzania likiendelea wakati wa maonesho ya kimataifa ya Kahawa yaliyofanyika Japan kuanzia tarehe 27 hadi 29 Septemba 2023
Balozi Luvanda katika picha ya pamoja na washiriki na wadau wa kahawa kutoka Tanzania na Japan

Picha ya pamoja

 

Thursday, September 28, 2023

WAZIRI BYABATO AKOSHWA NA MRADI WA MABADILIKO YA TABIANCHI WILAYANI MAGU


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato (Mb.) ameeleza kuridhishwa kwake na utekelezaji wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabia Nchi katika Bonde la Ziwa Victoria (Adapting to Climate change in Lake Victoria Basin – ACC – LVB)kupitia Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) unaotekelezwa katika kijiji cha Ng’haya, Wilayani Magu.

Naibu Waziri Byabato ameeleza hayo alipokuwa ziarani katika Kijiji cha Ng’haya Wilayani Magu tarehe 27 Septemba 2023 ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi katika Kanda ya Ziwa ambapo anatembelea na kuona ufanisi wa miradi mbalimbali ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inayotekelezwa kupitia LVBC. 

Akipokea taarifa ya utelekezaji wa mradi huo uliogharimu kiasi cha Shilingi 656,785,965 iliyowasilishwa na Watendaji wa Wilaya ya Magu ambapo pia alipata nafasi ya kutembelea miradi hiyo ameleza namna alivyofarijika kuona mradi huo ulivyochangia ustawi wa kiuchumi kwa wananchi wa kijiji cha Ng’haya. 

“Nimefarijika sana na namna mradi huu ulivyowanufaisha wananchi kwa kuwaongezea kipato kupitia miradi iliyotajwa kwenye taarifa yenu ambayo pia muda mfupi ujao nitaenda kuitembelea. Natoa pongezi sana kwa Uongozi na safu nzima ya Watendaji wa Wilaya kwa namna mlivyosimamia utekelezaji wa mradi huu na kufikia malengo mliyojiwekea” Alieleza Naibu Waziri Mhe.Byabato

Utekelezaji wa Mradi huu wa kuhimili mabadiliko ya Tabianchi katika kijiji cha Ng’haya unalenga kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwa jamii inayoishi katika bonde la Ziwa Victoria kwa nchi za Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda. Vilevile kujenga uwezo wa jamii inayoishi katika maeneo hayo kuweza kuhimili mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia teknolojia za uvunaji wa maji ya mvua, maji chini ya ardhi, kilimo kinachohimili mabadiliko ya Tabianchi, mbinu zinazozingatia mifumo ya ikolojia katika shughuli zao za kijamii na kiuchumi.

Shughuli zingine zinazotekelezwa Wilayani Magu kupitia mradi huo kwa lengo la kuongeza kipato kwa jamii kupitia kilimo cha kisasa cha bustani na mboga mboga (kupitia vitalu nyumba) vikundi vya ufugaji wakuku, kondoo, unenepeshaji wa ng’ombe, ushonaji nguo na ufugaji wa nyuki. 

Kwa upande wake mwakilishi wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria Bw. Amos Ndoto ameeleza kuwa kwa tathmini iliyofanywa na Kamisheni hiyo imebainisha kuwa Tanzania ndio nchi iliyofanya vizuri zaidi katika utekelezaji wa mradi huo ukilinganisha na nchi wanachama wanaonufaika na mradi, hivyo kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kuendelea kunufaika na mradi katika awamu inayofuata.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Byabato alipata fursa ya kutembelea Shule ya Sekondari Ng’haya, Wilayani Magu ambayo inatekeleza Kilimo bora kinachotumia mbinu za kuhimili mabadiliko ya tabianchi (Climate Smart Agriculture) kupitia mradi huo ambao umewawezesha katika ujenzi wa kitalu nyumba kimoja kinachotumika kutoa mafunzo ya kilimo bora kwa vitendo kwa wanafunzi. 

Mradi huu ni wa Majaribio wa Kikanda wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi katika Bonde la Ziwa Victoria unatekelezwa katika Nchi 5, ambazo ni; Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda. Mradi huu ni ulikuwa ni wa miaka 3, ambapo ulianza kutekelezwa mwaka 2019 hadi 2022 kwa ufadhili wa Adaptation Fund (AF)/UNEP) chini ya uratibu wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC). Kwa upande wa Tanzania mradi huu unatekelezwa katika kijiji cha Ng’haya, Wilayani Magu.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato (Mb.) akisaini kitabu cha wageni alipowasili Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Magu
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akielekeza jambo kwa Viongozi na Watendaji wa Wilaya ya Magu (hawapo pichani) alipokuwa ziarani wilayani humo
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akitazama moja ya miundombinu ya utekelezaji wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabia Nchi katika Bonde la Ziwa unaotekelezwa katika kijiji cha Ng’haya, Magu
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akimsikiliza mratibu wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabia Nchi katika Bonde la Ziwa Bw. Ngussa Buyamba
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akiwasili kwenye moja ya mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabia Nchi katika Bonde la Ziwa katika kijiji cha Ng’haya, wilayani Magu
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akielekeza jambo alipotembelea mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabia Nchi katika Bonde la Ziwa katika kijiji cha Ng’haya, wilayani Magu
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akizungumza na Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ng’haya, wilayani Magu Bi.Glory Sulungu Daudi alipotembelea shule hiyo kwa lengo la kujionea mradi wa Kilimo bora kinachotumia mbinu za kuhimili mabadiliko ya tabianchi
 Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akizungumza na wanafunzi wa Sekondari ya Ng’haya, wilayani Magu
Picha ya pamoja
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akiwa picha ya pamoja na wanafunzi wa Sekondari ya Ng’haya, wilayani Magu.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akipanda mti kwenye Shule ya Sekondari ya Ng’haya, wilayani Magu 

Wednesday, September 27, 2023

TANZANIA YASHIRIKI KWENYE MAONESHO YA KIMATAIFA YA KAHAWA NCHINI JAPAN,

TANZANIA YASHIRIKI KWENYE MAONESHO YA KIMATAIFA YA KAHAWA NCHINI JAPAN,

Mheshimiwa Baraka Luvanda, Balozi wa Tanzania nchini Japan ameungana na mabalozi pamoja na viongozi mbalimbali wa nchi zinazozalisha kahawa duniani, kwenye hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya 20 ya Kimataifa ya Kahawa nchini Japan (2023 Japan Specialty Coffee Conference & Exhibition) iliyofanyika jijini Tokyo, Japan tarehe 27 Septemba 2023 

Uzinduzi huo umeenda sanjari na Maadhimisho ya Miaka 20 ya Maonesho hayo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2003.

Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa Japan yameandaliwa na Taasisi ya Kahawa ya Japan (Specialty Coffee Association of Japan – SCAJ) na kushirikisha makampuni na taasisi zinazohusika na kahawa zipatazo 250 kutoka nchi zinazozalisha kahawa duniani. Maonesho haya yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 29 Septemba 2023; na kuhudhuriwa na wadau wa kahawa wapatao 45,000 wakiwemo, wazalishaji, wanunuzi na wasafirishaji wa zao hilo.

Tanzania inawakilishwa na Bodi ya Kahawa Tanzania (Tanzania Coffee Board) ambayo, imeshiriki pamoja na wawakilishi wa vyama vya ushirika na makampuni ya Kitanzania yanayohusika na uzalishaji, usafirishaji, uuzaji na ufungashaji wa kahawa yakiwemo, Kagera Cooperative Union (KCU),  Kampuni ya Kaderes Peasants Development (KPD), Kampuni ya Kamal Agro, Kampuni ya TANJA, Kampuni ya Ubumwe na Kampuni ya Interbulk Packaging.

Aidha, katika maonesho hayo, Tanzania ina banda maalum la kuonesha bidhaa za kahawa zinazozalishwa Tanzania, zinajumuisha kahawa iliyochakatwa katika hatua za awali (green coffee) kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania. Pia, kupitia maonesho hayo inaoneshwa na kutangazwa kahawa iliyo tayari kwa ajili ya matumizi ikiwemo, kahawa mumunyifu (instant coffee) inayozalishwa na viwanda vikubwa vya kukaanga kahawa nchini Tanzania vya Amimza, Afri Café na Tanica.

Vilevile, siku ya pili ya maonesho hayo tarehe 28 Septemba 2023,  Tanzania itapata fursa ya kufanya semina maalum kuhusu kahawa ya Tanzania itakayoambatana na zoezi la uonjaji wa sampuli za kahawa za Tanzania (Tanzania Coffee Seminar and Cupping Session) kwa makampuni yapatayo 80 ya ukaangaji (coffee roasters) na usafirishaji kahawa ya nchini Japan. Katika tukio hilo, sampuli za kahawa za wazalishaji na makampuni ya Tanzania yapatayo 30 zitaoneshwa, kutangazwa na kuonjwa kwenye siku hiyo iliyotengwa maalum kwa ajili ya kuitangaza kahawa ya Tanzania. Sampuli hizo ni za kahawa ya Arabica laini (full washed), Arabica ngumu (naturals) na kahawa ya Robusta.

Maonesho haya, ni fursa adhimu katika kukuza soko la kahawa ya Tanzania nchini Japan ambayo ni kahawa pendwa iliyopewa jina maarufu la kibiashara la “Tanzania Kilimanjaro Coffee”.  Jina hili hutumika nchini Japan, kwa kahawa zinazozalishwa Tanzania pekee, kwa kutambua kivutio kikubwa cha Mlima Kilimanjaro uliopo nchini Tanzania.

Tanzania inasifika Japan kwa kutoa kahawa bora aina ya Arabica (Arabica laini - full washed na Arabica ngumu - natural) inayolimwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mara, Tanga, Morogoro, Njombe, Iringa, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Kigoma, Songwe na Mbeya; na kahawa ya Robusta inayolimwa mkoani Kagera.



Uzinduzi wa Maonesho ya 20 ya Kimataifa ya Kahawa nchini Japan (2023 Japan Special Coffe Conference & Exhibition)
Washiriki wakiwa katika banda la Tanzania katika Maonesho ya 20 ya Kimataifa ya Kahawa nchini Japan (2023 Japan Special Coffe Conference & Exhibition)

Washirikiwakiwa katika banda la Tanzania katika Maonesho ya 20 ya Kimataifa ya Kahawa nchini Japan (2023 Japan Special Coffee Conference & Exhibition)