Wednesday, December 6, 2023

TANZANIA , UTURUKI KUIMARISHA USHIRIKIANO SEKTA YA ELIMU

 


Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (kulia) akizungumza na Rais wa Taasisi ya Presidency For Turks Abroad and Related Communities ya Jamhuri ya Uturuki (YTB) Bw. Abdullah Eren (kushoto) walipokutana katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Rais wa Taasisi ya Presidency For Turks Abroad and Related Communities ya Jamhuri ya Uturuki (YTB) Bw. Abdullah Eren (kushoto) akizungumza na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (kulia)

Rais wa Taasisi ya Presidency For Turks Abroad and Related Communities ya Jamhuri ya Uturuki (YTB) Bw. Abdullah Eren (katikati) akizungumza na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (kulia) huku Balozi wa Uturuki nchini Mhe. Dkt. Mehmet Gulluoglu (kushoto) akifuatilia mazungumzo hayo
Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika picha ya pamoja na Rais wa Taasisi ya Presidency For Turks Abroad and Related Communities ya Jamhuri ya Uturuki (YTB) Bw. Abdullah Eren (kushoto) walipokutana katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

 

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (katikati) katika picha ya pamoja na Balozi wa Uturuki nchini Mhe. Dkt. Mehmet Gulluoglu (kulia ) Rais wa Taasisi ya Presidency For Turks Abroad and Related Communities ya Jamhuri ya Uturuki (YTB) Bw. Abdullah Eren (kushoto) katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam

 

 

 

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amekutana kwa mazungumzo na Rais wa Taasisi ya Presidency For Turks Abroad and Related Communities ya Jamhuri ya Uturuki (YTB) Bw. Abdullah Eren katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Mbarouk ameiahidi Taasisi hiyo kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Uturuki kuendelea kuimarisha uhusiano uliopo kwa manufaa ya pande zote mbili.

Amesema uhusiano kati ya Tanzania na Uturuki ni wa muda mrefu na unaoongoza hasa katika sekta za elimu, afya, biashara na uwekezaji na kuelezea matumaini yake kuwa uhusiano huo utaendelea kuimarika zaidi.

Naye Bw. Eren amesema YTB ni Taasisi ya Uturuki inayojihusisha na utoaji fedha za ufadhili katika ngazi ya elimu ya juu kwa wanafunzi wa mataifa mengine na kusaidia juhudi za mtangamano za Diaspora wa Uturuki wanaoishi nje ya nchi hiyo.

Mazungumzo ya viongozi hao yamelenga kuimarisha uhusiano zaidi katika sekta ya elimu kati ya Tanzania na Uturuki na Mkutano huo umewezesha kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala mbalimbali yenye maslahi kwa pande mbili ikiwa ni pamoja na kuona jinsi ushirikishwaji wa diaspora unavyovyoweza kuchangia maendeleo ya kisiasa, kijamii na kiutamaduni katika nchi husika.
 

Monday, December 4, 2023

BALOZI SAID AFUNGUA SEMINA YA NGAZI YA JUU KUJADILI MAENDELEO BARANI AFRIKA


 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Mussa Shaib akizungumza wakati wa kufungua Semina ya siku tatu ya Ngazi ya Juu kuhusu Afrika tunayoitaka inayojadili fursa na changamoto mbalimbali zinazolikabili bara la Afrika katika masuala ya maendeleo inayofanyika jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Mussa Shaib akizungumza wakati wa kufungua Semina ya siku tatu ya Ngazi ya Juu kuhusu Afrika tunayoitaka inayojadili fursa na changamoto mbalimbali zinazolikabili bara la Afrika katika masuala ya maendeleo inayofanyika jijini Dar es Salaam.   

Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania Mhe. Milisick Milovan (kulia) akifuatilia ufunguzi wa Semina ya siku tatu ya Ngazi ya Juu kuhusu Afrika tunayoitaka inayojadili fursa na changamoto mbalimbali zinazolikabili bara la Afrika katika masuala ya maendeleo inayofanyika jijini Dar es Salaam.

Balozi wa Comoro nchini Tanzania Mhe. Dkt. Ahamada El- Badaoui akipiga makofi kushangilia kitu wakati wa ufunguzi wa Semina ya siku tatu ya Ngazi ya Juu kuhusu Afrika tunayoitaka inayojadili fursa na changamoto mbalimbali zinazolikabili bara la Afrika katika masuala ya maendeleo inayofanyika jijini Dar es Salaam.
Balozi na Mwakilishi wa Tanzania nchini Ethiopia na katika Umoja wa Afrika Addiss Ababa, Mhe. Innocent Shio akishiriki ufunguzi wa Semina ya siku tatu ya Ngazi ya Juu kuhusu Afrika tunayoitaka inayojadili fursa na changamoto mbalimbali zinazolikabili bara la Afrika katika masuala ya maendeleo inayofanyika jijini Dar es Salaam.



Washiriki wa Tanzania katika  Semina ya siku tatu ya Ngazi ya Juu kuhusu Afrika tunayoitaka inayojadili fursa na changamoto mbalimbali zinazolikabili bara la Afrika katika masuala ya maendeleo inayofanyika jijini Dar es Salaam wakifuatilia ufunguzi wa Semina hiyo.

Washiriki wa Semina ya siku tatu ya Ngazi ya Juu kuhusu Afrika tunayoitaka inayojadili fursa na changamoto mbalimbali zinazolikabili bara la Afrika katika masuala ya maendeleo inayofanyika jijini Dar es Salaam katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa Semina hiyo.

 

 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Mussa Shaib amefungua Semina ya Ngazi ya Juu kuhusu Afrika tunayoitaka inayojadili fursa na changamoto mbalimbali zinazolikabili bara la Afrika katika masuala ya maendeleo.

Akifungua semina hiyo Balozi Said amesema Tanzania imejidhatiti kutekeleza Ajenda 2063 na Ajenda 2030 kwakuwa imeziweka katika mipango ya maendeleo ya kitaifa na kufanya ajenda hizo kutekelezwa kwa vitendo kupitia mipango ya maendeleo.


“Bara la Afrika bado linakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo umasikini, ukosefu wa maendeleo, ajira, amani na usalama, kutokuwa na sauti moja katika majukwaa ya kimataifa, nchi za Afrika lazima ziendelee kupambana ili kuhakikisha Afrika inayotakiwa inafikiwa” alisema Balozi Said Mussa
Shaib.


Amesema Tanzania imepiga hatua katika kutekeleza malengo ya Ajenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063 na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2030 na hivyo kuendelea kuimarika kwa kiwango cha ukuaji ambacho alisema kuwa kinatarajiwa kuendelea kukua kwa zaidi ya asilimia 5 kwa mwaka 2024 na kuendelea. 


Amesema Kiwango hicho cha ukuaji kimechochewa na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya miundombinu na uwekezaji inayotekelezwa na Serikali katika sekta mbalimbali. Ametaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR, Barabara, Bwawa la kuzalisha Umeme la Mwalimu Nyerere pamoja na urekebishaji wa miundombinu ya bandari na viwanja vya ndege nchini.


Amesema Tanzania imeendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika kilimo ili kuongeza uzalishaji wa chakula na kutokomeza njaa nchini na kuongeza kuwa hatua kadhaa zimechukuliwa kuimarisha upatikanaji na usawa katika Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Ufundi (TVET) na elimu ya juu. 


Amesema Tanzania pia imefanikiwa kupunguza viwango vya vifo vya mama na watoto wachanga na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano huku ikiendelea kufurahia amani na utulivu kwa kuboresha demokrasia, utawala bora, haki za binadamu na kuzingatia utawala wa sheria.


“Mbali na mafanikio niliyoyaeleza, bado nchi wanachama zinakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kutekeleza Ajenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063 na Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2030 na hivyo taarifa za tathmini katika nchi mbalimbali zinaonyesha utendaji wa jumla uko katika kiwango cha wastani” alisema Balozi Mussa.


Ametaja baadhi ya sababu zinazochangia utekelezaji wa ajenda hizo kuwa wa kiwango cha wastani kuwa ni pamoja na utawala dhaifu, mifumo mibovu ya usimamizi na uratibu kati ya wahusika wa maendeleo wa ndani na nje katika ngazi ya nchi, pamoja na rasilimali zisizotosha. 


Ameishukuru Ofisi ya Umoja wa Mataifa Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha utekelezaji wa Malengo ya Milenia yanaendelea kufanyiwa kazi na kuahidi kuwa Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Ofisi hiyo  ili  kufikia  malengo hayo kwa ukamilifu.

Semina hiyo imeandaliwa na Kamisheni ya Umoja wa Afrika kwa kushirikiana na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Barani Afrika (UNECA) inajadili utekelezaji wa Agenda 2063 na Agenda 2030 katika ngazi ya Nchi  na Mpango wa utekelezaji wa Miaka 10 wa Ajenda 2063 ambao utatoa ramani ya mabadiliko ya Bara la Afrika ndani ya muongo mmoja kama ulivyopitishwa na Mawaziri wa Umoja wa Afrika mwezi Oktoba 2023

Thursday, November 30, 2023

NIGERIA YARIDHISHWA NA UTENDAJI WA SERIKALI YA AWAMU YA SITA

Nigeria imeoneshwa kuridhishwa na utendaji wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takamawa alipokuwa akimuga Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika Ofisi Ndogo za Wizara baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi nchini.

Balozi Takamawa ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake za kuboresha Sera ya Mambo ya Nje pamoja na kuanzisha Tume ya kuboresha Haki Jinai nchini.

“Naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi Imara wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kweli imefanya mambo ambayo nadhani mataifa mengine tunapaswa kuiga hususan masuala ya kuboresha haki jinai, hili ni jambo kubwa na jema ambalo taifa lolote lile linapaswa kuiga mfano huo hapa Tanzania,” alisema Balozi Takamawa

Kuhusu Sera ya Mambo ya Nje, Balozi Takamawa amesema kuwa kuboreshwa kwa sera hiyo kunatoa mwanga wa kuimarisha utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, kuongeza wigo wa biashara za kimataifa, kuvutia uwekezaji wa mitaji na teknolojia kutoka nje katika sekta za kijamii na kiuchumi. 

Pamoja na mambo mengine, Balozi Takamawa ameishukuru Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Serikali kwa ujumla kwa ushirikiano iliompatia wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake hapa nchini.

Kwa Upande wake, Balozi Mbarouk amesema kuwa uhusiano wa Tanzania na Nigeria ni matunda yalijengwa kwa misingi imara ya viongozi wa mataifa haya mawili (Hayati Mwl. Julius Nyerere na hayati Dkt. Nnamdi Azikiwe) ambao umedumu kwa takriban miaka 60.

Kadhalika, Balozi Mbarouk alimpongeza Balozi Takamawa kwa kuimarisha misingi ya ushirikiano wa Nigeria na Tanzania wakati wa uwakilishi wake hapa nchini ambapo katika kipindi chake uhusiano uliimarika katika sekta mbalimbali hususan elimu, bishara na uwekezaji.

“Tanzania na Nigeria zimekuwa na ushirikiano mzuri kibiashara na wewe ni shahidi wa hilo, ambapo benki ya ‘United Bank of Afrika’ kutoka Nigeria imewekeza nchini, kadhalika Kiwanda cha kuzalisha Cement cha Dangote pia kimewekeza Tanzania na kutoa ajira…..huu ni Ushahidi tosha kuwa ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Nigeria ni Imara,” amesema Balozi Mbarouk.

“Naamini kuwa ukiwa nchini Nigeria utakuwa balozi mwema wa Tanzania, nakutakia kila la kheri katika utumishi wako,” amesema Balozi Mbarouk

“Katika kipindi chako umeiwakilisha vyema Australia na kuonesha mafanikio makubwa ambayo yamefikiwa kati ya Tanzania na Australia. 

Tanzania na Nigeria zimekuwa zikishirikiana katika sekta za elimu, utalii pamoja na biashara na uwekezaji.  

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akisalimiana na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takamawa alipokuwa akimuga 
katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi nchini

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akizungumza na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takamawa 
katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mazungumzo baina ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takamawa yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akimkabidhi zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takamawa baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi nchini



BALOZI SHELUKINDO AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA UJUMBE WA BENKI YA UWEKEZAJI YA ULAYA (EIB)


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amekutana kwa mazungumzo na Ujumbe wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank – EIB) ulioongozwa na Bw. Christian Elias Mkuu wa Kitengo cha Mashariki na Kusini mwa Afrika, katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma, tarehe 30 Novemba 2023.

Kupitia mazungumzo hayo ambayo ameyafanya kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb) wamejadili kuhusu ushirikiano katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa nchini Tanzania kupitia Benki hiyo.

Aidha, wamejadili yatokanayo na Mkutano wa Pamoja wa Baraza la Mawaziri la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki –OACPS na Umoja wa Ulaya – EU, uliofanyika tarehe 14 – 15 Novemba 2023 nchini Samoa, na baadae kufuatiwa na hafla ya kusaini Mkataba wa Ubia baina ya Nchi za OACPS na EU.


Vilevile, wamejadili juu ya utayari wa Tanzania kushirikiana na Umoja wa Ulaya ili kunufaika na Euro milioni 150 zilizotengwa kwa ajili ya Bara la Afrika kupitia mpango wake wa Global Gateway.

Pia, Balozi Shelukindo aliwasilisha shukrani za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Wawakilishi wa EIB kwa kuendelea kuwa mshirika wa maendeleo katika uwekezaji wa miradi ya umma, ikiwemo: Awamu ya pili ya mradi wa maji safi na usafi wa mazingira wa Ziwa Victoria mkoani Mwanza; Mradi wa huduma za usafirishaji wa mabasi yaendayo haraka; Mradi wa maji safi na usafi wa mazingira mkoani Tanga; ujenzi wa bandari mpya ya Mangapwani, Zanzibar na mradi wa umeme mkoani Kigoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Ujumbe wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya yaliyofanyika Wizarani jijini Dodoma
Mazungumzo yakiendelea 
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akimsikiliza Bw. Christian Elias Mkuu wa Kitengo cha Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank – EIB) kwenye mazungumzo yaliyofanyika Wizarani jijini Dodoma 
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na America Balozi Swaiba Mndeme wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akifafanua jambo wakati wa mazungumzo kati ya Wizara na Ujumbe wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya yaliyofanyika Wazarani jijini Dodoma

SERIKALI YAKITAKA KITUO CHA UHUSIANO WA KIMATAIFA CHA DKT. SALIM KUTOA ELIMU BORA YA DIPLOMASIA, STRATEJIA

Serikali imekitaka Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim kuhahikisha kinaendelea kutoa elimu bora ya Uhusiano wa Kimataifa, Diplomasia na Stadi za Stratejia.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) ambaye alimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) ametoa agizo hilo katika mahafali ya 26 ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim na kuwatunuku vyeti wahitimu 1,008.

Wahitimu hao wamwtunukiwa vyeti katika maeneo ya Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia, Diplomasia ya Uchumi, Usimamizi wa Amani na Migogoro na Utawala wa Kimkakati.

“Wizara inapenda kusisitiza umuhimu wa Kituo kuendelea kuelimisha Taifa kupitia mijadala na makongamano kwa lengo la kupanua uelewa wa masuala mbalimbali. Kituo kinapaswa pia kuendelea kusimamia na kutekeleza Majukumu ya Msingi ya kuanzishwa kwake ambayo yanajumuisha Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi,” alisema Balozi Mbarouk.

Balozi Mbarouk aliongeza kuwa ni vyema Kituo kikaboresha progamu zake ili kukidhi mahitaji ya Wizara, Nchi na watanzania kwa ujumla wake, ambapo alishauri kuwa Kituo kiendelee kutoa elimu ya masuala mbalimbali yanayohusiana na Uhusiano wa Kimataifa, Diplomasia ya Uchumi na Stratejia kwa taasisi za Serikali na sekta binafsi ili kusaidia kukuza ujuzi wa wananchi wetu. 

“Naelekeza usimamie utekelezaji wa mabadiliko yanayoendelea kama ilivyopendekezwa na Kamati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutathmini utendaji kazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na taasisi zilizo chini yake,” Aliongeza Balozi Mbarouk.

Kadhalika Balozi Mbarouk aliwasihi wahitimu kutambua kuwa soko la ajira serikalini na sekta binafsi kwa sasa ni ngumu, hivyo watumie ujuzi na elimu waliyoipata kujiajiri.

“Maarifa mliyoyapata ni mtaji mzuri kwenu unaowapa mwanga wa kutumia fursa za ndani na nje ya nchi katika kufanya biashara na kutoa huduma mbalimbali kwa mujibu wa kile mlichosomea,” alisema Balozi Mbarouk.

Kwa Upande wake Dkt. Reweta Wande ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim, Balozi Ramadhani M. Mwinyi, amesema Kituo kinaendelea kutoa elimu Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia ya uchumi pamoja na Stadi za Stratejia ambapo jitihada hizo zimetoa matunda ya ongezeko la wahitimu 1,008 kwa mwaka 2023 ikilinganishwa na wahitimu 990 kwa mwaka 2022.

“Lengo la kuanzishwa kwa Kituo ni kutoa elimu ya masuala ya Diplomasia kati ya Tanzania na Msumbiji. Ila kwa sasa Jukumu la Kituo ni kukuza maendeleo, ufahamu na uelewa wa masuala ya Uhusiano wa Kimataifa katika ngazi za kikanda na kimataifa kwa wataalamu wanaoendelea na wanaochipukia na umma kwa ujumla,” alisema Dkt. Wande

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Wande ameahidi kuwa Kituo kitaendelea kutoa elimu ya masuala mbalimbali yanayohusiana na Uhusiano wa Kimataifa, Diplomasia ya Uchumi na Stratejia kwa taasisi za Serikali na sekta binafsi ili kusaidia kukuza ujuzi wa wananchi kwa ujumla.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) akiwasilisha hotuba yake katika mahafali ya 26 ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim Jijini Dar es Salaam 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) akiwasilisha hotuba yake katika mahafali ya 26 ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim Jijini Dar es Salaam 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) akimkabidhi cheti mmoja kati ya wahitimu wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim wakati wa Mahafali ya 26 ya Kituo hicho Jijini Dar es Salaam 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) katika picha ya pamoja na baadhi ya wakufunzi wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim Jijini Dar es Salaam 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali katika mahafali ya 26 ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim Jijini Dar es Salaam


Sehemu ya wahitimu


TANZANIA NA VENEZUELA KUIMARISHA USHIRIKIANO


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akisalimiana na Balozi wa Venezuela nchini mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya, Mhe. Jesus Manzanilla Puppo walipokutana kwa mazungumzo katika ofisi za Wizara jijini Dodoma

Serikali ya Tanzania na Venezuela zimeahidi kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia uliopo baina ya nchi hizo ili kufungua maeneo mapya ya ushirikiano kwa manufaa ya pande zote.

Ahadi hiyo imetolewa katika mazungumzo kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na Balozi wa Venezuela nchini mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya, Mhe. Jesus Manzanilla Puppo walipokutana katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.

Mazungumzo ya viongozi hao yalijikita katika kuimarisha ushirikiano kwenye sekta za nishati hususan mafuta na gesi, kukuza teknolojia na maendeleo ya miji, elimu na utamaduni.

Pia, kupitia mazungumzo hayo Balozi Shelukindo amewakaribisha wawekezaji kutoka Venezuela kuja kuwekeza katika sekta za utalii, viwanda, madini, afya na kilimo.

Vilevile, kupitia mazungumzo hayo wamependekeza kuanzishwa kwa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Venezuela, ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano huo utakaokubaliwa kati ya pande mbili.
Mazungumzo yakiendelea
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akimsikiliza Balozi wa Venezuela nchini mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya, Mhe. Jesus Manzanilla Puppo walipokutana kwa mazungumzo jijini Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Venezuela nchini mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya, Mhe. Jesus Manzanilla Puppo yaliyofanyika jijini Dodoma

Monday, November 27, 2023

WAZIRI MAKAMBA APOKEA NAKALA ZA HATI ZA UTAMBULISHO ZA BALOZI MTEULE WA LIBYA NCHINI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amepokea nakala za hati za utambulisho za Balozi Mteule wa Libya nchini, Mhe. Abulmajed Albhloul Alshatewi katika hafla fupi iliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yao, Mhe. Makamba amemkaribisha nchini Mhe. Alshatewi na kumuahidi ushirikiano wa Wizara na Serikali kwa ujumla wakati wote atakaokuwa akitekeleza majukumu yake nchini.

Aidha, Waziri Makamba ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Libya umedumu kwa zaidi ya miaka 50 na na wakati wote umekuwa imara. “Tunaamini kuwa Mhe. Balozi wakati wa uwakilishi wako uhusiano baina ya mataifa yetu utaendelea kuimarika zaidi katika sekta mbalimbali za kimkakati,” aliongeza Waziri Makamba.

Kwa upande wake Balozi Mteule, wa Libya nchini, Mhe. Abulmajed Albhloul Alshatewi amesema kuwa atafanya kazi kwa ushirikiano na Tanzania wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake ya kibalozi hapa nchini.

Ni faraja kwangu kuja kufanya kazi Tanzania naahidi wakati wote wa uwakilishi wangu hapa Tanzania kama Balozi tutafanya kazi kwa ushirikiano katika kuendeleza sekta mbalimbali hususan biashara na uwekezaji, kilimo na nyingine.

Katika tukio jingine, Waziri Makamba amekutana kwa Mazungumzo na Balozi wa Uswisi nchini, Mhe. Didier Chassot, Balozi wa Vatican nchini, Mhe. Askofu Mkuu Angelo Accattino pamoja na Naibu Balozi wa Marekani nchini, Bw. Robert Raines.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Makamba amejadiliana na Mabalozi hao masuala mbalimbali ya ushirikiano wa uwili, kikanda na ushirikiano wa kimataifa baina ya Tanzania na nchi zao.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akipokea nakala za hati za utambulisho za Balozi Mteule wa Libya nchini, Mhe. Abulmajed Albhloul Alshatewi katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akipokea nakala za hati za utambulisho za Balozi Mteule wa Libya nchini, Mhe. Abulmajed Albhloul Alshatewi katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba katika picha ya pamoja na Balozi Mteule wa Libya nchini, Mhe. Abulmajed Albhloul Alshatewi pamoja na maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Maafisa kutoka Ubalozi wa Libya baada ya Balozi Mteule kuwasilisha nakala za hati za utambulisho 

Balozi wa Uswisi nchini, Mhe. Didier Chassot akizungumza jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akiteta jambo na Balozi wa Vatican nchini, Mhe. Askofu Mkuu Angelo Accattino katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza na Naibu Balozi wa Marekani nchini, Bw. Robert Raines katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



Sunday, November 26, 2023

WAZIRI MAKAMBA APOKEA TAARIFA MAALUM YA KUTATHMINI HALI YA UTUMISHI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akipokea taarifa Maalum ya kutathmini hali ya utumishi, majengo na uwakilishi katika Balozi zote za Tanzania kutoka kwa Kamati Maalum iliyoongozwa na Balozi Saidi Othman Yakubu katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.






Friday, November 24, 2023

SHIRIKISHO LA JAMHURI YA SOMALIA LAKUBALIWA KUJIUNGA NA JUMUIYA YA EAC



Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa kwenye Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha

Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umeridhia ombi la Shirikisho la Jamhuri ya Somalia kujiunga na Jumuiya hiyo katika Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Jumuiya hiyo uliofanyika jijini Arusha.

Mkutano uliopitisha ombi hilo umehudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. William Ruto, Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evereste Ndayishimiye, Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Sudani Kusini Mhe. Silver Kiir, Waziri Mkuu wa Rwanda aliyemwakilisha Rais Paul Kagame na Makamu Rais wa DRC aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Mhe. Antonie Tshisekedi.

Mkutano huo pia ulihudhuria na Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Somalia Mhe. Hassan Sheikh Mahmoud ambaye alialikwa kuhudhuria mkutano huo.

Mkutano huu pia ulipokea na kuridhia kwa kauli moja mapendekezo ya Majadiliano ya Juu kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi na Usalama wa Chakula yaliyofanyika jijini Arusha tarehe 23 Novemba na kuhudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Mawaziri wa Kisekta.

Kuridhiwa kwa mapendekezo hayo kunaifanya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenda katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabia Nchi (COP28) utakaofanyika nchini UAE kuanzia tarehe 28 Novemba 2023 na msimamo mmoja wa nchi wanachama.

Mkutano huo ulijadili na kukubaliana juu ya masuala mbalimbali ya Mtangamano wa Afrika Mashariki ambapo wameazimia kuendelea kuulinda na kuukuza mtangamano huo kwa lengo la kuwaenzi waasisi wake na kuinua kipato cha watu na kutoa rai za kutokuruhusu tofauti ndogondogo kuleta mtafaruku ndani ya Jumuiya

Viongozi hao wameitakia heri Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika nchini humo.

Katika Mkutano huo Wanafunzi sita kutoka nchi wanachama walishinda tuizo ya uanjdishi wa Insha na kupatiwa vyeti na zawadi ya fedha taslimu. Wanafunzi walioshinda tuzo hizo ni Lalom Joselin kutoka Sudani Kusini aliyepata Dola 550 za Marekani, Ilimfuwe Aija kutoka Burundi alipata dola 600 za Marekani, Amoron Evelyn kutoka Uganda alipata Dola 770 za Marekani, Irasore sania kutoka Rwanda alipata Dola 1000, Idirisa Musa Hamadi kutoka Tanzania alipata Dola 1200 za Marekani na Austin Alego Angoya 1kutoka Kenya alipata Dola 1500 za Marekani.

Wanafunzi hao washindi wa Tuzo hizo pia wamepata zawadi ya kutembelea Hifadhi ya Taifa Tarangire, Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro kuanzia tarehe 25 -27 Novemba 2023.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha

Rais wa Burundi Mhe. Évariste Ndayishimiye ambaye amemaliza muda wake wa Uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti Mpya wa Jumuiya hiyo Rais wa Sudan Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit wakati wa Mkutano wa kawaida wa 23 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha.
Viongozi mbalimbali wakifuatilia Mkutano wa kawaida wa 23 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea jijini Arusha.
Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Afrika Mashariki unapigwa kwenye Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akifuatilia Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliokuwa ukiendelea katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha
Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (Mb.) akifuatilia Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliokuwa ukiendelea katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akifuatilia Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliokuwa ukiendelea katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha
Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Ruto akizungumza kwenye Mkutano wa 23 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha
Rais wa Somalia Mhe. Hassan Sheikh Mohamud akizungumza kwenye Mkutano wa 23 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha. Somalia imekuwa Mwanachama mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya ombi lake la kujiunga na Jumuiya hiyo kuridhiwa kwenye mkutano.
Rais wa Burundi Mhe. Évariste Ndayishimiye akitoa hotuba ya ufunguzi kwenye Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha
Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Museveni akihutuba ya ufunguzi kwenye Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha

Idirisa Musa Hamadi kutoka Tanzania akipokea zawadi ya uandishi wa Insha