Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana Janse akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa jijini Dodoma. |
Picha ya pamoja |
Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana Janse akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa jijini Dodoma. |
Picha ya pamoja |
TAARIFA KWA UMMA
SEMINA MAALUM KUHUSU MPANGO WA BIASHARA WA NCHI YA UINGEREZA NA NCHI ZINAZOENDELEA KUFANYIKA TAREHE
28 MACHI 2024, DAR ES SALAAM.
Dodoma, tarehe 19 Machi, 2024.
Semina maalum kuhusu Mpango wa Biashara wa nchi ya Uingereza na Nchi Zinazoendelea (UK Developing Countries Trading Scheme – DCTS) inatarajiwa kufanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa jijini Dar es Salaam, tarehe 28 Machi 2024, kuanzia saa 3:00 asubuhi.
Semina hiyo ya siku moja itafunguliwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) na kufungwa na Mhe. Omar Said Shabaan, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Zanzibar.
Semina hiyo ina lengo la kufahamisha wadau wa biashara nchini juu ya fursa ya mauzo ya bidhaa za Tanzania katika soko la Uingereza kupitia Mpango wa Serikali ya Uingereza wa Kufanya Biashara na Nchi Zinazoendelea uliozinduliwa mwezi Mei mwaka 2023. Tanzania ni miongoni mwa nchi 65 ambazo Uingereza imezijumuisha katika mpango huo ili kuweza kuuza bidhaa zake bila kulipa ushuru na imeingia pia katika kundi la nchi ambazo asilimia 99 ya bidhaa zake zitanufaika na msamaha wa kodi.
Walengwa wa semina hiyo ni wadau wa biashara wenye nia ya kuuza bidhaa za aina mbalimbali katika soko la Uingereza. Wadau wanaweza pia kushiriki katika Semina hiyo kwa njia ya mtandao, kupitia link maalum ya mtandao wa “Teams” itakayotolewa kwa watakaojisajili kupitiahttps://docs.google.com/forms/d/e/1FAIpQLSdjoGDLwkXfu9PWlV7Oc3LOnn5tRyELsimZVUaMaFhCGFB1Mw/viewform
Aidha, wananchi wote wanaweza kuifuatilia Semina hiyo kupitia na chaneli ya YouTube ya Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza ijulikanayo kama Ubalozi London (http://www.youtube.com/@ubaloziLondon).
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
Serikali ya Tanzania na Italia zimeahidi kuimarisha ushirikiano katika sekta za kimkakati ambazo ni kilimo, nishati, elimu pamoja na uchumi wa buluu kwa maslahi ya pande zote mbili.
Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbaouk (Mb.) alipokutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Italia, Balozi Riccardo Guariglia wakati wa Iftari iliyoandaliwa na Ubalozi wa Italia nchini Tanzania jana jioni.
Balozi Mbarouk ameipongeza Serikali ya Italia kwa kuipa Serikali ya Tanzania kipaumbele cha kuwa moja kati ya nchi nne za Bara la Afrika zitakazonufaika na mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan). “Tanzania tunaamini kuwa kupitia mpango wa Mattei ushirikiano wa kiuchumi kati yetu na Italia utazidi kuimarika,” alisema Balozi Mbarouk.
Balozi Mbarouk aliongeza kuwa mpango wa mattei utainua sekta za kimkakati ambazo ni kilimo, nishati, elimu na uchumi wa buluu kwa upande wa Zanzibar, Sekta hizi zimepewa kipaumbele kufuatia umuhimu wake katika kukuza uchumi.
Pamoja na masuala mengine Tanzania imeihakikishia Italia ushirikiano katika kuunda kamati ya kuratibu mpango wa mattei ambayo itahakikisha sekta za kimkakati zilizoainishwa katika mpango huo zinananufaika kama ilivyopangwa kwa maslahi ya pande zote mbili.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Italia, Balozi Riccardo Guariglia alisema kuwa Italia ni rafiki wa Tanzania wa muda mrefu na mataifa hayo yamekuwa yakishirikiana katika sekta mbalimbali. Hivyo mpango wa Mattei ni moja ya njia za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi baina ya Italia na Tanzania na Afrika kwa ujumla.
“Tupo hapa kuonesha na kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika na mpango wa mattei, lakini pia kuiona Afrika ikifanikisha kuweka vipaumbele vya malengo na kutekeleza majukumu yake kupitia mpango wa mattei kwa ufanisi,” alisema Balozi Guariglia
Balozi Guariglia aliongeza kuwa lengo la mpango wa mattei ni kuendelea kuimarisha uchumi wa Bara la Afrika kwa kuzishirikisha sekta za umma na binafsi za Italia katika kufadhili mpango huo kwa maslahi ya pande zote mbili.
Mwezi Januari 2024, baada ya kumalizika kwa mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Italia, serikali ya nchi hiyo iliahidi kutuma ujumbe wa wataalam kutoka Chemba ya Biashara ya Italia kuja Tanzania kwa ajili ya kukutana na timu ya wataalam ya upande wa Tanzania kwa lengo la kukamilisha hatua za awali za utiaji saini wa ushirikiano za kutekeleza mpango wa mattei.
Aidha, katika kutekeleza hilo, mwezi Machi 15, 2024 Ujumbe wa Italia ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Italia, Mhe. Stefano Gatti ulikutana na timu ya wataalamu wa Tanzania na kuainisha sekta za kipaumbele zitakazo nufaika na mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan).
Serikali ya Tanzania na Serikali ya Italia zimekutana na kuainisha sekta za kipaumbele zitakazo nufaika na mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan).
Sekta zinazotarajiwa kunufaika na Mpango wa Mattei ni kilimo, nishati, elimu afya na uchumi wa buluu. Akizungumza wakati wa mkutano uliokutanisha ujumbe wa Tanzania na Italia jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof Kitila Mkumbo (Mb,) amesema mkutano huo umelenga kujadili utekelezaji wa mpango mpya wa kimkakati wa Mattei kati ya Tanzania na Italia.
Prof. Mkumbo amesema katika mpango huo vipaumbele vikubwa vimetolewa katika sekta za elimu, kilimo, maji na nishati na kuongeza kuwa maeneo waliyobainisha yanaendena na vipaumbele vya Serikali ya Tanzania ambavyo ni elimu, afya, nishati, miundombinu na kilimo.
“Tumekubalina kuanza kutengeneza miradi kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huu. Miradi hiyo inatekelezwa katika nchi nne za Afrika ambazo ni Tanzania, Ethiopia, Kenya na Uganda. Tumekubaliana kujikita katika maendeleo ya zao la kahawa,” amesema Prof. Mkumbo
Prof. Mkumbo ameongeza kuwa Tanzania imekuwa ikipambana kuongeza uzalishaji wa mazao hususan kahawa, kuongeza masoko hasa katika bara la Ulaya pamoja na kuongeza thamani katika mazao. “Hivyo kupitia Mpango wa Mattei Tanzania itasafirisha mazao yenye thamani nje ya nchi na kuliwezesha Taifa kupata fedha za kigeni,” amesema Waziri Mkumbo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Italia, Mhe. Stefano Gatti amesema Mpango wa Mattei umetoa kipaumbele kwa Tanzania katika sekta ya Kilimo hususan zao la kahawa ambapo nchi hizo mbili zitaendelea kushirikiana kuendeleza zao la Kahawa.
“Sisi kama Serikali tutashirikiana na sekta binafsi katika kuhakikisha zao la Kahawa kutoka Tanzania tunaliongezea thamani pamoja na kuwanufaisha wakulima wa zao hilo licha ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Mhe. Gatti
Mhe. Gatti aliongeza kuwa Mpango wa Mattei utaihusisha sekta ya uchumi wa buluu – Zanzibar pamoja na kutoa elimu katika sekta zitakazo nufaika na Mpango wa Mattei.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Italia katika kukuza na kuimarisha ushirikiano baina ya pande zote mbili.
Mpango wa Mattei umelenga kuimarisha malengo ya maendeleo endelevu yenye lengo la kuboresha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Italia.
“Kupitia Mpango wa Matei, Italia na bara la Afrika sasa wamekuja na dhana mpya ya ushirikiano kwa ajili ya maendeleo ambayo yatakuza kiuchumi kwa viwango vya juu zaidi,” alisema Balozi Mussa.
Mkutano huo pia umehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na usshirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.), Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mhe. Marco Lombardi, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme na maafisa mbalimbali waandamizi wa serikali kutoka wizara za kisekta.
Mwezi Januari 2024, Tanzania ilichaguliwa kuwa moja ya nchi za Afrika zitakazopewa kipaumbele na Italia kupitia mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan) ambapo kiasi cha Euro bilioni 5 za awali kilitengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo. Miradi hiyo ya kipaumbele kupitia Mpango mpya wa Kimkakati wa Mattei (Mattei plan) ipo katika sekta ya nishati, elimu na kilimo.
Mkutano kati ya ujumbe wa Tanzania na Italia ukiendelea jijini Dar es Salaam. Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof Kitila Mkumbo |
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof Kitila Mkumbo akitioa hotuba ya ufunguzi wakati wa mkutano uliokutanisha ujumbe wa Tanzania na Italia jijini Dar es Salaam |
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida akichangia jambo wakati wa mkutano uliokutanisha ujumbe wa Tanzania na Italia Jijini Dar es Salaam |
Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akiwasilisha mchango wake kuhusu mradi wa Mattei |
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (Mb.) ametembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya na kuzungumza na watumishi wa ubalozi wa Tanzania jijini Nairobi
Pamoja na mambo mengine, Mhe. Byabato amewataka watumishi wa ubalozi huo kuendelea kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Kenya pamoja na Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyopo jijini Nairobi.
Alipowasili nchini Kenya, Mhe. Byabato amepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini huko, Mhe. Dkt. Bernard Kibesse.
Katika hatua nyingine, Waziri Byabato amekutana na kupata chakula cha jioni na Wabunge wa Tanzania wanaoiwakilisha nchi katika Bunge la Afrika Mashariki.
Aidha, Mhe. Byabato alitumia fursa hiyo kuwaasa na kuwakumbusha Wabunge kuendelea kuiwakililisha vyema Tanzania na kusimamia maslahi na misimamo ya nchi yetu.
Waziri Byabato yupo Jijini Nairobi kushiriki Mkutano wa Tano Kikao cha Tatu cha Bunge la Afrika Mashariki linalofanyika Jijini Nairobi Kenya.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato akizungumza na watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya |
Mheshimiwa Baraka Luvanda akitoa salamu za ukaribisho katika hafla ya uzinduzi wa aina tatu mpya za kahawa ya Tanzania zilizozinduliwa na Kampuni ya ITO EN na Tully’s Coffee nchini Japan |
Mtaalam wa Kahawa (barista) wa Kampuni ya Tully’s Coffee akielezea maeneo inapolimwa kahawa ya Tanzania iliyozinduliwa nchini Japan na Kampuni ya ITO EN na Tully’s Coffee |
Bw. Osamu Aizawa, Meneja Mkuu wa Kampuni ya ITO EN, akitambulisha aina tatu mpya za kahawa ya Tanzania katika hafla ya uzinduzi wa kahawa hizo, nchini Japan |
Balozi Baraka Luvanda kwenye picha ya pamoja na Bw. Osamu Aizawa, Meneja Mkuu wa Kampuni ya ITO EN, wakitambulisha kahawa za Tanzania katika hafla ya uzinduzi wa kahawa hizo, nchini Japan |
Tanzania na Pakistan zimeahidi kuendelea kushirikiana kuimarisha zaidi sekta za biashara na uwekezaji kwa maslahi ya pande zote mbili.
Ahadi hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Salvastory Mbilinyi alipokutana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan, Bw. Shehryar Akbar Khan katika majadiliano ya Kidiplomasia kati ya Tanzania na Pakistan kwa lengo la kuimarisha, kukuza na kudumisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za kipaumbele.
Bw. Mbilinyi amesema Pakistan ni miongoni mwa nchi za Asia ambazo zina majadiliano ya kidiplomasia na Tanzania. Amesema chimbuko la majadaliano hayo ni kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Pakistan.
Akizungumza katika mkutano uliokutanisha pande hizo mbili katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam, Bw. Mbilinyi amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imejikita zaidi katika kuboresha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji nchini hivyo wafanyabiashara kutoka Pakistan wasisite kuwekeza Tanzania kwani ni salama.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan, Bw. Shehryar Akbar Khan amesema Pakistan na Tanzania zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu na zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali wakati wote.
“Nchi zetu zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali, ila kwa sasa tunaona ni vyema zaidi tukaimarisha zaidi sekta ya biashara na uwekezaji kwani kila nchi inahitaji biashara na uwekezaji,” alisema Bw. Khan na kuongeza kuwa Pakistan imekusudia kushirikiana na Tanzania katika sekta ya uchumi wa buluu.
Katika mazungumzo hayo pande zote mbili zimeahidi kuimarisha ushirikiano katia sekta za elimu, afya, ulinzi, kilimo, nishati uchumi wa buluu na usafirishaji.
Majadiliano ya Kidiplomasia kati ya Tanzania na Pakistan yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. |
Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamewasilisha salamu za rambirambi kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha Rais wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Ali Hassan Mwinyi katika Baraza la Mawaziri la Jumuiya hiyo lililoanza leo tarehe 10 Machi 2024 jijini Luanda, Angola
Wakati wa ufunguzi wa Baraza hilo, Waziri wa Mambo Nje wa Angola na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC, Mhe. Balozi Tete António pamoja na Mawaziri wengine wa nchi za SADC walitoa salamu hizo na kusifu uongozi mahiri na mchango wa Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi katika kuchangia maendeleo ya Tanzania na Kanda ya SADC hususan pindi alipokuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Jukwaa la Uratibu wa masuala ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADCC) mwaka 1989 - 1990 na pia aliongoza mchakato wa kubadili Jukwaa hilo kuwa SADC.
Kwa muda wa siku mbili Baraza hili litajikita kupitia, kujadili na kuridhia Bajeti ya SADC kwa mwaka wa fedha wa 2024/25. Vile vile, Baraza litajadili hatua iliyofikiwa katika kugharamia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Maendeleo wa SADC wa 2020–2030, Taarifa ya Kamati ya Rasilimali Watu na Utawala na hatua iliyofikiwa katika kutafsiri nyaraka muhimu za SADC kwa lugha ya Kiswahili.
Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Baraza la Mawaziri la SADC umeongozwa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) ambaye ameambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (Mb.) na viongozi wengine waandamizi wa Serikali.
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, Bw. Elias Magosi akihutubia wakati wa ufunguzi wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) linaloendelea jijini Luanda, Angola tarehe 10 – 11 Machi, 2024 |
Meza kuu ikiongoza Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) linaloendele jijini Luanda, Angola tarehe 10 – 11 Machi, 2024 |
Picha ya pamoja ya wakati wa hafla ya ufunguzi wa Baraza la Mawaziri wa SADC |