Serikali ya Tanzania imeipongeza Serikali ya Ethiopia kwa kuweka historia katika Mji wa Serikali Dodoma ya kuwa nchi ya kwanza kujenga majengo ya Ofisi na Makazi ya Balozi na kuzitolea wito nchi nyingine kuiga mfano huo.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethipia, Mhe, Birtukan Ayano ambapo kwa pamoja waliweka Jiwe la Msingi la ujenzi huo kwa niaba ya Serikali zao katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma leo Mei 17, 2024.
Balozi Mbarouk alieleza kuwa uwekaji wa jiwe la msingi huo ni kielelezo tosha cha kuimarika kwa ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Ethiopia ambao ulianza tangu enzi za waasisi wa mataifa haya, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Haile Selassie.
Balozi Mbarouk alisisitiza umuhimu wa kukuza biashara baina ya nchi hizi mbili kwa kuwa kiwango cha biashara kinachofanyika hivi sasa hakiakisi uhusio mzuri uliopo baina ya mataifa hayo mawili.
Kwa upande wake, Mhe. Ayano alisema uwekaji wa jiwe la msingi huo ni ishara ya ushirikiano mzuri uliopo baina ya nchi hizi mbili na dhamira ya dhati ya Serikali ya Ethiopia ya kuuimarisha zaidi, hususan katika nyanja ya biashara na uwekezaji.
Hafla ya uwekaji jiwe la msingi ilihudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule ambapo aliwahakikishia jumuiya ya wanadiplomasia nchini kuwa Dodoma ipo tayari kuwapokea na miundombinu ya kijamii ikwemo maji, elimu, afya na usafirishaji, Serikali inaendelea kuijenga na kuiboresha iliyopo.
Viongozi
wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe.
Ummy Nderiananga; Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya
Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vicent Mbogo, Naibu Katibu wa Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Mussa, Meya wa Halimashauri
ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe na viongozi waandamizi wa Serikali
Naibu Waziri Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor
Mbarouk akiwa na Naibu Waziri Mambo ya Nje Ethiopia Mhe. Balozi Birtukan
Anayo wakifungua kitambaa kuonesha jiwe la Msingi la ujenzi wa Ubalozi wa Ethiopia katika
mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma baada ya kuweka jiwe hilo huku
wakishuhudiwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Mhe. Ummy
Nderiananga, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, Balozi wa
Ethiopia nchini Mhe. Shibru Mamo Kedida, Makamu Mwenyekiti Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje , Ulinzi na Usalama na viongozi wengine
wa Chama na Serikali. |
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la Msingi la ujenzi wa Ubalozi wa Ethiopia katika mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma. |
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Mhe. Ummy Nderiananga akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la Msingi la ujenzi wa Ubalozi wa Ethiopia katika mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma. |
Balozi wa Ethiopia nchini Tanzania Mhe. Shibru Memo Kadida akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la Msingi la ujenzi wa Ubalozi wa Ethiopia katika mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma |
Wajumbe wa Meza kuu wakifuatilia hafla ya uwekaji jiwe la Msingi la ujenzi wa Ubalozi wa Ethiopia katika mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma. |