Tuesday, May 14, 2024

RAIS SAMIA "BAJETI KUU YA SERIKALI KUWEZESHA NISHATI SAFI YA KUPIKIA NA WANAWAKE"

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefungua Mkutano wa Nishati Safi ya Kupikia Barani Afrika unaofanyika katika Makao Makuu ya UNESCO jijini Paris, Ufaransa tarehe 14 Mei, 2024.

Katika hotuba yake ya ufunguzi Mheshimiwa Rais Samia amesisitiza umuhimu wa nishati safi kwa Nchi za Afrika ili kudhibiti madhara yatokanayo na kadhia za kukosa nishati hiyo kama vile, uharibifu wa mazingira unaosababishwa na ukataji wa miti na uchomaji wa mkaa, unyanyasaji wa kijinsia na vifo kwa wanawake na watoto.

Aidha, amesema Tanzania imelipa kipaumbele suala la nishati safi ya kupikia ambapo imeongeza bajeti ya Serikali ili kuwezesha upatikanaji wa nishati safi kwa urahisi, gharama nafuu pamoja na uwekezaji katika teknolojia. Vilevile  itasimamia utekelezaji wa sera, mikakati na miongozo ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa ustawi wa jamii.

"Serikali imelipa umuhimu suala la nishati safi ya kupikia ambapo katika kuyafikia malengo hayo bajeti kuu ya Serikali imeweka kipaumbele katika kuwezesha upatikanaji wa nishati hiyo sambamba na kuwainua wanawake." Rais Samia

Rais Samia ameongoza mkutano huo akiwa pamoja na wenyeviti wenza: Waziri Mkuu wa Norway, Mhe. Jonas Gahr Støre; Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Nishati, Dkt. Fatih Birol; na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina.

Pamoja na masuala mengine, mkutano huo una lengo la kufanya matumizi ya nishati safi ya kupikia kuwa suala la kipaumbele katika agenda ya kimataifa; kuainisha hatua madhubuti za kisera zitakazoharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia; na kutoa fursa kwa washiriki kutoa ahadi za kifedha, sera, na ubia ili kufikia azma ya kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Kupitia mkutano huo, jumla ya ahadi za kiasi cha USD 2.2 bilioni zimekusanywa  ili kusaidia katika usimamizi wa sera na miongozo mbalimbali na uwekaji wa miundombinu itakayowezesha upatikanaji wa nishati safi.

Ikumbukwe  kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshapiga hatua katika jitihadi za kitaifa za kuhakikisha nishati safi ya kupikia inapatikana nchini kupitia Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia ulizozinduliwa tarehe 8 Mei, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akitambulika kama Kimara wa Nishati Safi ya Kupikia Ulimwenguni.

Matarajio ya kitaifa ni kuwa ifikapo mwaka 2034, Tanzania itakuwa imepiga hatua katika kukuza kiwango cha matumizi ya nishati safi ya kupikia, hali itakayowezesha utunzaji wa mazingira, kuboresha afya na ustawi wa jamii, kukuza uchumi na kusaidia kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya Mwaka 2030.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan,akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia barani Afrika unaofanyika katika Makao Makuu ya UNESCI jijini Paris, Ufaransa tarehe 14 Mei, 2024.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akifuatilia majadiliano katika  Mkutano wa Nishati Safi ya Kupikia barani Afrika uliofanyika Makao Makuu ya UNESCO jijini Paris, Ufaransa tarehe 14 Mei, 2024.

Mkutano ukiendelea

Ujumbe kutoka sekta binafsi ukifatilia mkutano huo.

Picha ya pamoja ya meza kuu baada ya ufunguzi wa mkutano huo.




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.