Friday, May 31, 2024

TANZANIA KUJIIMARISHA KATIKA UKANDA WA IORA


Tanzania imeweka nia ya dhati ya kunufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana katika Jumuiya ya Nchi za Mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) kupitia uanachama wake kwenye Jumuiya hiyo. 


Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa ambaye aliongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 26 wa Kamati ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya hiyo uliofanyika kwa njia ya mtandao kutokea jijini Dodoma na kuhitimishwa leo tarehe Mei 31, 2024.


Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao huku ujumbe wa Tanzania ukishiriki kutokea jijini Dodoma, Balozi Mussa amesema zipo fursa nyingi katika Jumuiya hiyo ambazo Tanzania ikijipanga itanufaika nazo ikiwemo utunzaji wa mazingira na rasilimali za bahari, ulinzi na usalama baharini, namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, uvuvi na utalii na kwamba wakati umefika sasa wa kuhakikisha wananchi wa Tanzania wananufaika kupitia jumuiya hiyo.


Aidha, kupitia mkutano huo Balozi Mussa amewasisitiza wajumbe wa mkutano waliotoka katika Taasisi, Wizara na Idara za Serikali kuendelea kuhakikisha maazimio mbalimbali yanayofikiwa kupitia Jumuiya hiyo yanatekelezwa kikamilifu ili kulinufaisha taifa kiuchumi na kijamii kwa ujumla.


“Ninawahimiza tuendelee kushirikiana ili taarifa za utekelezaji wa maazimio ya mkutano huu yaweze kufanyiwa kazi kwa haraka na kuiwezesha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuendelea kuratibu shughuli za kikanda na kimataifa kwa tija na maslahi mapana ya Nchi’’ alisema Balozi Mussa.


Kadhalika wakati wa Mkutano huo, Tanzania iliwasilisha pendekezo la Mradi kuhusu Ushirikishwaji wa Jamii za Pwani katika Utunzaji wa Rasilimali za Bahari za ukanda wa Pwani ambalo linalenga pamoja na mambo mengine kuzijengea uwezo jamii za Pwani kutunza rasilimali za bahari na kuibua fursa za kiuchumi zitakazowanufaisha na kuinua kipato cha wananchi wa ukanda wa Pwani.


Akiwasilisha pendekezo hilo, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dkt. Saida Fundi amesema Chuo hicho kilikuja na wazo la kuandaa mradi huo baada ya kuona upo umuhimu mkubwa wa kuziwezesha jamii zilizopo kwenye mwambao wa Pwani ya Bahari ya Hindi kunufaika na rasilimali zitokanazo na bahari.


Amesema pendekezo la mradi huo ambalo litahusisha Warsha itakayofanyika hapa nchini mwezi Oktoba 2024 na kuzihusisha nchi wanachama na wadau mbalimbali lina malengo mahsusi ikiwemo kuimarisha mtandao wa watumiaji wa rasilimali za bahari katika ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi na kuzijengea uwezo jamii za ukanda wa Pwani ili kunufaika na fursa mbalimbali.


========================

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akichangia katika Mkutano  wa 26 wa Kamati ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Nchi za Mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) uliofanyika kwa njia ya mtandao kutokea jijini Dodoma na kuhimishwa leo tarehe 31 Mei, 2024.

Balozi Mussa akijadili jambo na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, Bi. Talha Waziri wakati wa mkutano wa 26 wa Kamati ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Nchi za Mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) uliofanyika kwa njia ya mtandao kutokea jijini Dodoma na kuhitimishwa leo 31 Mei, 2024

Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia mkutano.

Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania.



Mkutano ukiendelea.



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.