Friday, May 17, 2024

TANZANIA, CHINA ZAINGIA ZAMA MPYA KIDIPLOMASIA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb.) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. WANG Yi walipokutana Ofini kwakwe jijini Beijing kwa mazungumzo. Terehe 17 Mei 2024

  • Nia ni kujenga dunia yenye usawa 
  • China yafuta machozi waathirika wa mafuriko
  • Yamwalika Rais Samia Septemba
  • Hadhi ya Chuo cha Dk. Salim kupanda
BAADA ya miaka 60 ya uhusiano wa kihistoria, Tanzania na China leo zimetangaza kuingia katika zama mpya za uhusiano wa kidiplomasia ambao lengo lake ni kujenga dunia iliyo bora zaidi, yenye maendeleo zaidi na usalama zaidi.

Katika mkutano wa pamoja uliofanyika jijini Beijing, China, leo Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, alimweleza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, kwamba katika miaka 60 iliyopita tangu kuanza kwa uhusiano nchi hizi mbili, Tanzania imejipambanua kama rafiki wa kwenye shida na raha.

“Tanzania mara zote amekuwa rafiki za China. Kwa China, miaka 60 ina maana kubwa sana kwenye uhusiano. Hatua inayofuata sasa baada ya hapa ni kuendeleza uhusiano huu katika zama mpya za kujenga dunia yenye maendeleo, ya haki na iliyo na usalama kwa watu wote” alisema Wang.

Waziri Makamba yuko nchini China kwa ziara ya kikazi kufuatia mwaliko wa mwenzake huyo na alitumia nafasi hiyo pia kueleza namna Tanzania inavyothamini mchango wa taifa hilo la bara la Asia katika maendeleo yake na kwamba wakati umefika sasa wa kuingia katika zama mpya kuendana na changamoto za dunia ya sasa.

“China ni rafiki zetu kwenye nyakati zote. Ni rafiki ambaye anatabirika na habadilikibadiliki wakati wote. Baada ya miaka hii 60 ya uhusiano uliotukuka, sasa tuingie katika zama mpya za uhusiano ambao utazingatia changamoto zilizopo kwenye kujenga dunia bora zaidi kuliko ile iliyokuwepo wakati wa waasisi wa uhusiano huu” alisema.

Katika kuonyesha uhusiano wa karibu baina ya wananchi wa mataifa hayo, Waziri Wang alisema China inatoa mchango wa dola 500,000 za Marekani, sawa na shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya kusaidia waathirika wa mafuriko ya mvua yaliyoikumba Tanzania mwaka huu.

Maeneo kadhaa ya Tanzania yameathiriwa na mvua kubwa za masika zilizochanganyika na zile za El Nino na Waziri huyo wa China alisema Wachina wamesikia kuhusu athari hizo na wametoa mchango huo ili kusaidia waathirika kuanza upya maisha yao. Waziri Makamba alishukuru kwa mchango huo akisema ni ushahidi mwingine wa urafiki wa kipekee baina ya nchi hizo mbili.

Katika hatua nyingine, Serikali ya China leo imetoa mwaliko rasmi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhudhuria mkutano wa masuala ya usalama baina ya China na Afrika (FOCAC) uliopangwa kufanyika Septemba mwaka huu.

Mkutano wa FOCAC hufanyika kila baada ya miaka mitatu na katika miaka ya karibuni umekuwa ni miongoni mwa mikutano muhimu kwenye uhusiano wa kimkakati baina ya nchi za Afrika na China.

Kadhalika, China imekubali ombi la Tanzania la kufanya maboresho ya Chuo cha Diplomasia cha Dkt. Salim Ahmed Salim ikiwemo kuongeza majengo, kuongeza mitaala na kukifanya kuwa cha kutengeneza ajenda kwa ajili ya masuala ya kimkakati ya kubadili mfumo wa uendeshaji wa dunia.

Dk. Salim ni mmoja wa wana diplomasia wa Tanzania wenye heshima kubwa nchini China na uamuzi wa kuongeza hadhi ya chuo hicho umezingatia hadhi yake kidiplomasia na umuhimu wake kwa nchi hizi mbili.

Katika ziara yake hiyo inayoendelea nchini China, Makamba ambaye ameambatana na Mhe. Zahor Haji Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), alitembelea na kufanya mazungumzo na taasisi na viongozi wa mashirika yanayohusika na misaada kwa Tanzania ikiwemo benki ya EXIM ambayo imeahidi kuendelea kukopesha kwenye miradi ya kimkakati.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akisalimiana na Rais wa Benki ya Exim ya China Bw. Ren Shengjun walipokuna kwa mazungumzo jijini Beijing, China
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akisalimiana na Mwenyekiti wa Shirika la Ushikiano wa Maendeleo ya Kimataifa (CIDCA) Bw. Luo Zhaohui walipokutana kwa mazungumzo Ofini kwakwe jijini Beijing, China.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. WANG Yi na ujumbe wao wakiwa katika mazungumzo yaliyofanyika jijini Beijini, China. 
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. WANG Yi akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba yaliyofanyika jijini Beijing, China.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba na Mwenyekiti wa Shirika la Ushikiano wa Maendeleo ya Kimataifa (CIDCA) Bw. Luo Zhaohui na ujumbe wao wakiwa katika mazungumzo yaliyofanyika jijini Beijing, China.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Rais wa Benki ya Exim ya China Bw. Ren Shengjun yaliyofanyika jijini Beijing, China
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. WANG Yi yaliyofanyika jijini Beijing, China
azungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba na Rais wa Benki ya Exim ya China Bw. Ren Shengjun yakiendela jijini Beijing, China
Picha ya pamoja

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.