Thursday, June 13, 2024

WAATALAM WA SEKTA YA AFYA KUTOKA NCHI ZA EAC WAKUTANA JIJINI ARUSHA

Wataalam wa sekta ya afya kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana jijini Arusha katika kikao cha maandalizi ya Mkutano wa Saba (7) wa Dharura wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Afya utakaofanyika kesho tarehe 14 Juni, 2024 na kutanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu.

 

Mkutano huu wa wataalamu pamoja na masuala mengine utapitia na kujadili  pendekezo la Tanzania la kuanzisha vituo  viwili vya umahiri ambavyo ni: Kituo cha Umahiri cha Sayansi ya Afya ya Kinywa chini ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Uloto na Sayansi ya Matibabu ya Magonjwa ya Damu chini ya Hospitali ya Benjamin Mkapa.

 

Akifungua mkutano huo Mkurugenzi wa Sekta ya Jamii kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Irene Isaka ameeleza kuwa kupitia mkutano huu wajumbe watachangia na kushauri juu ya umuhimu wa vituo hivyo viwili vya umahiri ambavyo vinachangia utoaji wa huduma za kibingwa za afya pamoja na mafunzo katika kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

Naye Mwenyekiti wa mkutano wa Wataalam kutoka Jamhuri ya Sudan Kusini, Mhandisi Ring Dut katika hotuba yake ya ufunguzi ameeleza kuwa kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 kumeleta somo katika ukanda wa Afrika Mashariki hususan katika suala la kujijengea uwezo wa kujitegemea katika masuala ya huduma za afya, uanzishaji wa programu saidizi na uimarishwaji wa miundombinu katika sekta hiyo.

 

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano Ngazi ya Wataalam umeongozwa na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi Abdillah Mataka ambaye ameambatana na Wataalamu Waandamizi kutoka sekta ya Afya na Elimu.

 

Katika hotuba yake ya ufunguzi Mhandisi amesisitiza umuhimu wa mkutano huo, akibainisha kuwa andiko dhana ya kuanzisha vituo vya umahiri vilivyopendekezwa na Tanzania vitaleta mabadiliko muhimu katika mifumo ya afya, huduma za kibingwa, mafunzo, na kujengea uwezo.

 

Pia, amewahimiza wajumbe kujadili na kushiriki katika mijadala ya wazi na yenye kujenga ili kuboresha afya kwa ustawi wa watu wa EAC, huku akitoa shukrani kwa wadau wote walioshiriki katika kuandaa maandiko haya ya dhana.

============================================

Mwenyekiti wa Mkutano wa Wataalam kutoka Jamhuri ya Sudan Kusini, Mhandisi Ring Rut (wa pili kushoto) akifungua Mkutano Ngazi ya Wataalamu kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano wa Saba (7) wa Dharura wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Afya utakaofanyika tarehe 14 Juni, 2024 jijini Arusha. Kulia kwake ni: Mkurugenzi wa Sekta ya Jamii kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Irene Isaka, Mkuu wa Idara ya Afya kutoka kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Eric Nzeyimana na kushoto ni Mnukuu (Rapportuer) kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Dkt. Dieumerci Kaseso.
Mkurugenzi wa Sekta ya Jamii kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Irene Isaka (kati) akitoa hotuba ya ufunguzi katika Mkutano Ngazi ya Wataalam unaofanyika tarehe 13 Juni, 2024 jijini Arusha.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi Abdillah Mataka akitoa neno la ufunguzi katika Mkutano Ngazi wa Wataalam unaofanyika jijini Arusha tarehe 13 Juni, 2024.
Ujumbe kutoka Tanzania

Ujumbe kutoka Uganda

Ujumbe kutoka Tanzania

Sehemu nyingine ya Ujumbe kutoka Tanzania


Picha ya pamoja

 

Monday, June 10, 2024

BALOZI MUSSA AWAASA VIJANA KUWA MABALOZI WAZURI NJE YA NCHI


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa amewaasa vijana waliochaguliwa kushiriki katika programu ya mafunzo ya uongozi kwa vijana maarufu kwa jina la “Mandela Washington Fellowship for Young African Leaders” kuwa mabalozi wazuri katika mafunzo hayo yanayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 18 Juni, 2024 jijini Washington, Marekani.

Nasaha hizo zimetolewa katika hafla fupi ya kuwaaga vijana hao 26 ambayo ilihusisha makabidhiano ya bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni ishara ya kuitangaza na kuiwakilisha nchi katika heshima inayostahili iliyofanyika katika Ofisi za Wizara Mtumba, Dodoma tarehe 10 Juni, 2024.

Balozi Mussa aliwapongeza vijana hao kwa kuonesha uwezo na jitihada binafsi kuchukua nafasi ya kuomba na kufanikiwa kupita katika mchujo wa vijana wengi walioihitaji fursa hiyo. Hivyo, ni wema wakazingatia mafunzo na kuhakikisha ujuzi na elimu watakayoipata inaleta manufaa kwao na kuwajengea uwezo vijana wengine waliopo nchini.

"Hii ni programu maalum ambayo itawajengea uwezo katika masuala ya uongozi hususani, uongozi katika masuala ya usimamizi wa umma, uongozi katika usimamizi wa biashara na uongozi katika masuala ya ushirikishwaji wa jamii yakiwa ni maeneo mtambuka katika ukuaji wa nchi za Afrika.” alisema Balozi Mussa.

Pia akawaeleza umuhimu wa kuzingatia sheria na taratibu za nchi husika pamoja na kujikita katika malengo yanayowapeleka nchini Marekani ili kufanikisha kutumia fursa hiyo kujenga uwezo katika maoneo yao husika ya kiutendaji sambamba na kuijengea nchi sifa nzuri.

Aidha, amewasisitiza kuzingatia tamaduni na mila za kitanzania wawapo nchini humo kwakuwa mafunzo hayo yanahusisha mataifa tofauti hivyo ni vema kuepuka changamoto mbalimbalii za kimaadili zinazoweza kuwaharibia sifa binafsi na taifa kwa ujumla. Vilevile, katika hilo akasisitiza umuhimu wa kuwasilisha taarifa zao katika ofisi za ubalozi zilizopo jijini Washington.

Nao vijana wanaoenda kushiriki mafunzo hayo wameishukuru Serikali kwa kuendeleza kuimarisha ushirikiano mzuri na Serikali ya Marekani na hivyo kuwawezesha kushiriki kwa wingi katika mafunzo hayo ambayo pamoja na masuala mengine yatawajengea na kukuza uwezo katika teknolojia inayopatikana katika taifa hilo kubwa lililopiga hatua kimaendeleo sambamba na kukutana na wadau katika sekta husika.

Programu hii inatarajiwa kutimiza miaka 10 tangu ianzishwe mwaka 2014 ambapo imekuwa ikitoa mafunzo kwa washiriki kwa njia ya vitendo na kuingia darasani na hivyo, kuwawezesha kushiriki katika majukumu ya kijamii pamoja na kufanya ziara katika ofisi mbalimbali za umma na mashirika nchini Marekani.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akisisitiza jambo alipokuwa akiwaaga washiriki wa programu ya mafunzo ya uongozi kwa vijana(Mandela Washington Fellowship for Young African Leaders is the flagship program)yatakayofanyika nchini Marekani.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akiwa katika mazungumzo na vijana waliochanguliwa kushiriki katika programu ya mafunzo ya uongozi kwa vijana (Mandela Washington Fellowship for Young African Leaders is the flagship program) kwenye hafla fupi ya kuwaaga vijana hao iliyofanyika Mtumba, jijini Dodoma.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akiwa katika mazungumzo na vijana waliochanguliwa kushiriki katika programu ya mafunzo ya uongozi kwa vijana (Mandela Washington Fellowship for Young African Leaders is the flagship program) kwenye hafla fupi ya kuwaaga vijana hao iliyofanyika Mtumba, jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akikabidhi Bendera ya Taifa kwa vijana waliochanguliwa kushiriki katika programu ya mafunzo ya uongozi kwa vijana (Mandela Washington Fellowship for Young African Leaders is the flagship program) kwenye hafla fupi ya kuwaaga vijana hao iliyofanyika Mtumba, jijini Dodoma.
Picha ya pamoja. 

KATIBU MKUU MAMBO YA NJE AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KIKAO CHA SADC MASUALA YA SIASA NA DIPLOMASIA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Kikao cha Pamoja cha Kamati Ndogo ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuhusu masuala ya Siasa na Diplomasia kilichofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 10 Juni 2024.


Akifungua kikao hicho ambacho kimefanyika kwa ngazi ya Makatibu Wakuu , Mwenyekiti ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Zambia,  Bi. Etambuyu Gundersen aliwataka wajumbe kujadili na kutoa mapendekezo katika agenda mbalimbali zilizowasilishwa kwao ili hatimaye mapendekezo hayo yawasilishwe kwenye kikao cha Mawaziri kitakachofanyika mwezi Julai 2024 kwa ajili ya kuridhiwa.

 

Akichangia hoja kwenye kikao hicho, Balozi Shelukindo amezishukuru na kuzipongeza Nchi Wanachama wa SADC kwa kufanikisha uundwaji na uzinduzi wa Sanamu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere uliofanyika mwezi Februari 2024 katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia.

 

Amesema  uzinduzi huo ambao ulihudhuriwa na idadi kubwa  ya wakuu wa nchi  wa Afrika  ulidhihirisha namna ambavyo  wanaenzi mchango mkubwa uliotolewa na Hayati Mwalimu Nyerere kwenye Ukombozi wa  Nchi za Kusini mwa Afrika.

 

Kadhalika amesema  Tanzania inaendelea na mawasilianao ya ndani ili kukamilisha Mpango  wa Taifa  wa Utekelezaji wa Azimio la Umoja wa Mataifa Namba 1325 kuhusu kuwawezesha Wanawake kushiriki  katika juhudi  za  kutatua, kuzuia na kudhibiti migogoro duniani huku akizipongeza nchi zilizokamilisha Mpango huo ikiwemo Zimbawe na Madagascar.

 

Vilevile, ametumia fursa hiyo kuzipongeza Jamhuri ya Afrika Kusini na Jamhuri ya Madagascar kwa kufanikisha uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge uliofanyika kwenye nchi hizo kwa amani na utulivu  tarehe 29 Mei 2024 mtawalia.

 

Amesema, kikanda uchaguzi katika nchi hizi mbili umeakisi viwango vya kimataifa vya demokrasia pamoja na kanuni na miongozo ya SADC kuhusu uchaguzi unaofuata misingi ya demokrasia.

 

Kikao hicho ambacho kimefanyika kwa ajili ya kuandaa mkutano wa Mawaziri unaotarajiwa kufanyika mwezi Julai 2024,  kimehudhuriwa na Nchi za Tanzania, Lesotho, Eswatini, Botswana, Angola, Namibia, Afrika Kusini, Shelisheli ,  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia na Zimbabwe.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza wakati wa Kikao cha Pamoja cha Kamati Ndogo ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuhusu masuala ya Siasa na Diplomasia kilichofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 10 Juni 2024
Katibu Mkuu, Balozi Shelukindo akichangia hoja wakati wa Kikao cha Pamoja cha Kamati Ndogo ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuhusu masuala ya Siasa na Diplomasia kilichofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 10 Juni 2024. Kulia ni Afisa Mambo ya Nje anayeshughulikia Dawati la SADC, Bi. Shazma Msuya akinukuu taarifa ya kikao hicho. 

 
Kikao kikiendelea

Friday, June 7, 2024

WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA CANADA AKUTANA NA MABALOZI WA AFRIKA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada, Mhe. Melanie Joly akisalimiana na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Canada, Bw. Charles Faini wakati wa Mkutano kati yake na Mabalozi wa Afrika  uliofanyika hivi karibuni jijini Ottawa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada, Mhe. Melanie Joly akizungumza na Mabalozi wa Afrika waliopo nchini humo uliofanyika hivi karibuni jijini Ottawa



 

Monday, June 3, 2024

MKUTANO WA BARAZA LA KISEKTA LA MAWAZIRI LINALOSHUGHULIKIA MASUALA YA EAC NA MIPANGO WAANZA ARUSHA


Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Benjamini Mwesiga akichangia hoja kwenye Mkutano 33 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango ngazi ya Wataalam unaofanyika jijini Arusha

Mkutano 33 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango umeanza leo tarehe 3 Juni 2024 jijini Arusha.

Mkutano huo wa siku tano kuanzia Juni 3-7, 2024 umeanza kwa Ngazi ya Wataalam na na baadaye utafuatiwa na Ngazi ya Makatibu Wakuu utakaofanyika tarehe 6 Juni 2024 na kuhitimishwa na Mkutano Ngazi ya Mawaziri ukaofanyika tarehe 7 Juni 2024. 

Mkutano huo katika Ngazi ya Wataalam pamoja na mambo mengine utapokea na kujadili mapendekezo na taarifa mbalimbali za Jumuiya ikiwemo: Utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya; Mapendekezo ya kuhuisha Mipango ya Jumuiya na Mipango ya Nchi Wanachama; Taarifa ya Wakurugenzi wa Masuala ya Kazi kuhusu Ukamilishaji wa Rasimu Iliyorekebishwa ya Sera ya Uhamiaji ya Wafanyakazi wa Jumuiya.

Masuala mengine yatakayo jadiliwa ni pamoja na taratibu za Uanzishwaji wa Jukwaa la Mashauriano kuhusu Uhamaji katika Jumuiya ya Afrika Mashariki; Kuidhinisha Sera na Mkakati wa Pili wa Mawasiliano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; na Kuidhinisha Kalenda ya Shughuli za Jumuiya kwa kipindi cha Julai – Desemba 2024.

Akifungua mkutano huo Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya forodha, biashara na fedha Bi. Annette Ssemuwemba amehimiza kuhusu umuhimu wa mkutano huo katika kusimamia utekelezaji na ufanisi wa sera na mipango ya Jumuiya ili kukidhi matarajio ya Wananchi. 

“Mtakumbuka kuwa takriban miaka miwili sasa hakupata fursa ya kufanya mkutano huu, kwa sababu hiyo kwa umoja wetu tutumie fura hii hadhimu kujadili na kutafuta majawabu yatakayotupa uelekeo mpya na sahihi wa kutekeleza na kusimamia kwa ufanisi sekta mbalimbali ikiwemo bishara na fedha kwa maendeleo ya Jumuiya yetu” Alieleza Bi. Annette Ssemuwemba

Vilevile mkutano huo unatarajiwa kufanya tathimini ya hatua iliyofikiwa kwenye utekelezaji wa masuala mbalimbali yaliyoamuliwa kwenye mikutano iliyopita ikiwemo mpango wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) na Uondoaji wa Vikwazo vya Biashara visivyokuwa vya kikodi,.

Mkutano huo umehudhuriwa na nchi zote Wanachama wa Jumuiya, huku ujumbe wa Tanzania ukijumuisha Mkurugenzi wa Mawasiliano Balozi Mindi Kasiga, Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Mhandisi Abdillah Mataka, na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji Bw. Benjamini Mwesiga ambaye pia ni kiongozi wa ujumbe huo, wote kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mkutano ukiendelea
Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga akifuatilia Mkutano 33 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango ngazi ya Wataalam unaofanyika jijini Arusha
Mkutano ukiendelea
Meza kuu wakiongoza Mkutano 33 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango ngazi ya Wataalam unaofanyika jijini Arusha

KAMATI YA BUNGE YA NUU YASISITIZA UWAJIBIKAJI


Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) imeisisitiza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi yake kwa wakati iliyo katika hatua mbalimbali.

 

Msisitizo huo umetolewa katika kikao cha ufuatiliaji kati ya kamati hiyo na Menejimenti ya Wizara kilichofanyika Bungeni jijini Dodoma, tarehe 3 Juni 2024.

 

Akiwasilisha taarifa ya miradi ya ujenzi iliyo chini ya Wizara, Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato (Mb.), kwa niaba ya Mhe. January Makamba (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ameeleza kuwa, Wizara imewekeza nguvu kubwa katika kuhakikisha mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Wizara lililopo mji wa Serikali Mtumba, Dodoma na jengo la mihadhara la Kituo cha Uhusiano cha Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim kilichopo Kurasini, jijini Dar es Salaam yanakamilika kwa wakati.

 

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya NUU na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Mhe. Vita Kawawa (Mb.) alieleza juu ya umuhimu wa Wizara kushirikiana na Kamati hiyo katika kutekeleza majukumu yake.

 

Aidha, wajumbe wa Kamati wamepongeza jitihada zilizofanywa na Wizara katika utekelezaji wa miradi na wamesisitiza weledi katika usimamizi wa matumizi ya kifedha na mikataba ya miradi ya ujenzi.

 

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amewashukuru wajumbe wa Kamati ya NUU kwa kuendelea kuwa chachu katika usimamizi wa miradi inayotekelezwa na Wizara. Pia, amewaalika Wajumbe wa Kamati hiyo kutembelea mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu unaotekelezwa katika eneo la Lakilaki, Arusha.

========================================

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Mhe. Vita Kawawa (Mb.) akifungua kikao cha kamati yake na Menejimenti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kilichofanyika tarehe 3 Juni, 2024 Bungeni, jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (Mb.) akiwasilisha taarifa ya Wizara ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi kwa kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama tarehe 3 Juni, 2024 Bungeni, jijini Dodoma.

Mhe. Byabato akiteta jambo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Dkt. Samwel Shelukindo (Kulia) pamoja na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Eng. John Kiswaga (kati).

Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) wakifuatilia kikao.

Sehemu ya Menejimenti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikifuatilia kikao.

Sehemu nyingine ya Ujumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikifuatilia kikao.

Kikao kikiendelea.