Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Kikao cha Pamoja cha Kamati Ndogo ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuhusu masuala ya Siasa na Diplomasia kilichofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 10 Juni 2024.
Akifungua kikao hicho ambacho kimefanyika kwa ngazi ya Makatibu Wakuu , Mwenyekiti ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Zambia, Bi. Etambuyu Gundersen aliwataka wajumbe kujadili na kutoa mapendekezo katika agenda mbalimbali zilizowasilishwa kwao ili hatimaye mapendekezo hayo yawasilishwe kwenye kikao cha Mawaziri kitakachofanyika mwezi Julai 2024 kwa ajili ya kuridhiwa.
Akichangia hoja kwenye kikao hicho, Balozi Shelukindo amezishukuru na kuzipongeza Nchi Wanachama wa SADC kwa kufanikisha uundwaji na uzinduzi wa Sanamu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere uliofanyika mwezi Februari 2024 katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Amesema uzinduzi huo ambao ulihudhuriwa na idadi kubwa ya wakuu wa nchi wa Afrika ulidhihirisha namna ambavyo wanaenzi mchango mkubwa uliotolewa na Hayati Mwalimu Nyerere kwenye Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika.
Kadhalika amesema Tanzania inaendelea na mawasilianao ya ndani ili kukamilisha Mpango wa Taifa wa Utekelezaji wa Azimio la Umoja wa Mataifa Namba 1325 kuhusu kuwawezesha Wanawake kushiriki katika juhudi za kutatua, kuzuia na kudhibiti migogoro duniani huku akizipongeza nchi zilizokamilisha Mpango huo ikiwemo Zimbawe na Madagascar.
Vilevile, ametumia fursa hiyo kuzipongeza Jamhuri ya Afrika Kusini na Jamhuri ya Madagascar kwa kufanikisha uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge uliofanyika kwenye nchi hizo kwa amani na utulivu tarehe 29 Mei 2024 mtawalia.
Amesema, kikanda uchaguzi katika nchi hizi mbili umeakisi viwango vya kimataifa vya demokrasia pamoja na kanuni na miongozo ya SADC kuhusu uchaguzi unaofuata misingi ya demokrasia.
Kikao hicho ambacho kimefanyika kwa ajili ya kuandaa mkutano wa Mawaziri unaotarajiwa kufanyika mwezi Julai 2024, kimehudhuriwa na Nchi za Tanzania, Lesotho, Eswatini, Botswana, Angola, Namibia, Afrika Kusini, Shelisheli , Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia na Zimbabwe.
Kikao kikiendelea |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.