Wataalam
wa sekta ya afya kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana
jijini Arusha katika kikao cha maandalizi ya Mkutano wa Saba (7) wa Dharura wa
Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Afya utakaofanyika kesho tarehe 14 Juni, 2024
na kutanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu.
Mkutano
huu wa wataalamu pamoja na masuala mengine utapitia na kujadili pendekezo la Tanzania la kuanzisha vituo viwili vya umahiri ambavyo ni: Kituo cha
Umahiri cha Sayansi ya Afya ya Kinywa chini ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi
Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Uloto na
Sayansi ya Matibabu ya Magonjwa ya Damu chini ya Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Akifungua
mkutano huo Mkurugenzi wa Sekta ya Jamii kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki, Dkt. Irene Isaka ameeleza kuwa kupitia mkutano huu wajumbe
watachangia na kushauri juu ya umuhimu wa vituo hivyo viwili vya umahiri
ambavyo vinachangia utoaji wa huduma za kibingwa za afya pamoja na mafunzo katika
kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Naye Mwenyekiti
wa mkutano wa Wataalam kutoka Jamhuri ya Sudan Kusini, Mhandisi Ring Dut katika
hotuba yake ya ufunguzi ameeleza kuwa kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa
COVID-19 kumeleta somo katika ukanda wa Afrika Mashariki hususan katika suala
la kujijengea uwezo wa kujitegemea katika masuala ya huduma za afya, uanzishaji
wa programu saidizi na uimarishwaji wa miundombinu katika sekta hiyo.
Ujumbe
wa Tanzania katika Mkutano Ngazi ya Wataalam umeongozwa na Kaimu Mkurugenzi
Idara ya Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi Abdillah Mataka ambaye
ameambatana na Wataalamu Waandamizi kutoka sekta ya Afya na Elimu.
Katika hotuba yake ya ufunguzi Mhandisi amesisitiza
umuhimu wa mkutano huo, akibainisha kuwa andiko dhana ya kuanzisha vituo vya
umahiri vilivyopendekezwa na Tanzania vitaleta mabadiliko muhimu katika mifumo
ya afya, huduma za kibingwa, mafunzo, na kujengea uwezo.
Pia, amewahimiza wajumbe kujadili na kushiriki
katika mijadala ya wazi na yenye kujenga ili kuboresha afya kwa ustawi wa watu
wa EAC, huku akitoa shukrani kwa wadau wote walioshiriki katika kuandaa
maandiko haya ya dhana.
============================================
Ujumbe kutoka Uganda |
Ujumbe kutoka Tanzania |
Sehemu nyingine ya Ujumbe kutoka Tanzania |
Picha ya pamoja |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.