Monday, June 3, 2024

MKUTANO WA BARAZA LA KISEKTA LA MAWAZIRI LINALOSHUGHULIKIA MASUALA YA EAC NA MIPANGO WAANZA ARUSHA


Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Benjamini Mwesiga akichangia hoja kwenye Mkutano 33 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango ngazi ya Wataalam unaofanyika jijini Arusha

Mkutano 33 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango umeanza leo tarehe 3 Juni 2024 jijini Arusha.

Mkutano huo wa siku tano kuanzia Juni 3-7, 2024 umeanza kwa Ngazi ya Wataalam na na baadaye utafuatiwa na Ngazi ya Makatibu Wakuu utakaofanyika tarehe 6 Juni 2024 na kuhitimishwa na Mkutano Ngazi ya Mawaziri ukaofanyika tarehe 7 Juni 2024. 

Mkutano huo katika Ngazi ya Wataalam pamoja na mambo mengine utapokea na kujadili mapendekezo na taarifa mbalimbali za Jumuiya ikiwemo: Utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya; Mapendekezo ya kuhuisha Mipango ya Jumuiya na Mipango ya Nchi Wanachama; Taarifa ya Wakurugenzi wa Masuala ya Kazi kuhusu Ukamilishaji wa Rasimu Iliyorekebishwa ya Sera ya Uhamiaji ya Wafanyakazi wa Jumuiya.

Masuala mengine yatakayo jadiliwa ni pamoja na taratibu za Uanzishwaji wa Jukwaa la Mashauriano kuhusu Uhamaji katika Jumuiya ya Afrika Mashariki; Kuidhinisha Sera na Mkakati wa Pili wa Mawasiliano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; na Kuidhinisha Kalenda ya Shughuli za Jumuiya kwa kipindi cha Julai – Desemba 2024.

Akifungua mkutano huo Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya forodha, biashara na fedha Bi. Annette Ssemuwemba amehimiza kuhusu umuhimu wa mkutano huo katika kusimamia utekelezaji na ufanisi wa sera na mipango ya Jumuiya ili kukidhi matarajio ya Wananchi. 

“Mtakumbuka kuwa takriban miaka miwili sasa hakupata fursa ya kufanya mkutano huu, kwa sababu hiyo kwa umoja wetu tutumie fura hii hadhimu kujadili na kutafuta majawabu yatakayotupa uelekeo mpya na sahihi wa kutekeleza na kusimamia kwa ufanisi sekta mbalimbali ikiwemo bishara na fedha kwa maendeleo ya Jumuiya yetu” Alieleza Bi. Annette Ssemuwemba

Vilevile mkutano huo unatarajiwa kufanya tathimini ya hatua iliyofikiwa kwenye utekelezaji wa masuala mbalimbali yaliyoamuliwa kwenye mikutano iliyopita ikiwemo mpango wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) na Uondoaji wa Vikwazo vya Biashara visivyokuwa vya kikodi,.

Mkutano huo umehudhuriwa na nchi zote Wanachama wa Jumuiya, huku ujumbe wa Tanzania ukijumuisha Mkurugenzi wa Mawasiliano Balozi Mindi Kasiga, Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Mhandisi Abdillah Mataka, na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji Bw. Benjamini Mwesiga ambaye pia ni kiongozi wa ujumbe huo, wote kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mkutano ukiendelea
Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga akifuatilia Mkutano 33 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango ngazi ya Wataalam unaofanyika jijini Arusha
Mkutano ukiendelea
Meza kuu wakiongoza Mkutano 33 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango ngazi ya Wataalam unaofanyika jijini Arusha

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.