Monday, June 10, 2024

BALOZI MUSSA AWAASA VIJANA KUWA MABALOZI WAZURI NJE YA NCHI


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa amewaasa vijana waliochaguliwa kushiriki katika programu ya mafunzo ya uongozi kwa vijana maarufu kwa jina la “Mandela Washington Fellowship for Young African Leaders” kuwa mabalozi wazuri katika mafunzo hayo yanayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 18 Juni, 2024 jijini Washington, Marekani.

Nasaha hizo zimetolewa katika hafla fupi ya kuwaaga vijana hao 26 ambayo ilihusisha makabidhiano ya bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni ishara ya kuitangaza na kuiwakilisha nchi katika heshima inayostahili iliyofanyika katika Ofisi za Wizara Mtumba, Dodoma tarehe 10 Juni, 2024.

Balozi Mussa aliwapongeza vijana hao kwa kuonesha uwezo na jitihada binafsi kuchukua nafasi ya kuomba na kufanikiwa kupita katika mchujo wa vijana wengi walioihitaji fursa hiyo. Hivyo, ni wema wakazingatia mafunzo na kuhakikisha ujuzi na elimu watakayoipata inaleta manufaa kwao na kuwajengea uwezo vijana wengine waliopo nchini.

"Hii ni programu maalum ambayo itawajengea uwezo katika masuala ya uongozi hususani, uongozi katika masuala ya usimamizi wa umma, uongozi katika usimamizi wa biashara na uongozi katika masuala ya ushirikishwaji wa jamii yakiwa ni maeneo mtambuka katika ukuaji wa nchi za Afrika.” alisema Balozi Mussa.

Pia akawaeleza umuhimu wa kuzingatia sheria na taratibu za nchi husika pamoja na kujikita katika malengo yanayowapeleka nchini Marekani ili kufanikisha kutumia fursa hiyo kujenga uwezo katika maoneo yao husika ya kiutendaji sambamba na kuijengea nchi sifa nzuri.

Aidha, amewasisitiza kuzingatia tamaduni na mila za kitanzania wawapo nchini humo kwakuwa mafunzo hayo yanahusisha mataifa tofauti hivyo ni vema kuepuka changamoto mbalimbalii za kimaadili zinazoweza kuwaharibia sifa binafsi na taifa kwa ujumla. Vilevile, katika hilo akasisitiza umuhimu wa kuwasilisha taarifa zao katika ofisi za ubalozi zilizopo jijini Washington.

Nao vijana wanaoenda kushiriki mafunzo hayo wameishukuru Serikali kwa kuendeleza kuimarisha ushirikiano mzuri na Serikali ya Marekani na hivyo kuwawezesha kushiriki kwa wingi katika mafunzo hayo ambayo pamoja na masuala mengine yatawajengea na kukuza uwezo katika teknolojia inayopatikana katika taifa hilo kubwa lililopiga hatua kimaendeleo sambamba na kukutana na wadau katika sekta husika.

Programu hii inatarajiwa kutimiza miaka 10 tangu ianzishwe mwaka 2014 ambapo imekuwa ikitoa mafunzo kwa washiriki kwa njia ya vitendo na kuingia darasani na hivyo, kuwawezesha kushiriki katika majukumu ya kijamii pamoja na kufanya ziara katika ofisi mbalimbali za umma na mashirika nchini Marekani.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akisisitiza jambo alipokuwa akiwaaga washiriki wa programu ya mafunzo ya uongozi kwa vijana(Mandela Washington Fellowship for Young African Leaders is the flagship program)yatakayofanyika nchini Marekani.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akiwa katika mazungumzo na vijana waliochanguliwa kushiriki katika programu ya mafunzo ya uongozi kwa vijana (Mandela Washington Fellowship for Young African Leaders is the flagship program) kwenye hafla fupi ya kuwaaga vijana hao iliyofanyika Mtumba, jijini Dodoma.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akiwa katika mazungumzo na vijana waliochanguliwa kushiriki katika programu ya mafunzo ya uongozi kwa vijana (Mandela Washington Fellowship for Young African Leaders is the flagship program) kwenye hafla fupi ya kuwaaga vijana hao iliyofanyika Mtumba, jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akikabidhi Bendera ya Taifa kwa vijana waliochanguliwa kushiriki katika programu ya mafunzo ya uongozi kwa vijana (Mandela Washington Fellowship for Young African Leaders is the flagship program) kwenye hafla fupi ya kuwaaga vijana hao iliyofanyika Mtumba, jijini Dodoma.
Picha ya pamoja. 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.