Monday, June 3, 2024

KAMATI YA BUNGE YA NUU YASISITIZA UWAJIBIKAJI


Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) imeisisitiza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi yake kwa wakati iliyo katika hatua mbalimbali.

 

Msisitizo huo umetolewa katika kikao cha ufuatiliaji kati ya kamati hiyo na Menejimenti ya Wizara kilichofanyika Bungeni jijini Dodoma, tarehe 3 Juni 2024.

 

Akiwasilisha taarifa ya miradi ya ujenzi iliyo chini ya Wizara, Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato (Mb.), kwa niaba ya Mhe. January Makamba (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ameeleza kuwa, Wizara imewekeza nguvu kubwa katika kuhakikisha mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Wizara lililopo mji wa Serikali Mtumba, Dodoma na jengo la mihadhara la Kituo cha Uhusiano cha Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim kilichopo Kurasini, jijini Dar es Salaam yanakamilika kwa wakati.

 

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya NUU na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Mhe. Vita Kawawa (Mb.) alieleza juu ya umuhimu wa Wizara kushirikiana na Kamati hiyo katika kutekeleza majukumu yake.

 

Aidha, wajumbe wa Kamati wamepongeza jitihada zilizofanywa na Wizara katika utekelezaji wa miradi na wamesisitiza weledi katika usimamizi wa matumizi ya kifedha na mikataba ya miradi ya ujenzi.

 

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amewashukuru wajumbe wa Kamati ya NUU kwa kuendelea kuwa chachu katika usimamizi wa miradi inayotekelezwa na Wizara. Pia, amewaalika Wajumbe wa Kamati hiyo kutembelea mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu unaotekelezwa katika eneo la Lakilaki, Arusha.

========================================

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Mhe. Vita Kawawa (Mb.) akifungua kikao cha kamati yake na Menejimenti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kilichofanyika tarehe 3 Juni, 2024 Bungeni, jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (Mb.) akiwasilisha taarifa ya Wizara ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi kwa kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama tarehe 3 Juni, 2024 Bungeni, jijini Dodoma.

Mhe. Byabato akiteta jambo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Dkt. Samwel Shelukindo (Kulia) pamoja na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Eng. John Kiswaga (kati).

Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) wakifuatilia kikao.

Sehemu ya Menejimenti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikifuatilia kikao.

Sehemu nyingine ya Ujumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikifuatilia kikao.

Kikao kikiendelea.


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.