Saturday, June 15, 2024

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA YATEMBELEA MRADI WA UJENZI WA MAHAKAMA YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU NA WATU


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imefanya ziara jijini Arusha leo tarehe 15 Juni, 2024 ili kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.


Baada ya kuwasili Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Vita Kawawa aliyeambatana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa walipokelewa na  Makamu wa Rais wa Mahakama hiyo, Mhe. Jaji Modibo Sacko.


Kufuatia umuhimu wa ziara hiyo kamati ilianza ziara kwa kufanya kikao na menejimenti ya Mahakama kilichoongozwa na Mhe. Jaji Sacko akiwa na mwenyekiti mwenza Mhe. Vita Kawawa.


Akiongea katika kikao hicho Mhe. Jaji Modibo Sacko ameishukuru Kamati ya Bunge kwa kuendelea kuipigania Bungeni Mahakama hiyo hususan katika kupata fedha za Maendeleo zinazowezesha kuendelea kwa ujenzi na kuwa na mazingira mazuri ya kufanyia kazi.


Naye Naibu Katibu Mkuu Mambo ya Nje, Balozi Mussa ameipongeza Mahakama kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kusimamia Haki za Watu kila inapotakiwa kufanya hivyo kulingana na itifaki ya uanzishwaji wake.


"Kamati imefanya ziara ili kujionea hatua iliyofikiwa katika ujenzi na pia tunashukuru kwa kuwa na kamati imara katika usimamizi wa majukumu hivyo, niwaondoe hofu kuwa Wizara itaendelea kusimamia ujenzi unaoendelea pamoja na kuzingatia thamani ya fedha," alisema Balozi Mussa .


Akiwasilisha salamu za  shukrani Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Kawawa ameeleza kuwa Kamati yake inatambua umuhimu na majukumu makubwa yanayolotekelezwa na Mahakama hiyo katika kuimarisha haki barani Afrika, hivyo Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.


Mara ya mwisho Kamati ya Mambo ya Nje, ulinzi na Usalama kutembelea ujenzi wa mradi wa Mahakama hiyo ilikuwa mwezi Machi, 2023. Hata hivyo, wabunge hao kwa umoja wao wametoa pongezi kwa hatua nzuri ya ujenzi iliyofikiwa na kusisitiza usimamizi makini.


Mradi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ulianza ujenzi mwezi Agosti, 2023 na unatarajiwa kumalizika mwezi Februari, 2025 na utagharimu takriban shilingi za Kitanzania Millioni 22.97.

======================================

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa akisisitiza jambo wakati wa kikao cha kamati yake na menejimenti ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu wakati walipofanya ziara ya kutembelea mradi wa ujenzi wa Mahakama hiyo tarehe 15 Juni, 2024 jijini Arusha.
Naibu Katibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akieleza nia ya dhati ya Wizara ya kuhakikisha inasimamia utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu unaoendelea jijini Arusha wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ilipofanya ziara katika Mahakama hiyo tarehe 15 Juni, 2024 jijini Arusha.

Makamu wa Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Mhe. Jaji Modibo Sacko akiishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ilipofanya ziara katika Mahakama hiyo jijini Arusha tarehe 15 Juni, 2024.

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu na Utawala katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi John Kiswaga akiwasilisha taarifa ya hali ya utekekelezaji wa ujenzi wa mradi wa Mahakama katika kikao hicho.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama wakipata ufafanuzi kutoka kwa msiamamizi wa ujenzi wa mradi huo.

Mhe. Kawawa akitoa ufafanuzi kwa wasimamizi wa mradi wa ujenzi wa Mahakama baada ya kukamilisha kupata taarifa ya hali ya utekelezaji wa mradi huo.

Mhe. Jaji Sacko akimvisha Mhe. Kawawa nembo ya Mahakama hiyo ikiwa ni ishara ya shukrani kwa mchango mkubwa unaotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama katika utekelezaji wa majukumu ya Mahakama hiyo.
Mhe. Jaji Sacko akimvisha Balozi Said Shaib Mussa nembo ya Mahakama hiyo ikiwa ishara ya shukrani kwa ushirikiano mkubwa unaotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kufanikisha majukumu ya Mahakama hiyo.


Picha ya Pamoja





No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.