Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)
wamekutana jijini Arusha kwa kikao cha siku tatu (3) kuanzia tarehe 25 hadi 27
Juni, 2024 ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa 45 wa Kawaida wa Baraza la
Mawaziri wa Jumuiya hiyo utakaofanyika tarehe 28 Juni 2024.
Mkutano huo wa Makatibu Wakuu ulitanguliwa na mkutano wa
wataalam uliofanyika tarehe 22 hadi 24 Juni, 2024 umepokea na kupitia taarifa
na mapendekezo yaliyowasilishwa na Mkutano wa wataalam kuhusu masuala
mbalimbali ya kikanda yatakayowasilishwa
kwenye Mkutano wa Baraza la Mawaziri.
Masuala ya kikanda yaliyojadiliwa ni taarifa ya utekelezaji
wa maamuzi mbalimbali yaliyofikiwa na baraza hilo kwenye vikao vilivyopita,
taarifa kuhusu masuala ya forodha na biashara na taarifa ya miundombinu, sekta
za uzalishaji, sekta za jamii na masuala ya kisiasa.
Taarifa nyingine ni taarifa ya kamati na fedha, taarifa ya
kamati ya rasilimali watu, taarifa ya mkutano wa Makatibu Wakuu uliofanyika
tarehe 17 Mei, 2024 pamoja na taarifa ya ratiba za matukio ya jumuiya ya Afrika
Mashariki kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba, 2024.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa Makatibu Wakuu
umeongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki - anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi
ambaye ameambatana na, Naibu Katibu Mkuu, Afisi ya Rais Kazi, Uchumi na
Uwekezaji (Uchumi na Uwekezaji) Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw. Rashid Ali
Salim, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya
Viwanda na Biashara, Balozi Dkt. John Simbachawene
Viongozi wengine ni, Mkurugenzi wa Uendelezaji Sera kutoka
Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Cyrus
Kapinga, Kamishna Msaidizi Utafiti kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Kanali Bonus Nombo, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Uwekezaji Sekta Binafsi
Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Bw. Fadhili Chilumba na Kaimu Mkurugenzi
Idara ya Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Kijamii, Mhandisi Abdillah
Mataka.
======================================
Naibu Katibu Mkuu, Afisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji
(Uchumi na Uwekezaji) Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw. Rashid
Ali Salim na Mkurugenzi wa Uendelezaji Sera kutoka Ofisi ya Rais –
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Cyrus
Kapinga wakifuatilia majadiliano.
Mwenyekiti wa mkutano wa Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki na Katibu Mkuu - Ofisi ya Rais, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Sudan Kusini, Mhe. Beny Gideon Mabor (kati) akiongoza majadiliano ya mkutano huo. Kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Miundombinu, Sekta za Uzalishaji, Kijamii na Siasa, Mhe. Andrea Aguer Ariik Malueth na kulia kwake ni Mwenyekiti wa mkutano wa Maafisa Waandamizi kutoka Jamhuri ya Sudan Kusini, Bw. Eulwango Ugo. |
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania ikifuatilia mkutano.
Ujumbe kutoka Uganda ukifuatilia mkutano. |
Ujumbe kutoka Kenya na Rwanda ukifuatilia mkutano. |
Ujumbe kutoka Burundi. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.